UFARANSA imesema itaongeza mchango wake katika kuendeleza sekta
mbalimbali nchini kutoka wastani wa Euro milioni 50 kila mwaka, ambazo
huzitoa kupitia shirika lake la maendeleo la AFD.
Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Maendeleo
ya Kimataifa wa Ufaransa, Jean-Marc Ayrault ambaye alifanya ziara nchini
juzi na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Dk Augustine Mahiga.
Waziri huyo akiwa nchini pia alifanya mazungumzo na Serikali ya Awamu
ya Tano ya Rais John Magufuli. Katika mazungumzo yake na Dk Mahiga,
Waziri huyo alisema uhusiano kati ya Ufaransa na Tanzania uliodumu kwa
muda mrefu utaendelea kuimarishwa.
Aidha Ayrault aliipongeza Tanzania kwa kuendelea kupigania amani na
usalama katika bara la Afrika na hasa juhudi zake za mara kwa mara za
kuhakikisha kunapatikana suluhu kwa migogoro ya nchi za Maziwa Makuu.
Aliipongeza Tanzania kwa kukubali kupokea maelfu ya wakimbizi kutoka
Burundi na kuwahifadhi na pia mchango wake katika kukabiliana na ugaidi
duniani.
Mawaziri hao pia walitambua mchango wa AFD ambayo ipo chini ya Wizara
ya Mambo ya Nje na Maendeleo ya Kimataifa ya Ufaransa kwa kutoa mikopo
kwa Tanzania inayolenga kuendeleza sekta mkakati za nishati, maji, usafi
na usafirishaji.
Waziri Ayrault katika ziara yake hiyo alikutana na Rais mstaafu wa
Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, ambaye ni msuluhishi wa mgogoro wa
Burundi.
Katika mazungumzo yake alimpongeza msuluhishi huyo kwa juhudi zake za
kutaka pande zinazokinzana nchini humo kufikia muafaka kwa mujibu wa
makubaliano ya Arusha.
Aidha alisema taifa lake lipo bega kwa bega naye katika kuhakikisha
kwamba mgogoro wa Burundi unamalizika. Waziri Ayrault pia alikutana na
wawakilishi wa kampuni za Ufaransa zinazofanya shughuli mbalimbali
nchini Tanzania na kuwasisitizia kwamba uwekezaji wanaoufanya una maana
kubwa kwa Tanzania hasa katika kuwezesha upatikanaji wa nafasi za kazi.
Aidha alisema kwa uwekezaji huo na kuambukiza utaalamu na teknolojia
katika sekta mkakati za maendeleo kama uhandisi, maji, fedha na
mawasiliano, kutakuza zaidi ushirikiano wa Tanzania na Ufaransa katika
masuala ya kiuchumi.
Waziri Ayrault alimaliza ziara yake kwa kuzuru Bandari ya Dar es
Salaam ambayo ni lango kubwa la uchumi kwa Tanzania na nchi jirani.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment