MKUU wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla, amemwagiza Mkuu wa Wilaya ya
Mbeya, Paul Ntinika, kufuatilia eneo lililotengwa na Serikali kwa ajili
ya ujenzi wa Ikulu ndogo mjini Mbeya, ambalo inasemekana limeuzwa.
Eneo hilo ambalo ukubwa wake haujajulikana, lipo katika eneo la Veta
jijini Mbeya na inasemekana limeuzwa kwa wananchi ambao baadhi yao
wamejenga nyumba za makazi, huku wengine wakiendelea na ujenzi.
Makalla alitoa agizo hilo jana baada ya kutembelea na kulikagua eneo
hilo, huku akishuhudia jinsi baadhi ya watu walivyojenga nyumba zao
katika eneo hilo.
“Nimeambiwa eneo hili ni mali ya Serikali lililotengwa kwa ajili ya
ujenzi wa Ikulu, lakini wapo baadhi ya watu wameanza kulitumia kwa
kujenga nyumba za makazi.
“Kwa hiyo, nakuagiza wewe mkuu wa wilaya ulifuatilie eneo hili kujua
uhalali wake. Nataka ufahamu ukubwa wa eneo, ujiridhishe kama kweli
limeuzwa na baada ya hapo, walioliuza wachukuliwe hatua,” aliagiza
Makalla.
Wakati Makalla akisema hayo, mmoja wa watumishi wa Halmashauri ya
Mbeya ambaye hakutaka kutaja jina lake, aliliambia MTANZANIA kwamba eneo
hilo awali lilikuwa likimilikiwa kiasili na wananchi kabla ya Ikulu
haijalichukua.
“Hata hivyo, baada ya Serikali kulichukua eneo hilo kwa ajili ya
ujenzi wa Ikulu, ilitakiwa kuwalipa wananchi wote waliokuwa
wakilimiliki, lakini haikufanya hivyo na badala yake iliwafidia watu
wachache.
“Waliolipwa fidia ni wachache kwa hiyo, mtu anaposema eneo la Ikulu
limeuzwa mimi napata tabu kumwelewa kwa sababu kuna eneo halikulipwa
fidia ingawa Serikali ilikuwa ikilihitaji,” alisema mtoa taarifa huyo.
Naye Katibu Tawala Mkoa wa Mbeya (RAS), Mariamu Mtunguja, alipotakiwa
na MTANZANIA kutoa ufafanuzi wa eneo hilo, alisema aliomba apewe muda
ili afanye uchunguzi wa kina.
“Hapa naona kama kuna mgawanyiko wa taarifa, ninaomba nipewe muda ii
nilifuatilie suala hili kwa undani zaidi ili nitakapotoa taarifa iwe ni
taarifa sahihi,”alisema Mtunguja.
Home
News
Slider
Makalla amwagiza DC Ntinika kufuatilia eneo la Ujenzi wa Ikulu ndogo linalodaiwa kuuzwa Mbeya.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)


0 comments:
Post a Comment