Image
Image

Nida iwe makini utoaji namba za vitambulisho.

KATIKA mkakati wa kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata Vitambulisho vya Taifa, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), imesema ifikapo Desemba 31, mwaka huu, Watanzania milioni 23 watakuwa na namba za utambulisho wa Vitambulisho vya Uraia.

Hayo yalisemwa na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Nida, Rose Mdami, na kufafanua kuwa hatua hiyo ni utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli la kuitaka Nida kuweka saini ya mwombaji na mtoaji wa vitambulisho hivyo.
Kwa mujibu wa ofisa huyo, mamlaka imeanza kutekeleza agizo la Rais Magufuli tangu Juni, mwaka huu na kwamba vitambulisho vyote ilivyochapisha kuanzia Juni hadi sasa, vina saini ya muombaji, saini ya mtoaji na tarehe ya kuzaliwa.
Mdami alisema kuwa ifikapo Desemba 31, mwaka huu, Nida itakuwa imetoa namba za utambulisho wa vitambulisho hivyo kwa Watanzania milioni 23 kwa kutumia taarifa za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) zilizo katika vitambulisho vya kupigia kura na kuzihamishia katika kanzi data ya Nida.
Nida inaeleza kuwa ili mwananchi apate kitambulisho cha uraia, atatakiwa kufika katika ofisi zake akiwa na vielelezo vinavyoonyesha mwaka wake wa kuzaliwa pamoja uthibitisho wa uraia wake kwa kuwa Nec haina viambatanisho hivyo.
Kuanza upya kwa mchakato huo ambao ulisitishwa, baada ya kubainika madudu kadhaa na kusababisha watendaji wakuu wa Nida kusimamishwa kazi kunaibua matumaini mapya kwamba ahadi ya Serikali ya kuwapatia Watanzania vitambulisho vya uraia itatekelezwa.
Sio lengo letu kuzungumzia sababu zilizokwamisha upatikanaji wa vitambulisho hivyo kwa muda uliokuwa umepangwa na Serikali ya Awamu ya Nne kwa kuwa suala hilo kwa sasa liko katika vyombo vya uchunguzi.
Hata hivyo, tunatoa angalizo kwa Nida kuhakikisha kwamba inatekeleza kazi hiyo kwa umakini mkubwa kuepuka uwezekano wa kutokea madudu kama yaliyotokea awali na kuisababishia Serikali hasara ya mabilioni ya fedha, ambazo zingetumika kugharimia miradi mingine ya maendeleo.
Umakini huo pia uende sambamba na uchapakazi, uwazi, weledi na uadilifu ili Watanzania milioni 23 wawe wamepatiwa namba za utambulisho wa Vitambulisho vya Uraia ufikapo Desemba 31, mwaka huu.
Ili kufanikiwa lengo hilo kwa tija na ufanisi, tunaishauri Nida kuweka utaratibu mzuri wa mawasiliano na wananchi ili wapate taarifa kwa wakati na zinazoeleweka tofauti na mchakato wa kwanza ambao ulilalamikiwa na wengi kutokana na kutopata taarifa za kina na kwa wakati.
Vilevile, tunaishauri Nida kuweka utaratibu wa kutoa elimu kwa wananchi ikiwezekana kupitia kwa watendaji wa kata, mitaa, vijiji na vitongoji ambao wako karibu nao kuhusiana na masuala kadhaa, likiwamo la kupata namba za vitambulisho.
Wananchi nao watatakiwa kutoa ushirikiano kwa Nida kwa kwenda aidha katika ofisi za mamlaka au za watendaji wa vijiji, kata, vijiji, mitaa na vitongoji ili kupata ufafanuzi kuhusiana na mambo yatakayowakwaza.
Taarifa kwamba mpaka sasa Watanzania milioni 2.7 wameshapatiwa vitambulisho hivyo na milioni 6.5 wamesajiliwa kwa ajili ya kupata vitambulisho hivyo zinatia moyo na bila shaka kazi hiyo itakwenda kwa kasi huku idadi kubwa ikiendelea kusajiliwa na mwishowe kila Mtanzania mwenye sifa ya kupata kitambulisho hicho anakipata.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment