WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa anatarajiwa kuhutubia mkutano mkubwa wa
kwanza wa hadhara katika uwanja wa Jamhuri akiwa mkazi wa Mkoa wa Dodoma
mara tu baada ya kupokewa rasmi mkoani hapa Alhamisi wiki hii.
Taarifa hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya Dodoma Mjini, Christina
Mndeme, wakati wa mkutano wake na viongozi wa dini uliofanyika mjini
hapa mwishoni mwa wiki.
Alieleza kuwa, baada ya Waziri Mkuu kupokelewa katika eneo la Mtimba,
msafara wake utaelekea uwanja wa Jamhuri ambapo atazungumza na wananchi
wa mkoa wa Dodoma.
Mkuu huyo wa wilaya aliwaomba viongozi wa dini, kushirikiana na serikali wilayani kumpokea waziri mkuu.
Alisema, waziri mkuu anahamia rasmi mjini hapa kwa ajili ya makazi na
kuendesha shughuli zake mbalimbali, ikiwemo za chama na Serikali.
Kauli hiyo imetolewa wakati Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na
Bunge, ikisema ukarabati wa nyumba ya Waziri Mkuu upo katika hatua ya
mwisho kukamilika.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, Jenista
Mhagama alisema hayo, baada ya kutembelea na kukagua maendeleo ya
ukarabati wa makazi hayo.
Aidha, Mhandisi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Joseph Mhamba, alisema
shughuli zote za ukarabati zinazofanywa na Wakala wa Majengo (TBA),
zinaendelea vizuri. Mhamba alisema kazi itakamilika kama ilivyopangwa.
Kwa upande wake, Mhandisi Kashimilu Mayunga kutoka Mamlaka ya
Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma Mjini (Duwasa), alisema kazi
inayoendelea ni kuchimba mitaro na kulaza mabomba. Alisema kazi hiyo
imekamilika kwa zaidi ya asilimia 70 na wanachosubiri sasa ni pampu.
Meneja wa mtandao wa Shirika la Simu (TTCL), Flavian Mziray alisema
kazi ya kupeleka mawasiliano makazi ya Waziri Mkuu, inakaribia
kukamilika.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment