MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imetengua uamuzi wa kufutwa kwa
shitaka la utakatishaji fedha linalomkabili aliyekuwa Kamishna wa
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya na wenzake na kuamuru
kesi hiyo iendelee katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Jaji Edson Mkasimongwa alitoa uamuzi huo jana baada ya kukubali hoja
za rufaa ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) na kuamuru kesi hiyo iendelee
pale ilipoishia kabla ya kutolewa kwa uamuzi huo.
Katika rufaa hiyo, DPP alipinga uamuzi wa kufutwa kwa shitaka hilo
uliotolewa na Hakimu Mkazi, Emilius Mchauru wa Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu kwa madai kuwa alikosea kusema hati ya mashitaka ina dosari.
Mbali na Kitilya, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni aliyekuwa
Miss Tanzania mwaka 1996, Shose Sinare na Mwanasheria wa Benki ya
Stanbic, Sioi Solomon.
Akisoma uamuzi huo, Jaji Mkasimongwa alisema amekubali kuwa kila
kipengele katika Kifungu cha 12 cha Sheria ya Utakatishaji Fedha
kinajitegemea kujenga kosa la utakatishaji fedha.
Aidha, alisema kutokana na hilo Hakimu Mchauru alikosea kusema hati
ya mashitaka ina dosari na hata kama ilikuwa na dosari Mahakama ilikuwa
na mamlaka ya kuamuru shitaka hilo lifanyiwe marekebisho.
Jaji Mkasimongwa alisema, Kifungu cha 129 cha Mwenendo wa Makosa ya
Jinai (CPA), kinaeleza utaratibu unaotakiwa kufuatwa pale inapoona
shitaka lina dosari na kufafanua kuwa shitaka linakuwa na dosari
zinazohitaji ushahidi kuthibitisha na jingine ni la kwenye muundo wa
hati ya mashitaka ambayo haihitaji ushahidi.
Alisema katika kesi hiyo dosari ipo kwenye muundo wa hati ambayo
haihitaji ushahidi, hivyo Mahakama ilikuwa na mamlaka ya kuamuru hati ya
mashitaka ifanyiwe marekebisho.
Aidha, alisema Hakimu aliamua kufuta shitaka bila kueleza kwa nini
hakutumia mamlaka yake kuamuru hati ifanyiwe marekebisho, hivyo alikosea
kutoa uamuzi huo.
Katika kesi hiyo, Kitilya na wenzake walikuwa wakikabiliwa na
mashitaka manane likiwemo la kutakatisha fedha ambalo lilihusisha Dola
za Marekani milioni sita.
Wanadaiwa kutenda makosa hayo katika tarehe tofauti kati ya Machi
2013 na Septemba 2015 wakati wa mchakato wa mkopo wa Dola za Marekani
milioni 550 kwa Serikali ya Tanzania kutoka Benki ya Standard ya
Uingereza.
Hata hivyo, Aprili 27, mwaka huu, Mahakama ya Kisutu iliwafutia
washtakiwa shitaka hilo baada ya upande wa utetezi kuiomba Mahakama
iliondoe shitaka hilo kwa madai lina mapungufu ya kisheria, pia hakuna
maelezo ya wazi jinsi walivyotenda kosa hilo.
DPP alikata rufaa kupinga uamuzi huo hata hivyo Mahakama Kuu iliamuru
kesi hiyo iendelee, lakini DPP alikata rufaa tena katika Mahakama ya
Rufaa kupinga uamuzi huo na mahakama hiyo ikaamuru rufaa hiyo isikilizwe
mbele ya jaji mwingine wa Mahakama Kuu.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)


0 comments:
Post a Comment