Image
Image

Hatua zichukuliwe kuepusha mgomo wa mabasi Jumapili.

UAMUZI uliotangazwa juzi na Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa) kuwa itasitisha huduma ya kusafirisha abiria kwenda mikoa yote nchini Jumapili kwa madai ya kukagua mabasi yake, inatia shaka na unaashiria kuwa ni mgomo.

Hatua hiyo ilitangazwa na Katibu wa Taboa, Enea Mrutu, baada ya kumalizika kwa kikao cha dharura cha wamiliki wa mabasi ya mikoani na kufafanua kuwa hawatakatisha tiketi kuanzia Jumapili ili kujipa muda wa kukagua mabasi yao kama yana uwezo wa kufanya safari ama la.
Mrutu alidai kuwa wameamua kuanzia Jumapili waanze kufanya ukaguzi wa mabasi yao kote nchini ili yale ambayo hayana sifa yakae pembeni na yale yanayostahili kusafirisha abiria yafanye hivyo, badala ya utaratibu wa Serikali wa kuyafungia yote bila kujali gari lililohusika kwenye ajali.
Kauli ya Katibu wa Taboa inaonyesha dhahiri kuwa uamuzi wa kusitisha safari kwa ajili ya ukaguzi wa mabasi ni mgomo baridi kwa sababu kama lengo ni hilo, ukaguzi huo ungefanyika kwa kutumia utaratibu maalum ambao hautaathiri shughuli za usafirishaji wa abiria.
Katika kutekeleza uamuzi huo, Taboa ingeweka angalao kipindi cha mwezi mmoja kutengeneza ratiba na kila basi kupangiwa siku ya kukaguliwa badala ya kutangaza ghafla ukaguzi bila kueleza utachukua muda gani. Hivyo basi hatua hiyo itasababisha kukosekana kwa usafiri wa mabasi ya kwenda mikoani, na kusababisha athari kubwa kwa wananchi wengi.
Lingine linalotia shaka kama kweli lengo la kusitisha huduma za usafiri Jumapili ijayo ni kwa ajili ya ukaguzi wa magari, ni uamuzi huo kutangazwa sambamba na malalamiko kadhaa ya wamiliki wa mabasi hayo dhidi ya Serikali.
Malalamiko hayo ni kupinga agizo la Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra) la kuyafungia mabasi 60 ya kampuni 12 kwa makosa ya kusababisha ajali na wanataka mabasi yanayohusika pekee ndio yafungiwe.
Pia kupinga azimio la Serikali kutaka mabasi yanayosafiri masafa marefu kama mikoa ya Mwanza na Mbeya kutumia siku mbili, badala yake yatumie siku moja kama ilivyokuwa awali.
Azimio lingine ni kufunga mfumo maalum wa udhibiti wa magari (Car Track System) ambao utaunganishwa na ule wa Sumatra ili kuliona gari lilipo kwa lengo la kudhibiti ajali.
Kadhalika, Mrutu alisema wamekubaliana mabasi yote yatatembea kilometa 80 kwa saa moja na 50 pale inapohitajika kama kwenye matuta ili kuepuka ajali na pia wamekubaliana dereva atakayehusika kutembea zaidi ya mwendo waliokubaliana, afukuzwe kazi na kumchukulia hatua stahiki.
Alisema wamekubaliana mabasi yasikaguliwe kila kituo ili kuepuka kupoteza muda wakati wakisafiri kwenda mikoani ambako kunasababisha madereva kutembea mwendo kasi ili kuokoa muda waliopoteza njiani.
Tungewaelewa Taboa kama wangechukua hatua ya kuwasilisha madai hayo kwa mamlaka husika ikiwamo Sumatra na Jeshi la Polisi kupata suluhu ya kero zao, lakini hatua ya kutangaza ghafla kusitisha usafiri Jumapili haimaanishi kingine bali ni mgomo.
Sisi tunaamini kuwa hatua zilizotangazwa hivi karibuni na Jeshi la Polisi za kudhibiti kasi ya ajali za barabarani, ikiwamo kupunguza muda wa mabasi ya mikoani lengo lake ni zuri.
Tunawashuri Taboa kukutana na mamlaka husika kujadili hoja zao, lakini vilevile tunazishauri mamlaka hizo kuhakikisha mgomo huo haufanyiki ili kuepusha athari zake.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment