RAIS Dk. John Magufuli, sasa amegeukia utumbuaji majipu ndani ya
Chama Cha Mapinduzi (CCM), huku akituma salamu kwa viongozi wa chama
hicho ngazi ya taifa, mikoa, wilaya, kata na matawi.
Kutokana na hali hiyo, amesema hivi sasa mafisadi ndani ya CCM hawana
nafasi na anataka kukirudiusha chama hicho kwenye misingi ya uadilifu
na nidhamu, kama ilivyokuwa enzi za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius K.
Nyerere.
Kauli hiyo aliitoa jana jijini Mwanza, alipokuwa akihutubia mamia ya
wananchi katika Uwanja wa Furahisha, ambapo alisema ili kuhakikisha
nidhamu inarudi ndani ya CCM mali zote za chama hicho zitakaguliwa ili
mapato yake yaweze kujulikana na si kuwaachia viongozi wachache ambao
wamekuwa wakizitumia kwa masilahi yao binafsi.
Rais Magufuli, alisema hawezi kuhamasisha wananchi wawe na nidhamu
wakati chama chake hakina nidhamu jambo ambalo atahakikisha analirudisha
kwa nguvu zake.
“Napenda niongoze chama ambacho mali na majengo yake yanajulikana na
si kuongoza chama ambacho haujui kinaingiza mapato kiasi gani, lazima
ifike mahali turudishe hadhi ya chama kama ilivyokuwa enzi za Mwalimu
Nyerere na si kuwaachia watu wachache wagawane fedha za chama.
“Mafisadi hawako ngazi za chini ila wapo katika ngazi za mikoa na
taifa sasa nawaambia wajiandae. Naomba niseme kuwa, mafisadi hawana
nafasi ndani ya CCM… tayari wameshaanza kuondoka.
“…. waache waende na wakirudi watakuwa wamekatika mikia, siwataki
watu ambao mchana wapo CCM na usiku wanahamia chama kingine, waondoke tu
ni bora tubaki wachache ambao ni waadilifu ili tuendelee kutawala kwa
sababu Watanzania wanahitaji maendeleo na si vyama,” alisema Magufuli.
Alisema analazimika kuchukua hatua hiyo ndani ya chama baada ya
kuonekana mafanikio ndani ya Serikali ambayo kwa sasa imedhamiria
kurudisha nidhamu kwa viongozi.
“Hizi fedha za majengo ya chama zingekuwa zinakusanywa, wanachama
mngeweza kugawana walau mara mojamoja…, bahati nzuri nimekuwa mwenyekiti
sasa ni lazima wanachama muanze kuhoji kwenye vikao vyenu haya mapato
na wakiwauliza nani anawapa jeuri ya kuwahoji waambieni mwenyekiti,”
alisema.
Alisema CCM Mkoa wa Mwanza inalo jengo la ghorofa sita ambalo
limepangishwa maduka makubwa lakini ukiuliza gharama za upangishaji
huwezi kupata gharama sahihi kwa kuwa wamekuwa wakiandika Sh 50,000 na
wakati mwingine gharama halisi ni Sh 300,000.
Alisema lazima wasimamie mali za chama na kuonya kuwa chini ya
uongozi wake kamwe viongozi watakaowania nafasi mbalimbali katika
uchaguzi wa chama watakaobainika kutoa rushwa atawakata majina yao ili
kuwaengua kugombea.
Kutokana na hali hiyo alisema mafisadi wakae chonjo kwani atawatia
mbaroni na kuwafikisha kwenye mikono ya sheria ili rasilimali za
Watanzania ziendelee kudumu.
Alisema hadi sasa Serikali imetenga Sh bilioni 1.2 kwa ajili ya
kuanzisha Mahakama ya Mafisadi ambayo itawachukulia hatua watendaji wote
watakaobainika kutumia fedha za umma vibaya.
