NYOTA wa klabu ya Manchester City, Sergio Aguero, ameanza msimu
vibaya baada ya usiku wa juzi kuamkia jana kupewa adhabu na Chama cha
Soka nchini England (FA).
Mshambuliaji huyo hatari ambaye amekuwa akitoa mchango mkubwa hasa
katika michezo miwili ya awali ya Ligi Kuu kwa kuifungia jumla ya mabao
matatu, lakini mchezo huo wa juzi ulikuwa mgumu kwake katika dakika ya
75 baada ya kumchezea vibaya nyota wa West Ham, Winston Reid.
Kupitia mikanda ya video, Aguero alionekana akimpiga kiwiko beki huyo
wa klabu ya West Ham wakati akiwania mpira katika mchezo ambao
ulimalizika kwa Manchester City kushinda mabao 3-1.
Kutokana na kusambaa kwa video hiyo, chama cha soka nchini England
kimeamua kumfungia mchezaji huyo michezo mitatu kwa madai ya utovu wa
nidhamu uwanjani.
Mwamuzi wa mchezo huo, Andre Marriner, amedai kuwa hakuwa mbali na
eneo la tukio lakini hakukiona kiwiko hicho ila aliona kuwa Aguero
amemchezea vibaya mpinzani wake na kupigwa mpira wa adhabu.
Kutokana na hali hiyo ya Aguero kufungiwa michezo mitatu, ina maana
nyota huyo ataukosa mchezo muhimu dhidi ya wapinzani wao, Manchester
United kwenye uwanja wa Old Trafford, Septemba 10 mwaka huu.
Michezo mingine miwili ambayo ataikosa mchezaji huyo ni pamoja na
Bournemouth, kabla ya kwenda kwenye uwanja wa Liberty kuvaana na Swansea
City.
Hata hivyo, kocha wa klabu ya Manchester City, Pep Guardiola, amedai
kuwa tukio ambalo amelifanya mshambuliaji wake katika mchezo huo
hakuliona, hivyo anashindwa kulizungumzia.
“Sikuona chochote alichokifanya Aguero, hivyo siwezi kuelezea lolote,
nadhani hakuna ambacho alikifanya, lakini kama kweli kuna kitu kibaya
amefanya basi lazima tukubali.
“Hata kama tutamkosa Aguero katika mchezo dhidi ya wapinzani wetu
Manchester United, lakini ushindi ni pale pale, akili yangu kwa sasa
inawaza mchezo huo hivyo sina wasiwasi kumkosa Aguero,” alisema
Guardiola.
Hata hivyo, kwa upande wa kocha wa West Ham, Slaven Bilic, amedai
kuwa hata yeye hakuliona vizuri tukio hilo na suala la kumtoa mchezaji
wake lilikuwepo kabla ya tukio lenyewe.
“Sikuamua kumbadilisha Winston Reid kutokana na kuchezewa vibaya,
nilifanya hivyo kwa kuwa ulikuwa ni wakati sahihi wa kufanya hivyo,”
alisema Bilic.
Kocha huyo amedai kuwa wapinzani wake walistahili kushinda kutokana
na soka ambalo wameonesha kwa kuwa waliweza kufika kila wakati katika
lango.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment