MBUNGE wa Singida Mashariki , Tundu Lissu (Chadema), jana alihojiwa
kwa zaidi ya saa tano na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam
kwa tuhuma za kutoa maneno ya uchochezi.
Lissu ambaye pia Mwanasheria Mkuu wa Chadema, alifikishwa katika
Kituo Kikuu cha Polisi saa 7:46 jana mchana akitokea Kituo cha Polisi
Dodoma.
Ilikuwa ni safari iliyoanzia mkoani Singida ambako alitiwa mbaroni juzi baada ya kumaliza mkutano wake jimboni kwake.
Taarifa za kukamatwa kwa Lissu na polisi mkoani Singida zilienea juzi
kupitia ujumbe uliosambazwa kwenye mitandao ya jamii, ambao ulitolewa
na Lissu na baadaye kuthibitisha na Msemaji wa Chadema, Tumaini Makene.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Thobias Sedoyeka, jana
alithibitisha kukamatwa kwa Lissu kwa kile alichoeleza kuwa alitoa
maneno ya uchochezi katika mkutano wake wa hadhara jimboni kwake.
Sedoyeka alisema Agosti 3 mwaka huu saa 9:45 alasiri Lissu,
alifanya mkutano halali wa hadhara mjini Ikungi ambako alidai alitoa
maneno ya uchochezi.
“Katika mkutano huo mbunge huyo alitoa maneno ya uchochezi kwamba
Septemba mosi watu wote wajitokeze kufanya mikutano kuunga kaulimbiu ya
kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta), na kwamba Rais Magufuli hana mamlaka
ya kuwazuia kwa sababu jukumu hilo ni la Mkuu wa Polisi wa Wilaya,”
alisema Sedoyeka.
Alisema baada ya mkutano kumalizika mbunge huyo alikamatwa na polisi
kwa madai ya kutoa lugha ya uchochezi na kufunguliwa jalada namba
CD/IR/5962/2016 katika Kituo Kikuu cha Polisi.
ALIYESAMBAZA UJUMBE ASAKWA
Sedoyeka pia ametangaza kumsaka mtu aliyesambaza ujumbe ambao
amaedai “una ishara zote za uchochezi” unaoonyesha umeandikwa na Lissu
baada ya kukamatwa na jeshi hilo.
Alisema jeshi hilo linaendelea na uchunguzi wa kina kwenye mitandao ya jamii kuhusu ujumbe huo.
Ujumbe huo ambao pia umenukuliwa na jeshi hilo katika taarifa yake,
ulieleza jinsi polisi mkoani Singida walivyomkamata Lissu baada ya
kumaliza mkutano wake wa hadhara huku akihamasisha watu kutokubali
kunyamazishwa na “Udikteta Uchwara”.
“Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa kina kwenye mitandao ya
jamii kuhusu ujumbe mfupi wa maneno uliosambazwa katika mitandao hiyo
baada ya kukamatwa kwa Lissu ukiwa na ishara zote za uchochezi…,”
alisema Sedeyoka na kuongeza:
“Katika uchunguzi huo endapo mtu yeyote atabainika kutuma taarifa
hiyo basi Jeshi la Polisi halitasita kuchukua hatua kali za sheria
zinazostahili ikiwamo kumkamata na kuwafikisha mahakamani mara moja.”
Ujumbe huo ulisomeka, “Wakubwa sana salamu. Ninawaandikieni maneno
haya nikiwa chini ya ulinzi wa polisi Singida. Nimemaliza kuhutubia
mkutano wa hadhara mji mdogo wa Ikungi ambao ni makao makuu ya jimbo la
Singida Mashariki.
“Mara baada ya kushuka jukwaani nilifuatwa na RCO wa mkoa
aliyejitambulisha kwa jina la Babu Mollel na kuniarifu kuwa ameelezwa na
RPC nikamatwe. Wakati huohuo, kuna amri ya kunikamata iliyotoka Dar es
Salaam kwa hiyo nipo nguvuni ninasubiri maelekezo ya wanapotaka
kunipeleka…
“Its likely (kuna uwezekano) nitasafirishwa Dar usiku huu. Infact ni
usiku huu kwa taarifa za sasa hivi. Kwa vyovyote itakavyokuwa ‘there is
no turning back’ (hakuna kurudi nyuma), there is no shutting up (hakuna
kufunga mdomo). Nitapambana kutetea haki yetu ya kuwasema watawala
popote nitakapokuwa.
“Whether in freedom or in jail as long as I have a voice to speak
with. (Nikiwa huru au kifungoni ilimradi nina sauti ya kuzungumza)
sitakubali kunyamazishwa na Dikteta Uchwara. Msikubali kunyamazishwa na
Dikteta Uchwara. Aluta continua!!!! From Tundu Lissu”.
Kamanda Sedoyeka alisema endapo itathibitishwa kuwa Lissu ndiye
aliyeandika na kusambaza ujumbe huo ataingia tena matatani kwa kukamatwa
na kuchukuliwa hatua za sheria kama lilivyoeleza jeshi hilo.
Hiyo ni mra ya tatu kukamtwa kwa mbunge huyo kwa kipindi cha miezi
michache na amekwisha kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu kwa tuhuma za uchochezi.
Kesi ya kwanza ni ile iliyodaiwa ametoa lugha ya uchochezi katika
habari iliyochapishwa na gazeti la Mawio na kesi ya pili ni ya kutoa
maneno ya uchochezi kwa kumwita Rais Magufuli ‘Dikteta Uchwara’
ILIVYOKUWA DAR JANA
Mapema asubuhi kabla kiongozi huyo wa Chadema hajafikishwa kituoni
hapo, baadhi ya madiwani na wenyeviti wa Chadema walikuwa wamekwisha
kuwasili kwenye eneo hilo Kituo Kikuu cha Polisi.
Saa 7:45 gari namba T 312 CWM lenye vioo vyeusi liliwasili katika
eneo hilo likiwa limembeba Lissu ambaye alikuwa na maofisa wa polisi.
Baada ya kushuka katika gari hilo, Lissu alionyesha alama ya vidole
viwili juu kwa wafuasi wa Chadema waliokuwa pembeni mwa kituoni hapo,
ambao waliitiia kwa sauti baada ya Lissu kusema ‘Peoples’ nao wakaitikia
‘Power’
“Giza haliwezi kulishinda nuru, daima nuru itang’aa gizani…. Waache
wamkamate kila mara maana wanazidi kumpaisha tu, leo tunakaa hapa hadi
kieleweke,” walisikika wakisema wafuasi hao katika eneo hilo la
polisi
Wakati wote mahojiano hayo yakiendelea, askari walisimama kila upande kuimarisha ulinzi katika eneo hilo.
Saa 9:40 alasiri, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliwasili
kituoni hapo na gari namba T. 830 DEW lakini alijikuta akigonga mwamba
kumuona Lissu baada ya kuzuiwa na askari kuingia katika eneo hilo na
kulazimika kuegesha gari lake pembeni.
LOWASSA NA MACHUNGU
Ilipotimu saa 12: 15 jioni, Waziri Mkuu wa zamani ambaye alikuwa
mgombea urais kwa tiketi ya Chadema na kuungwa mkono na Vyama
vinavyounda Umoja ya Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa naye
aliwasili kituoni hapo na gari namba T 771 DEA.
Alipofika kituoni hapo, alikwenda alipokuwa Mbowe na viongozi wengine
wa Chadema akiwamo Meya wa Kinondoni ,Boniface Jacob huku wafuasi wa
chama hicho waliokuwapo kituoni hapo wakishangilia: “Rais..rais….rais…”
Baada ya muda mfupi askari waliongezwa huku watu waliokuwa
wakishangilia wakawa wanafukuzwa kutoka eneo la kituo hicho na askari
mmoja alisikika akisema kwa sauti kuwa ‘mkusanyiko huo si halali’.
Katika kufukuzana huko, kijana mmoja ambaye hakuweza kufahamika jina
lake mara moja, alikamatwa na askari hao na kuingizwa ndani ya kituo
hicho.
Punde, gari la maji ya kuwasha liliwasili na kuegeshwa katika lango
la kuingilia kituoni hapo na baadaye liliondoka na kuanza kuzunguka
mitaa inayozunguka kituo hicho.
Saa 12:50, Mbowe na Lowassa waliingia katika magari yao na kuondoka
kituoni hapo huku ulinzi ukiimarishwa zaidi kwa kuletwa askari wenye
bunduki za zisasi za moto.
KAULI YA KIBATALA
Akizungumza na waandishi wa habari kituoni hapo, Mwanasheria wa
Chadema, Peter Kibatala, alisema Lissu ameshikiliwa kwa tuhuma za kutoa
lugha ya uchochezi na kwamba wanatarajia kesho (leo) atafikishwa
mahakamani.
“Walimkamata Ikungi Singida wakamleta hadi Dodoma akalala selo
Chamwino na kusafirishwa usiku hadi Dar es Salaam saa 7.00 mchanatulimpa
chakula na saa 9.00 mahojiano yalianza hadi saa 12.00 jioni,” alisema
Kibatala na kuongeza:
“Kwa kuwa mteja wetu wameshamshikilia kwa saa 24 tunatarajia kesho watampandisha kizimbani kumsomea shtaka lake”.
Pamoja na Kibatala mawakili wengine waliokuwapo polisi ni Wakili John Mallya na Omari Msemo.
Home
News
Slider
Lissu (Chadema), ahojiwa zaidi ya saa tano na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za uchochezi.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment