Askari wakiwa katika harakati za kulinda usal;ama(Picha na Maktaba).
NI mwendo wa doria. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya askari polisi
kulazimika kupiga kambi katika Ofisi za Makao Makuu ya Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), zilizopo Mtaa wa Ufipa, Dar es
Salaam.
Polisi hao tangu jana asubuhi walikuwa wakifanya doria katika eneo
hilo huku wengine wakizingira ofisi za chama hicho wakiwa wamevaa
kiraia.
Kutokana na hali hiyo, MTANZANIA ilituma timu ya waandishi ambao
kutwa nzima ya jana waliwashuhudia askari polisi wakiwa nje ya ofisi za
chama hicho na wengine wakiwa ndani ya magari ya doria.
Hatua hiyo ilionekana kuzua taharuki kwa baadhi ya wanachama na
viongozi wa juu wa chama hicho ambao walijikuta wakishindwa kufanya
kikao cha dharura cha Kamati Kuu kwa hofu ya kuzuka vurugu.
Ilipotimu saa tano asubuhi, timu ya walinzi wa Chadema ‘Red Brigade’
waliongezeka na kusimama nje ya ofisi za makao makuu huku wakionekana
kuwa tayari kwa lolote, ikiwamo kujihami kwa kuwalinda viongozi wao;
mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye ambao
waliwasili katika ofisi hizo kwa ajili ya kikao.
Kikao hicho kilikuwa ni cha mwandelezo baada ya kile cha juzi
kushindwa kumalizika na baadhi ya viongozi wa chama hicho kukamatwa na
polisi.
Pamoja na hali hiyo, ilipotimu saa 9 alasiri, viongozi hao
wakiongozwa na Lowassa walitoka nje na kuelezwa kuwa kikao kimeshindwa
kufanyika kwa kuwa hali ya usalama si nzuri, hasa baada ya kuonekana
askari kanzu wakiingia ndani ya ofisi hiyo na wengine kujifanya ni
wanachama wa chama hicho.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe pamoja na Katibu Mkuu, Dk.
Vicent Mashinji, walilazimika kuondoka mapema na kwenda katika kikao cha
pamoja kati yao na viongozi wa dini ili kutafuta mwafaka, kuhusu
Operesheni Ukuta inayotarajiwa kufanyika kesho licha ya kuzuiwa na Jeshi
la Polisi.
Kikao hicho cha viongozi wa dini kilichofanyika katika Hoteli ya
Courtyard jijini Dar es Salaam, pamoja na mambo mengine kilijadili kwa
kina mkwamo wa kutafuta suluhu kati ya viongozi wa Chadema na Serikali
kuhusu kuzuiwa maandamano ya kesho.
MTANZANIA ilipomtafuta Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Mashinji ili
kupata ufafanuzi kuhusu kuzingirwa kwa ofisi zao na maofisa wa polisi,
alikiri kutokea kwa hali hiyo.
“Ni kweli tumeahirisha mkutano wetu wa Kamati Kuu mpaka hapo baadaye,
Ofisi zetu za Makao makuu zilizingirwa na askari wa kila aina, wengine
walivaa baraghashia, kanzu na kila aina ya nguo kwa lengo la kuvunja na
kutawanya mkutano wetu wa ndani, tumeuahirisha mpaka wakati mwingine,
tutawajulisha.
“Askari hao wamekuwa wakipiga kambi katika ofisi zetu kwa muda wa
wiki sasa, lakini kadiri siku zinavyokwenda idadi yao inazidi kuongezeka
kama ilivyokuwa leo (jana),” alisema Dk. Mashinji.
Taarifa kutoka ndani ya kikao hicho zilieleza kuwa wajumbe wa Kamati
Kuu walikutana ili kujadili mambo mbalimbali ikiwamo suala la maandamano
yanayotarajiwa kufanyika nchi nzima kuanzia kesho.
VIONGOZI WA DINI
Viongozi wa dini nchini wameendelea kukuna vichwa kutafuta suluhu
kati ya Serikali na vyama vya siasa vinavyojiandaa na Operesheni Ukuta
iliyopangwa kufanyika kote nchini kesho.
Viongozi hao walijichimbia jana Hoteli ya Courtyard katika kikao cha
siri ambacho kilihudhuriwa na Mwenyekiti wa Chadema, Mbowe, Katibu Mkuu
wake, Mashinji na mawaziri wakuu wa zamani; Sumaye na Lowassa.
Taarifa za ndani zinasema kuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM), Abdulrahman Kinana aliwasili hotelini hapo saa nne asubuhi,
lakini aliondoka punde baada ya kupokea simu ambayo inadaiwa alipigiwa
na Rais Dk. John Magufuli.
Kikao hicho kilichoanza saa mbili asubuhi hadi saa tisa alasiri ni
cha tatu kufanyika, ambacho mbali kuhudhuriwa na viongozi dini, pia
kilihudhuriwa na vyama vitano vyenye uwakilishi bungeni huku agenda kuu
ikiwa ni hali ya kisiasa nchini.
Akizungumza na MTANZANIA, Mwenyekiti Mwenza wa mkutano huo, Sheikh wa
Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum, alisema kuwa ulimalizika
salama na kukubaliana na kwamba watatoa taarifa rasmi ya kikao hicho leo
kwa umma.
“Kikao chetu tunamshukuru Mungu tumemaliza salama na kwa pamoja
tumeweza kukubaliana mambo mbalimbali, ikiwamo ya hali ya kisiasa
nchini, wabunge wa upinzani kususia vikao vya Bunge pamoja na Operesheni
Ukuta, ambayo tutayazungumza kwa waandishi wa habari kesho (leo) ili
Watanzania waweze kuyajua,” alisema Sheikh Alhad.
Pamoja na mambo mengine, alisema kwa sasa hali ni nzuri na wanaamini
mkutano huo utaweza kurudisha hali ya utulivu, umoja na mshikamano kwa
wananchi wote bila ya kujali tofauti zao za kisiasa, dini au kabila.
KAULI YA MASAJU
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa mkutano huo, Askofu Mkuu wa
Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Fredrick Shoo,
aliliambia MTANZANIA kuwa Serikali iwaache wafanye mambo kwa wakati
wanaoona unafaa.
Dk. Shoo alikuwa akizungumzia kauli iliyotolewa juzi na Mwanasheria
Mkuu wa Serikali, George Masaju, akiwataka viongozi wa dini kuliombea
taifa lisiingie kwenye uvunjifu wa amani kutokana na Operesheni Ukuta na
kwamba huu si wakati mwafaka wa kukaa meza ya majadiliano.
“Sisi tunafanya vitu kwa wakati tunaoona unafaa, siyo yeye atuamuru
cha kufanya, namuomba ayaache haya mambo hivi hivi kwani tunaujua wajibu
wetu kwa Serikali na wananchi ambao ni waumini wetu.
“Kwa sasa haya mambo tuyaache yabaki kama yalivyo, sisi tunazungumza
kuhusu masuala hayo hayo na tumefikia mahali pazuri, mtayasikia kesho
(leo), bado kikao hakijaisha,” alisema Dk. Shoo.
Habari hii imeandaliwa na Patricia Kimelemeta na Esther Mbussi, Dar es Salaam
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment