VIONGOZI wa vyama vya siasa wanaounda Klabu ya Viongozi wamesema
hawaungi mkono maandamano yaliyopangwa na Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema) katika kulinda amani ya nchi.
Mwenyekiti wa klabu hiyo, Fahmi Dovutwa alisema uamuzi wa kutounga
maandamano hayo imefikiwa kwenye kikao cha viongozi wa vyama wa siasa wa
klabu hiyo waliokutana jana kujadili hali ya siasa nchini.
“Vyama vya siasa tumekutana leo (jana) ili kufanya tafakari juu ya
hali ya siasa nchini hususan tamko la Chadema la kufanya maandamano na
hatimaye mikutano sehemu mbalimbali. Pia tumezingatia tamko lililotolewa
na Serikali na Rais John Magufuli la kutaka amani ya nchi idumishwe,
hivyo hatuungi mkono maandamano,” alisema.
Alisema pamoja na kutounga mkono, viongozi hao wanataka kufanyika kwa
mkutano ambao utashirikisha vyama vyote vya siasa nchini ili kupata
muafaka ambao utaepusha nchi kuingia katika malumbano na misuguano.
“Tarehe waliyopanga kufanya hayo maandamano ni maadhimisho ya Siku ya
Majeshi Duniani kote, hivyo wanajeshi watakuwa na shughuli zao ambazo
zinaweza kuleta taswira ya jeshi kuingilia maandamano, lakini jambo la
msingi ni kurudi kwenye meza ya mazungumzo kwa vyama vyote,” alisema
Dovutwa.
Vyama vilivyohudhuria mkutano huo ni Chama cha Sauti ya Umma (SAU),
Alliance For Tanzania Farmers Party (AFP), Chama cha Democratic (DP),
D-Makini, JAHAZI Asilia, Chama cha Union for Multiparty Democracy (UMD),
United Peoples Democratic Party (UPDP), ADA-TADEA na Chama Cha Kijamii
(CCK). Hivi karibuni, Chadema ilitoa tamko la kufanya maandamano na
mikutano nchi nzima katika kampeni waliyoiita Umoja wa Kupambana na
Udikteta Tanzania (UKUTA).
Azma ya Chadema inakuja baada ya siku kadhaa za Jeshi la Polisi
kuzuia mikutano ya hadhara na maandamano kwa sababu za kiusalama. Hata
hivyo, Rais Magufuli alipiga marufuku maandamano hayo kwa lengo la
kutaka amani ya nchi idumishwe na kuelekeza mikutano ya hadhara ya
wabunge walioshinda ifanywe kwenye majimbo yao.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)


0 comments:
Post a Comment