KWA kasi iliyopo kwenye muziki wa Singeli, ni wazi kwamba unaelekea
kuupoteza muziki wa Bongo Fleva kutokana na kasi ya kuenea kwake hapa
nchini, jambo linalosisitizwa na mkali anayetesa katika muziki huo,
Amani Khamisi ‘Man Fongo’.
Man Fongo ambaye amepachikwa jina la Mfalme wa Singeli, anayesumbua
na kibao chake cha Hainaga Ushemeji amesema wasanii wa Bongo Fleva wana
kazi kubwa kuhakikisha wanabaki kileleni kutokana na namna muziki wao
ulivyopokelewa vizuri na mashabiki.
“Muziki tunaouimba ni wa mtaani ambapo ndiko chimbuko na watu wa
uswahilini, kwa sasa huwaambii kitu kuhusu muziki wetu. Nawaambia ukweli
kabisa wasanii wa Bongo Fleva, wakaze buti twende sawa au watafute kitu
kingine cha kufanya.
“Ujue wao wanaimba vitu vya kubuni wakati sisi tunaimba maisha
halisi hasa ya uswahilini kwa masikini wenzetu,” anasema Man Fongo.
Awali watu waliuita muziki wa kihuni kutokana na vijana kufanya
matukio mbalimbali ulipokuwa unapigwa kwenye shughuli za mitaani nyakati
za usiku maarufu vigodoro.
Kadiri siku zinavyokwenda, muziki huo umeanza kueleweka kiasi cha
baadhi ya wasanii wa Bongo Fleva kushirikiana na wasanii wa Singeli
kwenye nyimbo zao.
Mfano mzuri ni mwana-Hip Hop mwenye nguvu Bongo, Joseph Haule maarufu
Profesa Jay ambaye ni Mbunge wa Mikumi kupitia Chadema alipofanya
kolabo ya nguvu na msanii wa Singeli Sholomwamba.
Katika mazungumzo na jarida hili, Man Fongo ambaye anasimamiwa na
Makes Entertainment amezungumza mengi kuhusiana na safari yake ya maisha
na muziki kwa jumla.
SAFARI YAKE KIMUZIKI
Anasema alianza muziki tangu akiwa darasa la tano mwaka 2006 wakati
akifanya shughuli zake za udj ambapo ilikuwa kama kurusha roho tu.
“Kipindi hicho Msaga Sumu ndiye alikuwa anajulikana zaidi na nilikuwa
napitisha maneno kwenye baadhi ya nyimbo zake, mashabiki wakatokea
kunikubali wakataka nijaribu kuimba.
“Licha ya kuanza muziki niliendelea na masomo yangu hadi nilipomaliza
darasa la saba mwaka 2008, sikufanikiwa kuendelea na sekondari kutokana
na kipato cha familia yangu.
“Muziki ukawa maisha yangu, namshukuru Mungu mwaka jana nilianza
kupata mashabiki wengi na mwaka huu naweza kusema wameuelewa zaidi
muziki wangu,” anasema Man Fongo.
FIESTA 2016
“Kwangu shoo kubwa ambazo nilikuwa nazifanya ni za kuitwa kwenye
shughuli za watu kama ndoa, sherehe za kuzaliwa nk, lakini mwaka huu
nashukuru Mungu nimeitwa Fiesta.
“Najua nitakutana na mashabiki wangu wengi katika mikoa nitakayopita.
Zamani Singeli ilionekana kama muziki wa kihuni lakini nashukuru sasa
watu wameuelewa muziki wetu.”
MALENGO YAKE
Anasema matarajio yake ni kufika mbali kimataifa lakini hawezi kufika kama Watanzania hawatauunga mkono muziki wa Singeli.
“Kila siku nawaza kuwaburudisha mashabiki wangu na kuupaisha muziki
huu kimataifa zaidi, ni ndoto yangu kuwainua wadogo zangu ambao
hawajasikika.
“Pia nimeamua kuacha tabia ya kutoa nyimbo tatu na sasa nitaanza
kutoa albamu nzima, natarajia kutoa albamu yangu ya kwanza hivi
karibuni,” anasema.
SINGELI KUONEKANA UHUNI
Anasema muziki huo umekuwa ukiitwa wa kihuni kutokana na mazingira
ambayo umekuwa ukichezwa kuwa ya uswahilini sana ambapo vijana wa huko
ndiyo wahuni.
“Naona ni kawaida kwa sababu Singeli ni muziki wa vijana na vijana ni
damu changa, kwahiyo wao muda wote wanataka kucheza labda katika
kufanya vile watu wengine wakauona ni wa kihuni.
“Muziki huu jamani siyo wa kihuni, labda watu wanaoupenda ndiyo
wanaonekana wahuni… uswahilini hawaishi mabrazamen, huku wanaishi watu
wa kawaida, ndiyo maana labda unachukuliwa kiivyo, lakini ni muziki
mzuri, mtamu na unachezeka,” anasema.
CHANGAMOTO
Unapokuwa staa lazima kuwe na changamoto mbalimbali unazokutana nazo,
kwa upande wake anasema amekuwa akipata usumbufu mkubwa kutoka kwa
wasichana katika mitandao mbalimbali ya kijamii wanaomtaka kimapenzi.
“Siishiwi kupigiwa simu na baadhi ya wadada wakinisumbua, Instagram
huko ndiyo shida zaidi… lakini najua ni mashabiki wangu, siwezi
kuwachukia ila ukweli ni kwamba mimi nina mchumba wangu ambaye nipo naye
miaka mitatu sasa na muda siyo mrefu tutafunga ndoa.
“Kupendwa kupo, lakini wajue tayari miye ni mali ya mtu. Napenda
sapoti yao, waendelee kupenda muziki wa Man Fongo lakini siyo mambo ya
mapenzi,” anasema Man Fongo.
Man Fongo pia alieleza kinachomchukiza zaidi katika muziki ambapo
alisema: “Sipendi kupigana kwa sababu tukipigana ndiyo tunaonekana
wahuni wakati lengo letu ni kuufanya kuwa wa kimataifa. Tukifanya vurugu
hatuwezi kufikia popote.”
Home
BURUDANI
Slider
Man Fongo: Kwa ukubwa wa Music wa Singeli hivi sasa, Bongo Flava itabaki Story.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)


0 comments:
Post a Comment