MSHAMBULIAJI mahiri wa timu ya Simba, Laudit Mavugo, amekana kuwa na
mkataba na klabu yake ya zamani ya Vital’O ya Burundi, akieleza kwamba
yeye ni mchezaji huru.
Mavugo ametoa kauli hiyo baada ya jana kuzuka taarifa kuwa klabu yake
hiyo ya zamani imedai kuwa na mkataba naye wa mwaka mmoja na imetuma
jina lake Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kama mmoja wa wachezaji
watakaokuwa nao.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Mavugo alisema kwamba alifikia uamuzi
wa kujiunga na Simba baada ya kuhakikisha kwamba amemaliza mkataba na
timu yake ya Vital’O, hivyo haoni kitakachomsumbua.
“Mashabiki wasiwe na wasiwasi kwani nilijiunga na timu ya Simba
nikiwa mchezaji huru, sina mkataba na yeyote na kama watafanya hivyo
basi ni kwa maamuzi yao wenyewe,” alisema Mavugo.
Hata hivyo, MTANZANIA lilijaribu kutafuta ukweli wa suala hili ndani
ya klabu ya Simba, ambapo lilielezwa kuwa wametuma majina ya wachezaji
waliowasajili katika Mtandao wa Usajili wa Kimataifa (TMS), ambao
kumbukumbu zake hutunzwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA),
hivyo Shirikisho hilo ndilo litaeleza kama Mavugo ana mkataba Vital’O au
la.
“Watu wa Simba wasitishwe sana na suala hili, tumetuma majina na
baada ya wiki mbili tutajua kama kweli alikuwa mchezaji huru au
alitudanganya kwa kuwa wakati huo Fifa watakuwa wakitoa hati za uamisho
kwa wachezaji wapya (ITC).
“Tumemalizana na mchezaji binafsi kuhusu mkataba, bado tunafuatilia
ukweli kuhusu madai ya klabu yake, yote yanawezekana kutatuliwa,”
kilisema chanzo hicho ambacho kilikataa kutajwa jina lake.
Awali kabla ya ujio wa nyota huyo wa Burundi katika timu ya Simba,
Rais wa Simba, Evans Aveva, alinukuliwa akisema kwamba walikosa
ushirikiano wa kutosha kutoka kwa viongozi wa Vital’O ili wazungumzie
suala la mkataba wa Mavugo.
Hata hivyo, Aveva alisema dhamira yao ni kumsajili Mavugo na wangeendelea na jitihada kuhakikisha wanafanikiwa.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)


0 comments:
Post a Comment