MOJA ya mbinu inayotumiwa na nyota mbalimbali wa muziki duniani ni
ile ya kutengeneza bifu bandia na kuwahusisha mashabiki wao. Mbinu hiyo
inasaidia kuuza idadi kubwa ya nakala za kazi za sanaa za wasanii hao
wenye bifu.
Asikwambie mtu! Hapo ndipo wasanii wengi wanapiga hela. Wakati
mashabiki wanatupiana vijembe vilivyojaa kejeli za hapa na pale kuhusu
bifu hilo bandia, ndiyo kazi za wasanii hawa zinapopata nafasi sokoni.
Hali hiyo inafanya wasanii wengine na kazi zao kutopewa nafasi ya
kujadiliwa kama wanavyojadiliwa wasanii waliopo kwenye bifu hilo bandia
lenye lengo kuwanufaisha kibiashara na mara nyingi uhodari wao wa kuunda
bifu hufanya mashabiki wasijue kama ni bifu kweli au ni bifu la
magumashi.
Ukiizungumzia Bongo Fleva hivi sasa akili yako moja kwa moja itagota
kwa vijana wawili, Ali Kiba na Diamond Platnumz. Sababu inayofanya
uwafikirie wasanii hao ni kile kinachoitwa bifu lililochukua miaka
minne na zaidi sasa.
Hapo ndiyo unaona Ali Kiba akifanya vyema kwenye biashara yake ya
muziki na Diamond Platnumz akinufaika vilivyo na bifu hilo pale anapotoa
kazi mpya.
CHANZO CHA BIFU LAO
Watu wao wa karibu wanasema chanzo kilianza mwaka 2012 pale ambapo
Diamond alitakiwa ashiriki kwenye wimbo wa Single Boy ulioimbwa na Ali
Kiba.
Lakini haikuwa hivyo kwani nafasi ya Diamond aliichukua Lady Jay Dee,
kitendo kilichomchukiza Diamond na kufikia hatua ya kufuta sauti ya Ali
Kiba kwenye wimbo aliomshirikisha.
WADAU WAWATULIZA
Unaweza ukashangaa ishu ndogo kama hiyo imewezaje kufanya wawili hawa
wawe kwenye bifu mpaka leo hii. Washkaji zao wa karibu wanasema mara
nyingi watu wenye heshima kwenye muziki huu wamewaita na kuwapatanisha
bila jitihada hizo kuzaa matunda kwani tayari faida ya bifu lao walianza
kuziona.
Hata pale wadau wakuu wa muziki huu walipofanikiwa kupunguza makali
ya hasira zao, walishindwa kuzuia hasira ya uzalendo iliyojengeka kwenye
mioyo ya mashabiki wao waliotengeneza timu zenye nguvu yaani Team Kiba
na Team Diamond.
KAZI KUBWA ZA TIMU
Baada ya mashabiki kuunda timu sasa ni mwendo wa kushindana na
kukomoana. Kazi ya timu ni kuhakikisha msanii wao anapotoa audio au
video basi timu ni lazima ipigane ihakikishe inafika mbali.
Diamond akitoa audio au video basi mashabiki wa Ali Kiba watatumia
mapungufu yaliyopo kwenye kazi hiyo, kukosoa ngoma ya Diamond, kadhalika
kwa Ali Kiba. Kumbuka wakati mashabiki wa Diamond wanaiponda kazi ya
Ali Kiba, mashabiki wa Ali Kiba wanaitetea na kufanya mjadala mzito
kuibuka na kugonga vichwa vingi vya habari.
Kiukweli wamefanikiwa na ndiyo maana kama wewe ni msanii ukitoa wimbo
siku moja na Diamond au Ali Kiba, basi kazi hiyo haitafika popote
itakufa mapema iwezekanavyo.
MAPENZI YANOGESHA BIFU
Diamond aliwahi kutoka kimapenzi na Jokate Mwegelo. Inasemekana hivi
sasa Jokate anatoka na Kiba. Mashabiki hawakosi neno kwani wale
mashabiki wa Diamond watauponda uhusiano wa Kiba na Jokate kadhalika wa
Kiba wanauponda uhusiano wa Diamond na Zari kwa kigezo cha kuzidiana
umri.
Mrembo yeyote aliyewahi kutoka na Diamond, akionekana amepiga picha
na Ali Kiba basi habari yake siyo ndogo hapa mjini, mfano ni Wema
Sepetu.
SHOO, MATUKIO YA KIJAMII
Mashabiki wa Diamond wapo tayari kulipa kiingilio ili wakaharibu
onesho la Ali Kiba, hivyohivyo Diamond anapata sana shida anapokutana na
nyomi lililojaa mashabiki wa Ali Kiba, tujikumbushe kwenye Fiesta 2014
pale Leaders Club.
Juzi kati hapa Diamond alikwenda kusaidia watoto wenye ugonjwa wa
mgongo wazi na vichwa vikubwa, habari ikawa kubwa zaidi pale Ali Kiba
naye alipokwenda kutoa msaada wa milioni 21 zaidi ya Diamond aliyetoa
milioni 20.
SIKIA HII
Mfano leo hii Ali Kiba na Diamond Platnumz wanamaliza tofauti zao,
wakapeana mikono na kufanya kazi pamoja, wewe shabiki utakuwa na hamu ya
kuendelea kuwafuatilia?
Na ujue kuwa wewe shabiki usipotia mzuka wako na biashara yao ya muziki inayumba na tunaweza kuwapoteza kabisa wawili hawa.
Hapo ndipo ninaposema bifu hili ndiyo uhai wa biashara yao ya muziki.
Wakija kupatana hakuna cha Chibu Dangote wala King Kiba, huo utakuwa
mwisho wa zama zao.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)


0 comments:
Post a Comment