Makamu
wa Rais wa Marekani Joe Biden ameunga mkono hatua ya Uturuki kuingia
kijeshi ndani ya Syria, kulipiga vita kundi la Dola la Kiislamu-IS.
Biden pia amesema wanashirikiana na Uturuki juu ya kumrejesha Gulen.
Makamu
wa rais wa Marekani Joe Biden ambaye amefanya ziara nchini Uturuki,
akizungumza baada ya kukutana na waziri mkuu wa Uturuki Binali Yildirim
amesema nchi hiyo haina rafiki yeyote mkubwa kuliko Marekani, na kuunga
mkono juhudu ya utawala wa rais Recep Tayyip Erdogan katika kuupiga vita
ugaidi.
Amesema, ''Ndio sababu niko hapa bwana waziri mkuu, kwa
sababu tutasimama bega kwa bega katika kuwapiga vita wale wanaounia
kukwamisha demokrasia yetu, na serikali zetu zilizochaguliwa na
wananchi. Tutaendelea kupigana pamoja, dhidi ya ugaidi nchini Syria na
Iraq''.
Ingawa serikali mjini Damascus imepinga kuingia kijeshi kwa
Uturuki ndani ya eneo lake, waasi kwa upande wao wameikaribisha hatua
hiyo. Muungano wa Upinzani wenye makao yake mjini Istanbul umetoa
tangazo ukisema operesheni hiyo ni uungaji mkono wa juhudi ambazo tayari
wanazifanya.
Uwezekano wa kumrejesha Fethullah Gulen.
Mbali na
masuala yanayohusu vita vya Syria, ziara ya makamu wa rais wa Marekani
pia iliazimia kuukarabati uhusiano kati ya nchi yake na Uturuki, ambao
umetiwa doa na kuwepo nchini Marekani kwa Ulamaa wa kituruki Fethullah
Gulen, ambaye Uturuki inamtuhumu kupanga jaribio la mapinduzi
lililoshindwa la tarehe 15 Julai.
''Wataalamu wetu wa masuala ya
sheria, wanashirikiana na wenzao wa Uturuki hivi sasa, kuandaa ushahidi
unaokidhi mahitaji ya sheria zetu, kuhusiana na mkataba wa kurejesheana
watuhumiwa, ili kumrejesha Gulen. Na tutaendelea kufanya hivyo, kadri
mnavyozidi kutoa maelezo zaidi''. Amesema Biden.
Syria yapinga 'uchokozi' wa Uturuki.
Tangazo
lililotolewa na wizara ya mambo ya nchi za nje ya Syria imetaka
kumalizika haraka kwa kile ilichokiita uchokozi wa Uturuki, unaofanywa
katika ardhi ya Syria kwa kutumia vifaru na magari ya kijeshi, kwa
kusaidiwa na ndege za kivita za muungano unaoongozwa na Marekani.
''Upande
wowote unaotaka kuwapiga vita magaidi kwenye ardhi ya Syria, unapaswa
kufanya hivyo kwa ashirikiano na serikali ya Syria na jeshi lake, ambalo
limekuwa likiyapiga vita makundi ya kigaidi kwa miaka 5 iliyopita'',
limesema tangazo hilo la wizara ya mambo ya nchi za nje, na kuongeza
kuwa kuliondoa kundi la IS na katika nafasi yake wakawekwa magaidi
wanaoungwa mkono na Uturuki, sio vita dhidi ya ugaidi.
Operesheni ya
kijeshi ya Uturuki iliyopachikwa jina la ''Ngao ya Euphrates'' imeanza
kabla ya mapambazuko leo, ikitajwa kuwa na lengo la kuwafurusha
wapiganaji wa IS kutoka mji wa Jarablus wanaoudhibiti, na pia kulisaka
kundi la wanamgambo wa kikurdi lijulikanalo kama PYD.
Mvutano huu
mpya kati ya Uturuki na kundi la IS umeibuka baada ya makombora kurushwa
ndani ya Uturuki, kutokea mji wa mpakani ndani ya Syria, ambao uko
mikononi mwa kundi hilo.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)


0 comments:
Post a Comment