MFANYABIASHARA Juma Mwinyi maarufu (Neti) aliyekuwa akidaiwa kumweka
reheni mdogo wake nchini Pakistani kwa Sh bilioni 1.5 afikishwa
mahakamani kwa tuhuma za kusafirisha binadamu.
Juma alipanda kizimbani jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
na kusomewa mashtaka yanayomkabili mbele ya Hakimu Mfawidhi, Cyprian
Mkeha.
Akisoma mashtaka Wakili wa Serikali Mkuu, Peter Njike alidai kati ya
Desemba Mosi mwaka 2015 na Julai 15 mwaka huu jijini Dar es Salaam
mshtakiwa alitenda kosa la kusafirisha binadamu kinyume cha sheria.
Njike alidai Juma alijifanya anakwenda kumpa mafunzo Adam Akida
Mkazi wa Magomeni, Mtaa wa Chemchem na Idirsa na badala yake
alimsafirisha kwenda nchini Pakistan kwa ajili ya kumweka reheni.
Mshtakiwa alipotakiwa kujibu kama kweli ama si kweli, alikana
kuhusika na tuhuma hizo na upande wa mashtaka ulidai upelelezi wa kesi
hiyo haujakamilika wakaomba kuahirisha kesi.
Hakimu Mkeha alimfahamisha mshtakiwa kwamba shauri lake halina
dhamana kisheria, anaamini upande wa mashtaka hautachukua muda mrefu
kukamilisha upelelezi.
Baada ya kusema hayo, alikubali kuahirisha kesi hiyo hadi Agosti 17
mwaka huu kwa ajili ya kutajwa na mshtakiwa alirudishwa rumande.
Hatua ya kukamatwa kwa Juma, ni matokeo ya gazeti hili kuripoti
habari za Mtanzania kushikiliwa ughaibuni kutokana na biashara ya dawa
za kulevya Julai 18, mwaka huu.
Habari hizo ziliripotiwa baada ya video kusambaa katika mitandao ya
kijamii Julai 17, mwaka huu ikimwonesha Adamu Akida alivyowekwa chini ya
ulinzi na maharamia hao wenye silaha.
MTANZANIA lilifuatilia tukio hilo na kubaini kuwa, Adamu alikuwa
amewekwa rehani kwa gharama ya Sh bilioni 1.5 kwa kile kilichoelezwa
kuwa ilikuwa ni utekelezaji wa mpango wa biashara ya ‘unga’.
Kutokana na hatua hiyo, timu ya MTANZANIA iliamua kuchimbua suala
hilo ili kujua ukweli wa namna kijana Adamu Akida, alivyokuwa kwenye
mateso hayo.
Akisimulia tukio hilo kaka yake aliyejitambulisha kwa jina la Hemed
Abdallah (si jina lake halisi) alisema miezi minane iliyopita, Adamu
alikwenda kwa kaka yake ambaye ni mtoto wa mama yake mdogo
aliyetambulika kwa jina la Juma na kuomba msaada wa mtaji kwani kazi
yake ya kinyozi haikuwa ikilipa na hali ya maisha ilikuwa ngumu.
Alisema baada ya kueleza shida yake, Juma alimuhoji kama yupo tayari
kwa ajili ya kutafuta maisha nje ya nchi na Adamu alikubali kufanya kazi
ya aina yoyote ili mradi aweze kupata fedha.
“Awali alikwenda kwa kaka yake mtoto wa mama yake mdogo anaitwa Juma
na kuomba asaidiwe mtaji kwani amekuwa na maisha magumu sana. Baada ya
hali hiyo aliambiwa kuna safari ya kwenda Pakistan ambayo waliondoka
wakiwa wameandamana watu watatu pamoja na Juma na kijana mwengine ambaye
jina lake limenitoka, ila anaishi Kinondoni.
“Walipofika kule, Juma akachukua mzigo akiwa na yule kijana wa
Kinondoni, huku Adamu akiachwa Pakistan kwa maelezo kuwa baada ya siku
tano atakuja nchini na mzigo mwingine. Muda wote hata tukihoji alipo
Adamu tunaambiwa yupo anaendelea na kazi huko aliko na angerudi mwezi wa
tisa au wa nane.
“Sasa hii video ndiyo imetupa picha halisi ya Adamu, maskini sijui
kama tutampata akiwa hai. Hata hivyo kwa kipindi cha hivi karibuni,
tulikuwa tukishangazwa na mwenendo wa Juma kwani amekuwa na fedha nyingi
sana hadi kufikia kuwajengea nyumba dada zake pamoja na kuwanunulia
magari,” alisema Abdallah huku akibubujikwa na machozi.
Kutokana na hali hiyo vyombo vya dola vilianza kuendesha msako wa
ndani na nje ya nchi kumsaka Juma Neti, ambapo kutokana na hali hiyo
ilielezwa kuwa walifika mara kadhaa nyumbani kwake Kunduchi Unonio kwa
ajili ya kumsaka bila mafanikio, kwani alitoroka.
Mke alivyohama
Julai 19, mwaka huu chanzo cha uhakika kililiambia MTANZANIA kuwa mke wa Adamu ambaye alikuwa akiishi Mtaa wa Sunna, Magomeni, alihamia Kijitonyama.
Mke huyo wa Adamu, alihamishwa na shemeji yake, Juma ambaye ndiye aliyempangia nyumba nyingine Kijitonyama.
“Katika suala hilo, tuna shaka kuwa hata mke wa Adamu anajua
kinachoendelea, maana miezi mitatu iliyopita alihama Magomeni na kuhamia
Kijitonyama, tena huku akisema mume wake karibu anarejea nchini.
“Lakini baada ya video kuanza kuonekana, sasa hata kupatikana
hapatikani na hatujui amehamia nyumba gani huko Kijitonyama,” alisema
Abdallah.
Kauli ya Mwenyekiti wa Mtaa
Akizungumza na Mtanzania, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Idrissa,
Issa Mpangile, alisema askari kutoka makao makuu ya Jeshi la Polisi
walifika katika ofisi yake na kumtaka waongozane kwenda katika nyumba ya
baba mdogo wa Adamu.
Alisema walipofika nyumbani kwa Kessy Baharia Mtaa wa Idisa, ambaye
ndiye baba mdogo wa Adamu, polisi walichukua maelezo yake na baadaye
wakarudi katika ofisi ya Serikali ya Mtaa kuchukua maelezo yake.
Akizungumzia kuhusu kijana huyo, Mpangile alisema kuwa ni mzaliwa wa
mtaa huo, lakini baadaye alihamia Mtaa wa Suna ambao ni jirani na Mtaa
wa Idrissa, Kata ya Magomeni.
Alisema wakati kijana huyo anahama mtaa huo, alikuwa bado ni kinyozi na hakuwa na rekodi ya kusafiri kwenda nje ya nchi.
Alisema katika mazungumzo na Baharia, alimweleza kuwa amewasiliana na baba wa kijana huyo ambaye anaishi Bagamoyo mkoani Pwani.
Mpangile alisema kwa mujibu wa Baharia, baba wa kijana huyo
anayejulikana kwa jina la Akida, amesikia habari za mtoto wake na kwamba
atakwenda kuripoti kituo cha polisi.
Naye mama mdogo wa Adamu, aliyetambulika kwa jina la Khadija Katundu, alikiri maofisa wa polisi kumuhoji mume wake.
Alisema wameendelea kutoa ushirikiano kwa watu wanaofika nyumbani
kwao kuhoji kuhusu suala hilo, na kwamba wanaamini ufumbuzi utapatikana.
Inasemekana kijana huyo aliwekwa rehani kwa ghamara ya Dola za Marekani 700, 000, sawa na zaidi ya Sh bilioni 1.5 za Tanzania.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa ndugu wa karibu wa Mtanzania huyo
zinasema kuwa, Adamu aliwekwa rehani na kaka yake aitwaye Juma akitakiwa
kulipa fedha za unga (mihadarati) aliyochukua.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment