POLISI mkoani Morogoro inawashikilia wanawake wawili, wakazi wa Mbezi
jijini Dar es Salaam, Sarafina Henry (28) na Johari Hussein (22) kwa
tuhuma za wizi wa mtoto wa kike ( jina lake limehifadhiwa) na kuishi
naye tangu mwaka 2013 hadi Agosti 7, mwaka huu.
Mtoto huyo alipoibwa, alikuwa na umri wa mwaka mmoja na nusu na
amepatikana akiwa ametimiza umri wa miaka minne na nusu, huku watuhumiwa
hao wakimwandaa kumwanzisha kusoma elimu ya awali (chekechea).
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Leonce Rwegasira alisema
jana kuwa watuhumiwa hao walikamatwa Agosti 7, mwaka huu Kawe jijini
Dar es Salaam.
Rwegasira alisema wanawake hao walimwiba mtoto huyo Julai 4, 2013 saa
11 jioni maeneo ya Karume Manispaa ya Morogoro akiwa na umri wa mwaka
mmoja na nusu.
Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi, mama mzazi wa mtoto huyo
aitwaye Ashura Shabani (33) mkazi wa Karume katika Manispaa ya Morogoro
aliripoti Kituo Kikuu cha Polisi mjini hapa kuwa mtoto wake huyo ameibwa
katika mazingira ya kutatanisha.
Akielezea tukio hilo kulingana na maelezo ya mama mzazi wa mtoto
huyo, mtoto wake aliibwa baada ya wanawake wawili waliofika nyumbani
kwake kwa ajili ya kutaka huduma za kusuka nywele.
Alisema wanawake hao walifanikisha uhalifu huo baada ya ndugu wa mama
wa mtoto huyo kwenda dukani kufuata rasta na ndipo walipomrubuni awape
mtoto wambebe na mmoja wao kumbeba na kisha kutokomea kusikojulikana kwa
kipindi chote tangu 2013 hadi Agosti 7, mwaka huu.
Akizungumzia mazingira ya kukamatwa kwa watuhumiwa hao, alisema mdogo
wa mama mwenye mtoto aliyeibwa akiwa anaishi eneo la Kawe jijini Dar es
Salaam, alimwona mwanamke mmoja akiwa amembeba mtoto anayefanana na wa
dada yake, ambaye aliibwa kipindi kirefu siku siku za nyuma.
Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi, mdogo huyo baada ya kumwona
mwanamke huyo akiwa na mtoto huyo, alikwenda kutoa ripoti Kituo cha
Polisi Kawe, ambako Askari Polisi walifanya uchunguzi na kufanikiwa
kumkamata Johari Hussein ambaye alikutwa na mtoto huyo.
Baada ya kuhojiwa kama mtoto huyo ni wake, Johari alikataa na kusema
kuwa hajawahi kuwa na mtoto isipokuwa mtoto aliyekuwa naye ni wa dada
yake, ambaye ni Sarafina na alimpeleka ili amwezesha kwenda kuandikishwa
shule ya watoto iliyopo eneo la Kawe.
Kaimu Kamanda alisema baada ya kufika nyumbani kwa dada yake huyo,
aliyekuwa amemwachia mtoto na alipohojiwa, alidai mtoto huyo alimzaa
akiwa Mwanza alipokuwa akiishi kabla ya kuhamia Dar es Salaam.
Aliongeza kuwa baada ya kuhojiwa kwa kina, mwanamke huyo alidai
hakuwa na mtoto isipokuwa mtoto huyo alitelekezwa na mama yake na yeye
aliamua kumchukua na kukaa naye kipindi chote hicho. Alisema uchunguzi
unaendelea kufanyika na kwamba watuhumiwa hao watafikishwa kwenye vyombo
vya sheria kujibu tuhuma za makosa yao.
Kwa upande wao, watuhumiwa hao walijitetea kwa nyakati tofauti, mmoja
akisema mtoto huyo aliletewa na dada yake ili amsaidie kumwandikisha
shule, wakati mtuhumiwa wa wizi wa mtoto huyo akidai alimchukua mtoto
huyo akiwa mdogo baada ya kutelekezwa na mama yake huyo na kuamua kuishi
naye kama mwanawe wa kumzaa.
Mama mzazi wa mtoto huyo, Ashura alilaani vitendo vinavyofanywa na
baadhi ya wanawake wenzao kuiba watoto, kwa kuwa ni dhambi kubwa na
matukio hayo yanawaletea majonzi na uchungu zaidi wanawake wanaotendewa
matukio hayo.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)


0 comments:
Post a Comment