Na Fatma Salum na Sheila Simba, MAELEZO
Spika
wa zamani wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Pius Msekwa
amewaasa watanzania kuacha kufuata mkumbo wa kisiasa badala yake watii
mamlaka ili kuepuka kuvunja sheria na kuleta madhara kwao binafsi na
taifa kwa ujumla.
Msekwa aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam
wakati akizungumzia masuala mbalimbali kuhusu mwenendo wa siasa za hapa
nchini na utendaji kazi wa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa
Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli. Alieleza kuwa watu wengi wana hulka ya
kufuata mkumbo kwenye mambo fulani bila ya kuchunguza na kufahamu ukweli
wake kabla ya kushabikia.
“Ni hulka ya watanzania kushabikia mambo
wasiyoyafahamu ilimradi tu yanawafurahisha masikioni au machoni mwao
kwani hata huko mitaani wanakimbilia ngoma bila ya kujua inatokea wapi
au inaelekea wapi, hivyo nawasihi wajaribu kuwa makini na mbinu za siasa
zinazotumiwa na baadhi ya vyama kwa kuwa nyingine zina madhara ndani
yake.” Alisema Msekwa.
Akifafanua mwenendo wa siasa za hapa nchini,
Mzee Msekwa alisema kuwa bado wanasiasa wengi hawafuati kanuni za
ushindani wa kisiasa katika kutafuta madaraka badala yake wanatumia
mbinu ambazo zinavunja sheria za nchi na hatimaye wanapambana na
mamlaka.
“Ushindani wa kisiasa ni jambo la kawaida na linalokubalika
ingawa ushindani huo ni lazima ufuate sheria, kanuni na taratibu
zilizowekwa ili kufikia lengo, hivyo kubuni vitu ambavyo vinachochea
utovu wa nidhamu na uvunjifu wa amani sio jambo zuri, ' alisisitiza.
Aidha,
Msekwa alieleza kuwa utendaji wa Mhe. John Magufuli ni wa kuridhisha na
wa aina yake kwa kuwa amekusudia kuleta mabadiliko chanya kwa
watanzania na kuondoa mfumo wa utendaji kazi kwa mazoea jambo ambalo
limesaidia kurudisha nidhamu kwa watumishi wa Serikali.
Akizungumzia
uzoefu wake katika masuala ya kuongoza Bunge, alieleza kuwa tofauti ya
Bunge la zamani ni kwamba lilikuwa na nidhamu kubwa na linaheshimika
lakini Bunge la sasa halina utii na hicho ndio chanzo cha malumbano
yanayojitokeza mara kwa mara katika vikao vya Bunge.
Aliongeza kuwa
tangu awali wapinzani kazi yao ni kuipinga Serikali iliyo madarakani
lakini kwenye Bunge la uongozi wake walikuwa wakipinga kwa kutumia hoja
na kufuata kanuni bila ya kudharau mamlaka ya Spika wala Serikali
iliyoko madarakani.
“Kanuni zinatoa nafasi kwa mbunge asiyeridhika na
maamuzi ya Spika kushitaki kwenye Kamati ya Kanuni za Bunge, na kamati
hiyo itasikiliza na kutoa uamuzi kama mahakama inavyosikiliza lakini
wabunge wa sasa hawataki kutumia utaratibu bali hutumia mbinu za tofauti
ili waweze kupata sifa ambazo hazina tija kwa wananchi waliowachagua,”
alisema.
Msekwa pia amewaasa vyama vya upinzani kutumia mbinu nzuri
katika kutafuta madaraka bila ya kuvunja sheria au kuhatarisha amani ya
nchi kwani waliowachagua wanategemea zaidi matokeo ya kazi waliyoahidi
kuwatumikia kuliko malumbano yasiyo na tija kwa ustawi wao na taifa.
mwisho
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment