Jeshi
la Polisi jana liliwahoji Mhariri Mtendaji wa Mwananchi, Frank Sanga na
mwandishi wa habari, Elias Msuya kuhusu makala iliyochapishwa juzi
kuhusu utendaji wa jeshi hilo.
Baada ya mahojiano yaliyofanyika kwa muda tofauti, waliachiwa kwa dhamana na kutakiwa kuripoti kituoni hapo leo asubuhi.
Msuya ndiye aliyeanza kuhojiwa baada ya juzi jioni kupigiwa simu na maofisa wa polisi akitakiwa kufika Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam kuhojiwa kutokana na makala yake ya uchambuzi yenye kichwa cha habari “Polisi na hofu ya watawala kuondoka madarakani.”
Makala
hayo yalichapishwa katika gazeti hilo toleo la Julai 13 na mwandishi
huyo alieleza mambo mbalimbali yanayohusu utendaji wa jumla wa jeshi
hilo kwa wananchi.
Baada ya kutoa maelezo kwa saa mbili, maofisa hao
walimpigia simu Sanga na kumtaka afike kituoni hapo kwa ajili ya
kuhojiwa kuhusu makala hiyo.
“Wamenihoji maswali mbalimbali
kuhusiana na makala niliyoandika. Nimewajibu kulingana na jinsi
walivyokuwa wakiniuliza,” alisema Msuya.
Msuya alifika katika kituo
hicho saa moja asubuhi na kukaa kwa saa mbili kabla ya kuanza kuhojiwa
na kisha Sanga ambaye alifika kituoni hapo mchana na kuhojiwa kwa dakika
90.
Akizungumzia suala hilo, Mhariri Mtendaji Mkuu wa Mwananchi
Communications Ltd (MCL), Bakari Machumu alisema baada ya wito huo wa
polisi, kampuni imetoa ushirikiano wa kutosha kwa kuwaruhusu Sanga na Msuya kwenda kutoa maelezo polisi.
Alisema
ni vyema masuala yanayohusu habari ambazo zinatakiwa kutolewa ufafanuzi
yakaihusisha Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Baraza la
Habari Tanzania (MCT).
“Nadhani jambo kama hili kuchukuliwa moja
kwa moja na polisi ni kama kuingilia uhuru wa habari. Vipo vyombo
vinavyoweza kutoa ufafanuzi wa habari iliyoripotiwa na vyombo vya
habari,” alisema Machumu.
Baada ya mahojiano hayo, Sanga na Msuya waliachiwa kwa kila mmoja kudhaminiwa na mtu mmoja.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment