WAKATI serikali ikianza taratibu za kuhamia Dodoma, Kamati ya Hesabu
za Serikali (PAC) imemuomba Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG) kwa kushirikiana na msimamizi wa mali za serikali kufanya
uchunguzi kuona namna Sh bilioni 12.5 zilivyotumika kwenye ujenzi wa
ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo ambayo bado inaendelea kujengwa.
Akitoa maazimio ya kamati hiyo mara baada ya kumaliza kuihoji
Sekretarieti ya Mkoa wa Dodoma, Mwenyekiti wa kikao hicho, Japhet
Hasunga ambaye ni Mbunge wa Vwawa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM),
alisema kamati inataka kujiridhisha thamani ya fedha zilizotumika katika
ujenzi huo.
Katika tukio lingine, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya
Gairo mkoani Morogoro, Agnes Mkandya ameangua kilio wakati akihojiwa na
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), kutokana na
kuulizwa maswali mfululizo ya ubadhirifu wa fedha kwenye halmashauri
hiyo.
Mkandya alijikuta katika wakati mgumu wakati akijibu maswali
mbalimbali, yanayohusiana na ubadhirifu hali iliyofanya kuanza kulia,
huku akichukua kitambaa na kujifuta machozi, hatua iliyofanya Mwenyekiti
wa Kamati hiyo, Mbunge wa Kilwa Mjini, Vedastus Ngombale (CUF) kumtaka
kuwa mtulivu wakati akijibu maswali.
CAG na ofisi ya RC
Hasunga akieleza maazimio ya Kamati ya PAC, alisema lengo ni
kujiridhisha usahihi wa fedha zilizotumika katika ujenzi wa ofisi hiyo
ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, ambayo iliungua moto miaka michache
iliyopita.
“Kamati inamuomba CAG kwa kushirikiana na Idara ya Usimamizi wa Mali
za Serikali kufanya tathmini ya kina ili kuiridhisha kamati iwapo
gharama ya Sh bilioni 12.5 zilizotumika katika ujenzi wa jengo la ofisi
ya Mkuu wa Mkoa hadi sasa zinakidhi thamani na hali halisi ya jengo hilo
lilipofikia,” alisema.
Pia kamati hiyo iliiagiza Idara ya Usimamizi Mali za Serikali,
kufanya uhakiki maalumu wa mali za serikali hususan magari yanayofanya
kazi, yaliyoharibika, yaliyouzwa na kuwasilisha taarifa ya uhakiki huo
maalumu kwa kamati ndani ya kipindi cha miezi mitatu ijayo.
Mwenyekiti huyo wa Kikao, pia alimtaka Ofisa Masuhuli kusimamia
kikamilifu Kitengo cha Uhasibu cha Sekretarieti ya Mkoa ili kuzingatia
viwango vya kimataifa vya utayarishaji wa mahesabu katika uandaaji wa
taarifa za hesabu za serikali ili kuepuka hati za ukaguzi zenye dosari.
Alisema Ofisa Masuhuli anaagizwa pia kuzingatia Sheria ya Manunuzi ya
Umma na kanuni zake katika shughuli za sekretarieti, ikiwa ni pamoja na
kupata vibali kwenye mamlaka husika unapofanyika uhamisho wa fedha
katika vifungu mbalimbali.
Alimuagiza Ofisa Masuhuli kuwasiliana na Ofisi ya Rais, Menejimenti
ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ili kuhakikisha nafasi za kazi
zinazokaimiwa zinajazwa mapema iwezekanavyo ili kuongeza ufanisi wa
Sekretarieti ya Mkoa wa Dodoma.
“Pia kuna hoja nyingi za ukaguzi bado hazijapata majibu ya kina,
kamati inatoa muda wa miezi sita kwa Sekretarieti ya Mkoa kukamilisha
majibu ya hoja za ukaguzi na taarifa za utekelezaji iwasilishwe kwa CAG
na kwa kamati ndani ya muda huo,” alisema.
Awali Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Rehema Madenge alisema
sekretarieti hiyo itafanyia kazi maagizo yote, ambayo kamati hiyo
imeelekeza.
Mbunge wa Dimani, Hadith Ally Tahiri (CCM) ambaye ni mjumbe wa kamati
hiyo, alihoji sababu zilizofanya chumba cha kuhifadhi maiti katika
Hospitali ya Mkoa wa Dodoma kuwa na majokofu mabovu kwa muda mrefu na
ubovu wa huduma zitolewazo katika Wodi ya Wagonjwa Walio katika
Uangalizi Maalumu (ICU).
‘’Makao Makuu ya Nchi yanakuwa hapa Dodoma, Je, hospitali hii itaweza kuhudumia wagonjwa wote?” Alihoji.
Akijibu hoja hizo, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, Dk
Zainabu Chaula aliiomba kamati hiyo kusaidia hospitali hiyo iweze
kupata huduma za kiwango cha kuridhisha.
DED aangua kilio akihojiwa
Katika tukio lingine lisilo la kawaida, Mkurugenzi Mtendaji wa
Halmashauri ya Wilaya ya Gairo mkoani Morogoro, Agnes Mkandya jana
alijikuta akiangua kilio wakati akihojiwa mbele ya Kamati ya Bunge ya
LAAC, kutokana na kuulizwa maswali mfululizo ya ubadhirifu wa fedha
kwenye halmashauri hiyo.
Mkandya alijikuta katika wakati mgumu wakati akijibu maswali
yaliyohusu ubadhirifu, hatua iliyofanya kuanza kulia na kumlazimu
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Ngombale, kumtaka kuwa mtulivu wakati akijibu
maswali.
Tukio hilo lilitokea wakati Mkurugenzi huyo, alipoulizwa swali na
Mbunge wa Viti Maalum, Leah Komanya (CCM) ambaye ni mjumbe wa Kamati
hiyo, aliyetaka majibu kuhusu ubadhirifu wa fedha katika Halmashauri ya
Gairo.
Akijibu, Mkurugenzi huyo alisema amewasimamisha kazi wakuu tisa wa
idara na halmashauri hiyo kutokana na ubadhirifu uliokithiri. Hata
hivyo, wakati wabunge wakiendelea kusikiliza maelezo zaidi, Mkurugenzi
huyo alishindwa kuendelea kujibu na badala yake kuangua kilio.
Kutokana na kitendo hicho, Mwenyekiti wa Kamati alimtaka Mkaguzi wa
Ndani wa Halmashauri kujibu swali hilo, lakini naye aliposimama alisema
wana muda mfupi tangu wakabidhiwe madaraka, hivyo inakuwa vigumu kuweza
kujibu maswali yote.
Kutokana na majibu hayo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo alimuinua Katibu
Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Dk John Ndunguru kujibu swali hilo, ambapo
aliposimama alisema viongozi wengi ni wageni na watajitahidi kufuata
maagizo watakayopewa.
Katika maelezo ya swali, Mbunge Komanya alisema Halmashauri ya Gairo
imekuwa na ubadhirifu mkubwa wa fedha kwa kutumia karatasi za nukushi
(carbon slip), hivyo kuikosesha serikali mapato na kumuagiza mkurugenzi
huyo kutoa majibu.
Akijibu hoja hiyo, mkurugenzi huyo alisema suala la wizi wa aina hiyo
lilijitokeza ambapo walikamata mtendaji mmoja na sasa wanaendelea na
kazi ya kufunga Mashine za Kielektroniki za Kukusanya Mapato (EFD’s)
huku Kampuni ya Simu (TTCL) ikifanya taratibu za kuwaunganisha.
“Mimi nilikuwa natoa angalizo, nataka Mkurugenzi ajibu kama
nilivyouliza, sitaki maelezo mengi,” alisema Komanya na kumfanya
mkurugenzi huyo kuangua kilio na kuchukua kitambaa cha kujifuta machozi.
Home
News
Slider
PAC yamuomba CAG kuchunguza namna Bilioni 12.5 zilivyotumika ujenzi wa ofisi ya RC.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)


0 comments:
Post a Comment