Alisema, kutokana na hali hiyo, viongozi wanapaswa kufanya kazi na
kuwachukulia hatua wale watakaobainika kwenda kinyume na majukumu yao na
kwamba watakaobainika wanataka kuwakwamisha, wawachukulie hatua ili
waweze kukwama wenyewe.
Rungu kwa Polisi
Alisema hadi sasa Jeshi la Polisi limeweza kutimiza majukumu yake ipasavyo hasa katika uamuzi wa kupambana na majambazi.
“Kazi mliofanya ya kupambana na majambazi wale ni kubwa, nawasisitiza
anayetaka kuchezea moto muwasheni hapo hapo…tumechoka kubembelezana
lazima watu wafanyekazi na si ujambazi,” alisema.
MACHINGA
Akizungumzia kuhusu wamachinga, Rais Magufuli aliwaagiza viongozi wa
Mkoa wa Mwanza kuacha kuwaondoa wamachinga katikati ya Jiji na kuwataka
kukaa nao ndani ya kipindi cha miezi miwili au mitatu ili waweze
kuangalia sehemu nzuri ya kuwapeleka kwa ajili ya kufanya shughuli zao.
“Huwezi kuwapeleka wamachinga mlimani, wanakwenda kumuuzia nani? Hawa
ndiyo walionichagua mimi, ninaomba muwaache hapo halafu mkae na
kujadiliana nao ndani ya miezi miwili au mitatu ili mjue wapi wataweza
kwenda kufanya shughuli zao ili waweze kupata faida kwa sababu na
wenyewe wanatafuta pesa,” alisema.
Aliongeza, lakini wamachinga wanapaswa kutambua kuwa, Serikali
inataka kodi, hivyo basi wasikubali kutumiwa na wafanyabiashara wakubwa
ambao ndiyo wakwepa kodi kwa kuwapa bidhaa bila ya stakabadhi hali
inayoweza kusababisha kukamatwa.
“Mkienda kununua bidhaa lazima wawape risiti ya EFD, kwa sababu
wafanyabiashara wamekuwa na tabia ya kuwapa bidhaa zao na kwenda kuuza
huku wakijua kuwa wanakwepa kodi,” alisema.
Simon Group kuchunguzwa
Kiongozi huyo wa nchi alimwagiza Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John
Mongella, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. CharlesTizeba pamoja na
vyombo vya ulinzi na usalama kuzirejesha mali za Chama Kikuu cha
Ushirika cha Nyanza (NCU LTD) kikiwemo Kiwanda cha New Era kilichouzwa
kwa Kampuni ya Simon Group inayomilikiwa na Simon Kisena.
Simon Group chini ya mwenyekiti wake mtendaji, Simon Kisena ndiyo
walipewa tenda ya kuendesha Shirika la Usafiri Jiji la Dar es Salaam
(UDA), ambapo suala hilo bado giza nene limetanda.
Hatua hiyo ilimfanya Rais Magufuli, kusema kuwa NCU iliwahi
kutangazwa kuwa miongoni mwa vyama vikubwa vya ushirika barani Afrika
kutokana na kufanya vizuri, lakini sasa iko hoi huku mali zake
zilizoenea kila sehemu zikiwemo Ginnery zikiuzwa kwa bei ya kutupa.
Kutokana na hali hiyo aliiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa
(Takukuru), vyombo vya ulinzi na usalama kuanza uchunguzi haraka ili
mali hizo za NCU zilizouzwa zirejeshwe huku akikitaja kiwanda cha New
Era ambacho alisema kimeuzwa kwa Simon Kisena wa Kampuni ya Simon Group
Ltd nacho kirejeshwe.
“Ninaifahamu Nyanza maana mimi nimefanya kazi New Era, sasa imeuzwa
kwa Shilingi milioni 32 badala ya Sh bilioni 1, vyombo vya usalama vipi,
Takukuru ipo sasa sijui mnachunguza nini kama siyo haya, mali zipo
nataka zirejeshwe kwa wakulima.
“Najua aliyeuziwa ni Simon Group, mimi huwa sifichi sasa nataka
mlisimamie hili na hizo mali zirejeshwe kwa wakulima kama ulivyoeleza
Mkuu wa Mkoa,” alisema Rais Magufuli.
Pamoja na hali hiyo alimtaka Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk.
Charles Tizeba, kusimamia jambo hilo huku akimuonya kutoogopa kupoteza
kura wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 kwani yeye kama Rais anavyo
viti vya ubunge na atamteua tena kushika nafasi hiyo.
Uvuvi haramu
Rais Magufuli amemuagiza Waziri Tizeba kuanzisha oparesheni ya kusaka
nyavu haramu na makokoro kwa kuyachoma moto ili kuliokoa Ziwa Victoria
kwa faida ya kizazi kijacho.
Alisema kabla ya kuwa rais aliwahi kuwa Waziri wa Uvuvi na kwamba
alichoma moto na kuteketeza makokoro hivyo kumtaka kuanzisha oparesheni
ndani ya Ziwa Victoria ikiwa ni pamoja na kukamata magari
yanayosafirisha nyavu haramu ikiwa ni pamoja na kutaifisha magari
yanayozisafirisha kuziingi hapa nchini.
Utekelezaji wa ahadi
Akizungumzia ahadi alizotoa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa
mwaka 2015, alisema alihaidi kutoa elimu bure na kwamba mara baada ya
kushinda aliamua kusaka fedha za kukamilisha mpango wake kwa kuanza
kusimamia ukusanyaji wa mapato bandarini ambako alifanikiwa kukusanya
mabilioni na kuanza mfumo wa utoaji elimu bure.
Alisema katika bajeti ya mwaka huu serikali yake imetenga fedha Sh
trilioni moja za kununulia meli moja mpya ya kubeba abiria 1000 na tani
400 za mizigo itakayotoa huduma Ziwa Victoria na ikiwa ni pamoja na
kuanza ujenzi wa reli ya kiwango cha Standard Gage.
Alisema pia kutokana na kubana matumizi na kuzuwia safari za nje ya
nchi kwa watumishi wa Serikali ameweza kupata fedha za kununulia ndege
mbili nchini Canada ambapo kwa sasa zinatarajia kuwasili mwezi Septemba
mwaka huu na kuanza kutoa huduma huku ndege nyingine ikiendelea
kutengenezwa.
Hata hivyo aliagiza mkandarasi anayeshughulika na ujenzi wa uwanja wa
ndege wa Mwanza kuendelea mara moja ili uwanja huo ukamilike na kuwa wa
kisasi utakaotoa huduma ya ndege kubwa hivyo kuufanya mji wa mwanza
kuwa kitovu cha nchi za maziwa makuu.
Mongela
Awali akizungumza kabla ya kumkaribisha Rais, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,
John Mongella alisema katika moja ya mipango yake Mkoa wa Mwanza
amedhamiria kufufua kilimo cha zao la pamba ikiwa ni pamoja na
kuhakikisha wanarejesha mali za Chama Kikuu cha Ushirika cha Nyanza
ambazo ziliuzwa kwa bei ya kutupa.
Mongella alisema NCU waliuza majengo yake manne likiwemo la jengo la
makao makuu ya chama hicho pamoja na hosteli za Pamba huku akibainisha
kuwa kiwanda cha New Era kiliuzwa kwa Sh milioni 32 pamoja na uuzwaji wa
viwanja vinne kwa Sh milioni 70 vyote vikiwa ni mali ya ushirika.
Mongella, alisema NCU imeliwa na sasa wameanza kusimamia urejeshaji
wa mali zake kwa kushirikiana Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk.
CharlesTizeba na kuomba awaunge mkono ili kuhakikisha mali hizo
zinarejea na ushirika unakuwa na hadhi yake.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akihutubia maelfu ya wananchi wa mkoa wa Mwanza na maeneo ya kanda ya ziwa katika mkutano wa hadhara katika uwanja wa Furahisha eneo la Kirumba jijini humo.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)

0 comments:
Post a Comment