MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, jana ilitupilia
mbali pingamizi lililotolewa na upande wa Jamhuri la kumzuia Wakili
Peter Kibatala kumtetea Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu,
anayekabiliwa na kesi yenye mashtaka matatu.
Lissu ameshtakiwa mahakamani kwa makosa mawili ya uchochezi na moja la kutoheshimu mahakama.
Uamuzi wa kutupilia mbali pingamizi hilo ulitolewa na Hakimu Mkazi
Mkuu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Cyprian Mkeha ambaye aisema kuwa kwa
mazingira yalivyo katika kesi hiyo, mahakama haioni kikwazo cha wakili
Kibatala kushindwa kumtetea mteja wake.
Alisema mahakama haoni sheria inayomzuia Kibatala kutoa ushahidi kwa Jamhuri huku akiwa wakili upande wa utetezi.
“Kutokana na mazingira ya kesi hii, mahakama haioni kikwazo cha
wakili wa mtuhumiwa kushindwa kuendelea na kazi yake, nimepitia kanuni
za uwakili na sheria za ushahidi, hakuna kifungu chochote kinachomzuia
wakili kumtetea mteja wake kwa kuwa ni shahidi na alikuwepo wakati wa
kuchukua maelezo,” alisema Hakimu Mkeha.
Aidha, hakimu huyo alirejea misimamo ya sheria za nchi mbalimbali
zinazoendana za zilizopo nchini zikiwemo sheria zinazotumiwa na mataifa
ya Uingereza na India na kusisitiza kuwa Jamhuri pia inaweza kumtumia
Kibatala kama shahidi endapo itakuwa imekubaliana naye.
Baada ya kutupiliwa kwa pingamizi hilo, Wakili Mkuu wa upande wa
Serikali, Faraja Nchimbi, alisema hajaridhishwa na uamuzi huo na kueleza
kuwa anasubiri kupata mwenendo mzima wa shauri hilo ili aweze kukata
rufaa.
Hoja ya upande wa Jamhuri iliibuliwa Agosti 5, mwaka huu ambapo Lissu
alifikishwa mahakamani kwa mara ya tatu kwa makosa ya uchochezi.
Wakili Mkuu wa Serikali, Nchimbi na wenzake watatu akiwemo Wakili
Mwandamizi Mutalemwa Kishenyi, Simon Wankyo na Paul Kudushi, walipinga
Kibatala kusimama kama wakili katika kesi hiyo baada ya kupitia jalada
la kesi na kugundua kuwa Kibatala anafaa kuwa shahidi upande wa Jamhuri
na uwepo kama wakili wa upande wa utetezi unaweza kuathiri mwenendo wa
kesi.
Wakili Nchimbi alidai kuwa baada ya kupitia maelezo ya wakili huyo,
walijiridhisha hakuna namna ambayo wanaweza kukwepa kumuita Kibatala
kama shahidi katika kesi hiyo, hivyo kimsimamo na kisheria hata kama
yeye hataki atalazimika kutoa ushahidi.
Aliiomba mahakama imwondoe Kibatala kumwakilisha Lissu kwa kuwa
wakati kesi inasikilizwa shahidi hatakiwi kuwepo mahakamani hasa wakati
mashahidi wengine wakitoa ushahidi.
Akijibu, Kibatala alidai hoja zote dhidi yake hazina mashiko wala
sifa za kuitwa pingamizi la kisheria kwa kuwa mawakili hao walitumia
maelezo waliyodai kuandikwa na Kibatala polisi hivyo wanapaswa
kuithibitishia mahakama kama ni yeye aliyeyaandika.
Aliendelea kujibu kuwa mahakama haiwezi kumwondoa kwa sababu hakuna
sheria inayosema iwapo wakili akihojiwa hawezi kumtetea mteja wake.
Kibatala aliiomba mahakama ilinde haki ya mshtakiwa kuwakilishwa
mahakamani na kwa kuwa suala hilo linahusu haki ya kikatiba kama inaona
ni zito ilipeleke Mahakama Kuu.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)


0 comments:
Post a Comment