Na Veoronica Romwald
DAR ES SALAAM
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman
Mbowe pamoja na Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Edward Lowassa
wamekamatwa na Jeshi la Polisi.
Viongozi hao walikamatwa jana jijini Dar es Salaam na askari polisi
waliokuwa wamevaa kiraia, baada ya kuvamia katika kikao cha Kamati Kuu
ya dharura ya chama hicho kilichokuwa kinafanyika katika Hoteli ya
Giraffe Ocean View.
Kikao hicho kilichoanza saa 5 asubuhi na kuhudhuriwa na viongozi
mbalimbali akiwemo Lowassa na wabunge wa chama hicho ambao ni wajumbe wa
Kamati Kuu.
Dalili za kuvunjwa kwa kikao hicho zilianza kujitokeza mchana, ambapo
ilipofika saa 8:30 hali ilibadilika ndani ya kikao hicho, baada ya
kufika maofisa wa polisi waliokuwa wamevaa kiraia na kuingia moja kwa
moja hadi ukumbini na kwenda meza kuu ambako alikuwa amekaa Mbowe pamoja
Katibu Mkuu, Dk. Vincent Mashinji na Naibu Katibu Mkuu upande (Bara),
John Mnyika pamoja na baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu akiwamo Edward
Lowassa pamoja na Profesa Mwesiga Baregu.
“Wakati kikao kikiwa kinaendelea waliingia polisi waliokuwa wamevaa
kiraia, licha ya kuzuiwa na walinzi wa chama hawakuelewa na kusema kuwa
wana ujumbe muhimu kwa viongozi wa chama.
“Pamoja na mabishano ya muda mrefu waliingia ndani ya ukumbi wakiwa kama
askari wanane na kwenda moja kwa moja meza kuu alipokuwa ameketi Mbowe
na kumtaka avunje kikao.
“Hata hivyo Mbowe aligoma na kusema kuwa wao wapo kisheria ndani ya
ukumbi ndipo wale polisi wakasema kwa kuwa amekaidi agizo hilo sasa
viongozi wote wanatakiwa kutii sheria na wao wenyewe waende Kituo Kikuu
cha Polisi cha Kati.
“…Kutokana na agizo hilo wajumbe wengi walibaki wamepigwa butwaa na
kulazimika kuahirisha kikao na kuongoza pamoja na viongozi hao kwenda
polisi,” alisema mmoja wa wajumbe wa Kamati Kuu.
Chanzo hicho kililiambia MTANZANIA kuwa muda wote polisi wakiwa ndani
ya ukumbi huo walikuwa wakihoji uhalali wa kikao hicho ikiwemo agizo
lililotolewa na Jeshi la Polisi la kuzuiwa kwa mikutano ya ndani pamoja
na ile ya hadhara.
Hata hivyo kadiri muda ulivyokuwa unakwenda polisi waliongeza nguvu
katika eneo hilo ambapo gari kadhaa za polisi zilionekana zikirandaranda
katika eneo hilo.
Namna walivyofikishwa Polisi
Ilipotimu saa 10:20 msafara kati ya maofisa wa Jeshi la Polisi na
viongozi hao uliwasili katika eneo la Kituo Kikuu cha Polisi Kati
(Central), ambapo viongozi hao walishuka ndani ya magari na kuingia moja
kwa moja katika chumba maalumu kwa mahoajiano.
Wakati wakiendelea na mahoajiano hayo baadhi ya wabunge na wanachama
walianza kuwasili ili kujua hatima ya viongozi wao ambao walikuwa chini
ya mikono ya polisi.
Hata hivyo walizuiwa kuingia ndani na kutakiwa kusimama mbali kabisa
na mlango wa kuingilia kituoni hapo hali iliyowalazimu kwenda kukaa
jirani eneo la stesheni.
Akizungumzia hatua ya kukamatwa kwa viongozi hao, Mbunge wa Iringa
Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema), alisema wameshangazwa na hatua
hiyo aliyoiita ya uonevu.
“Tulikaa Kamati Kuu kujadili mustakabali wa chama tulipo sasa na tufanye
nini kusonga mbele lakini kabla hatujafika mwafaka askari walituvamia
na kuwataka viongozi wetu kuvunja kikao,” alisema Msingwa.
Ilipofika saa 10:40 jioni wanasheria wa chama hicho wakiongozwa na
Tundu Lissu waliwasili kituoni hapo ambapo nao walijikuta wakizuiwa
kuingia ndani ya chumba cha mahojiano.
“Leo maajabu, haijawahi kutokea, chumba changu kimejaa wageni, “ alisema
Lissu akifananisha chumba hicho ambacho naye amehoajiwa mara kadhaa na
maofisa wa polisi wa kituo hicho.
Alisema hatua ya kukamatwa kwa viongozi wa Chadema si jambo la
kushangaza kwani pamoja na hali hiyo bado hawajakata tamaa na
wataendelea na harakati za kudai demokrasia ya kweli nchini.
“Viongozi wanakamatwa kwa sababu za kipuuzi zinazotolewa na Serikali,
Magufuli kabla hata hajamaliza mwaka mmoja wa uongozi wake amepoteza
kila sifa aliyokuwa aliyoanza kujipatia katika maeneo mengine.
“Kwa kuanzisha vita ya kuua demokrasia na atakumbukwa kwa kushindwa
kuirejesha nchi katika mfumo wa chama kimoja hatua ya kutolewa kwa amri
ya kuzuia vikao vya chama na maandamano ni haramu, wanasema tumekaidi
lakini si kweli vikao na maandamano ni halali kwa mujibu wa sheria na
tumeambiwa tuheshimu,” alisema Lissu
Alisema katika kikao hicho kulikuwa na wajumbe 178.
Wakati kina Lowassa wakihojiwa mwanamke mmoja mwenye umri wa makamu alizua tafrani katika geti la kuingilia kituoni hapo.
Hata hivyo haikufahamika bibi huyo alikuwa akihitaji kuonana na nani
na ingawa maofisa wa jeshi hilo walimzuia kuingia, lakini alipita chini
ya uzio wa geti hilo na kuingia ndani.
Muda kidogo mmoja wa maofisa wa jeshi hilo alimtoa nje ambapo aliondoka
katika eneo hilo. Wakati viongozi hao wakiendelea kuhojiwa waandishi wa
habari hawakuruhusiwa kuingia wala kusogea katika eneo hilo la polisi.
Kauli ya Sirro
MTANZANIA ilipomtafuta Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es
Salaam, Kamishna Simon Sirro, ili kujua sababua ya kushikiliwa kwa
viongozi hao, alisema kwamba wamewakamta viongozi hao ili kujua sababu
za wao kufanya mkutano hali ya kuwa imezuiwa.
Alisema mikutano hiyo imekuwa ikitumika kuchochea wananchi na
kuwahamasisha kuvunja sheria za nchi kwa kufanya mapambano na Jeshi la
polisi
“Ni kweli tunawashikilia viongozi kadhaa wa Chadema akiwemo Lowassa
na Mbowe na kubwa tunataka kujua kikao chao wamefanya kwa sababu gani
hali ya kuwa vimepigwa marufuku lakini wao wameendelea kufanya.
“Lakini pia tunataka kujua kwanini wanahamasisha maandamano wakati
yatapelekea uvunjivu wa amani. Suala la kutolewa kwa dhamana siwezi
kulisema kwa sasa maana bado tunaendelea na mahojiano nao,” alisema
Kamanda Sirro alipozungumza na gazeti hili jana saa moja usiku.
Hata hivyo taarifa zilizopatikana jana usiku wakati MTANZANIA likienda
mtamboni zilieleza kuwa, viongozi hao wa Chadema waliachiwa kwa dhamana.
Marufuku ya Polisi
Wiki iliyopita Kamishna Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi
nchini, Nsato Msanzya (CP), alitangaza jeshi hilo, kupiga marufuku
mikutano ya ndani yenye viashiria vya uchochezi na hata ikifanyika
kwenye majukwaa watamshusha muhusika na kumfikisha kwenye mkono wa
sheria.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment