JUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF), limetoa tamko na kusema kuwa
limeshtushwa na kusononeshwa kutokana na hatua ya Serikali kupitia kwa
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye kuvifungia
kwa muda usiojulikana vituo viwili vya redio.
Vituo vilivyofungiwa ni Radio 5 ya Arusha na Magic FM ya Dar es Salaam, uamuzi ambao ulitangazwa juzi.
Tamko hilo la TEF lilitolewa jana Dar es Salaam na Katibu wa jukwaa hilo, Neville Meena.
Alisema kwa muda wa miezi takriban kumi tangu alipoteuliwa kuwa
waziri, Nape amejitokeza mara nne na kutangaza kufuta na kufungia vyombo
vya habari.
“Alianza kulifuta Gazeti la Mawio, baadaye alitangaza kufuta mamia ya
magazeti na majarida ambayo hayajachapishwa kwa muda mrefu, ikafuata
adhabu ya kulifungia kwa miaka mitatu Gazeti la Mseto na sasa vituo
viwili vya redio.
“Katika tukio la kufutwa kwa Mawio, tulihoji ukubwa wa kosa la gazeti
hilo kiasi cha kufutwa. Leo hii tunahoji tena ukubwa wa makosa na
pengine historia ya redio husika siku zilizopita. Ndiyo maana tunasema
hili la sasa ni mwendelezo wa ukandamizaji wa uhuru wa habari.
“TEF inachukulia hatua hii kama mwendelezo wa ukandamizaji wa uhuru
wa vyombo vya habari nchini na tunashindwa kuelewa dhamira ya Serikali
ya awamu ya tano kwa sekta ya habari nchini. Kinachoonekana ni kutumia
kila aina ya sheria iliyopo kukandamiza uhuru wa vyombo vya habari.
Kimsingi TEF hatuoni nia (spirit) ya malezi katika uamuzi wa waziri
huyo,” alisema Meena.
Kutokana na hali hiyo, alisema msimamo wa TEF, unasikitishwa na
utaratibu uliotumiwa na waziri kufikia uamuzi huo, umekuwa wa makosa
yaleyale ya siku zote.
“Pamoja na kwamba vyombo vya habari hufanya makosa, lakini hata pale
makosa yanapotokea taratibu za kuyashughulikia lazima zizingatie misingi
ya utawala bora, haki na demokrasia.
“Mfumo wa kushughulikia matatizo au kasoro za kitaaluma katika vyombo
vya habari ni kandamizi kwani unamfanya waziri kuwa na mamlaka ya kutoa
adhabu kwa kuzingatia mtizamo wake, hata kama mtizamo huo unakinzana na
misingi ya taaluma,” alisema.
Meena alisema kuwa uamuzi wa Waziri Nape unaonekana hauna nia njema
ndani yake kwani kifungu cha 28 cha sheria ya Mamlaka ya Mawasiliano
nchini (TCRA) alichotumia kutoa adhabu hiyo, hakimlazimishi kufungia
vituo vya redio kama alivyofanya.
“Kosa la vituo hivyo kwa mujibu wa waziri ni uchochezi, lakini
hakuweka bayana maudhui ya vipindi au habari ambazo zilivifanya vituo
hivyo ‘kutiwa hatiani’ na baadaye kufungwa kwake kwa muda usiojulikana.
Kwa sababu hiyo si rahisi kwa waandishi wengine wa habari kujifunza kwa
makosa ya wenzao kwa kuwa mchakato uliotumika kushughulikia suala hilo
umebaki kuwa siri ya waziri.
“Tunapinga uamuzi wa Serikali kuvifungia vituo hivyo bila sababu na
tunatoa mwito kwa Waziri Nape kutafakari upya suala hili na kuachana
kabisa na dhamira hiyo isiyokuwa na tija kwa nchi yetu,” alisema Meena.
Home
News
Slider
JUKWAA la Wahariri Tanzania lasikitishwa na kufungiwa kwa vituo viwili vya radio Tanzania.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment