TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru), imeanza uchunguzi dhidi ya Kampuni ya Simon Group.
Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya Rais Dk. John Magufuli,
kuviagiza vyombo vya dola kuzirejesha mali za Chama Kikuu cha Ushirika
cha Nyanza (NCU LTD) kikiwemo Kiwanda cha New Era kilichouzwa kwa
Kampuni ya Simon Group na kurejeshwa NCU.
Akizungumza na MTANZANIA jijini Dar es Salaam jana, Mkuu wa Kitengo
cha Mawasiliano wa Takukuru, Mussa Misalaba, alisema tayari taasisi
hiyo imeanza uchunguzi dhidi ya Kampuni ya Simon Group ambayo
inamilikiwa na mfanyabishara, Robert Kisena.
Pamoja na hali hiyo Misalaba alisema, kinachofanyika sasa ni
kuainisha mambo muhimu ikiwemo kuongeza maeneo ya uchunguzi dhidi ya
mfanyabishara huyo ambaye pia anaendesha Shirika la Usafiri jijini Dar
es Salaam (UDA).
“Kuna mambo muhimu ambayo yameainishwa katika uchunguzi wetu
yanamhusu Robert Kisena ambayo yanahitaji muda zaidi ya kuyafanyia kazi
ili tuweze kujiridhisha kabla ya kumfikisha kwenye mikono mingine ya
sheria,”alisema Misalaba.
Msemaji huyo wa Takukuru, alisema suala la uchunguzi ni hatua ndefu,
hivyo basi lazima wahakikishe kuwa mambo yaliyokusudiwa yanakamilika
kabla ya kulifikisha katika vyombo vingine ikiwemo mahakamani.
Kampuni ya Simon Group chini ya Mwenyekiti wake Mtendaji, Robert
Kisena ndiyo walipewa tenda ya kuendesha Shirika la Usafiri katika Jiji
la Dar es Salaam (UDA), ambapo suala hilo hadi sasa bado giza nene
limetanda.
Mazonge kwa Simon Group
Pamoja na Rais Magufuli, kutoa agizo la kuhakikisha watu waliopora
mali za Chama cha Ushirika cha Nyanza (NCU), wanapatikana na kuzirudisha
mali hizo mara moja, huku akiitaja Kampuni ya Simon Group yenye umiliki
katika kampuni za UDA na Mabasi ya Haraka Dar es Salaam (UDA-RT), bado
kampuni hiyo imekuwa ikiandamwa na matukio mbalimbali yenye utata.
Akiwa jijini Mwanza Rais Magufuli alisema mfanyabiashara Robert
Kisena, ambaye ndiye mmiliki wa Kampuni ya Simon Group, alipewa Kiwanda
cha New Era kwa Sh bilioni moja lakini fedha aliyolipa ni Sh milioni 32
tu.
Simon Group ni kampuni iliyozaliwa na kampuni ya Simon Agency
iliyoanzishwa mkoani Shinyanga na Robert Kisena, kushughulika na ununuzi
na uchambuaji wa pamba karibu miaka minane iliyopita.
Hata hivyo kampuni hiyo imekuwa na historia ya kuingia kwenye
migogoro mikubwa ya kibiashara na vyama vikuu vya ushirika katika mikoa
ya Kanda ya Ziwa.
Vyama ilivyoingia navyo kwenye migogoro ni pamoja na Chama Kikuu cha
Ushirika cha Mkoa wa Mwanza (NCU) na Chama Kikuu cha Ushirika cha Mkoa
wa Shinyanga (SHIRECU), ambavyo vinaidai mamilioni ya fedha dhidi ya
Kisena kwa madai ya kukiuka mikataba mbalimbali, ikiwamo ya kukodi vinu
vya kuchambulia pamba na ununuzi wa rasilimali.
Mkataba wa DART
Licha ya mfanyabishara huyo kuendelea kuaminiwa na hata kudaiwa
kukingiwa kifua na baadhi ya vigogo, Serikali bado ilimfuatilia na
kunusa harufu ya ufisadi katika mkataba unaoihusisha Kampuni ya Simon
Group na Mradi wa Mabasi ya Mwendo wa Haraka (DART).
Aprili 19, mwaka huu, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa
na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene, ameeleza namna
mchezo mchafu ulivyotawala katika zabuni ya mradi huo.
Kwa mujibu wa Simbachawene, zabuni iliyotangazwa ilipaswa iwe katika
mfumo wa kimataifa, lakini katika hali ya kushangaza Kampuni ya Simon
Group ilianza maandalizi ya kuendesha mradi huo kinyume cha utaratibu.
Simbachawene, alisema Serikali ililazimika kuingilia kati suala hilo kwa lengo la kujiridhisha kuhusu zabuni hiyo.
Alisema katika hatua hiyo, Serikali ilibaini utata katika mkataba wa
kampuni hiyo, kwani kila kitu kilikuwa chini ya Simon Group ambao ni
wamiliki wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA).
“DART katika kumpata mwekezaji ilitangaza tenda kutokana na maoni
mbalimbali ambapo ilitakiwa kutangaza kimataifa (International tender),
lakini ikafanya tofauti na maoni ya watu na kuipa Kampuni ya Simon
Group kuendesha mradi huo.
“Kampuni ya Simon Group iliendelea kufanya maandalizi kwa ajili ya
mradi na sisi tukaendelea kufuatalia uhalali wa mikataba waliongia na
DART ili kuona ni jinsi gani huu mradi uanze lakini tulichokikuta pale
kila kitu kipo chini ya Kampuni ya Simon Group kwa kuwa wao ndiyo
wamiliki wa Shirika la UDA na wamenunua hisa zote za shirika hilo.
“…ndipo tulipo ulizia zile hisa ambazo haziuzwi bila wana hisa
sambamba na kutaka kujua kama fedha zimeshalipwa ndipo napo tukagundua
hakujalipwa hata senti tano na haijulikani ni nani kapokea zile hela,”
alisema Simbachawene.
Sakata la umiliki wa Shirika la Usafirishaji jijini Dar es Salaam
(UDA) ambalo limekuwa likitoa huduma za usafiri katika maeneo tofauti ya
Jiji la Dar es Salaam limechukua sura mpya baada ya kuzungumziwa ndani
ya Bunge huku Serikali ikishindwa kueleza sababu za shirika hilo
kuendeshwa na mtu binafsi.
Hata hivyo wingu dhidi ya Kampuni ya Simon Group, lilikuwa likichukua
sura mpya kila kukicha na kuibukia katika Bunge la 10 ambapo wabunge wa
Mkoa wa Dar es Salaam walihoji uhalali wa uuzwaji wake.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)

0 comments:
Post a Comment