SERIKALI
imeanza kuwashughulikia watumishi walionufaika na fedha za watumishi
hewa ambapo hadi sasa watumishi 839 wapo katika hatua mbalimbali
wakiwemo waliofikishwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(Takukuru) na wengine wanaendelea kuhojiwa polisi kwa ajili ya
kufikishwa mahakamani.
Sambamba na hilo, serikali inatarajia kutoa
ajira mpya 71,496 kwa mwaka huu wa fedha baada ya kukamilisha uondoaji
wa wafanyakazi hewa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na
Utawala Bora), Angella Kairuki aliyasema hayo wakati akizungumzia
utekelezaji wa mipango na mikakati ya wizara yake katika kipindi cha
‘Tunatekeleza’ kinachorushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC1).
Kairuki alisema,
“Kwa sasa tayari wapo watumishi wameshahojiwa na
kuchukuliwa maelezo yao polisi na upelelezi utakapokamilika
watachukuliwa hatua mbalimbali za kisheria, ikiwemo kufikishwa
mahakamani… Tunakamilisha ushahidi na tutawatangazia tutakapokamilisha,”
alisema.
Alisema waligundua kwamba kuna maofisa utumishi na wahasibu
ambao siyo waaminifu, badala yake walikuwa wakielekeza fedha kwa ndugu
zao na miradi yao na wengine walishastaafu lakini bado majina yao
yalikuwa yakiendelea kupokea mishahara wakati walitakiwa kuondolewa
kwenye mfumo.
Alisema kwa kipindi cha Machi mosi hadi Agosti 20 mwaka
huu, watumishi hewa waliogundulika ni zaidi ya 16,127 na kuisababishia
serikali hasara ya mabilioni ya fedha. Kwa kipindi cha Agosti pekee
watumishi hao hewa wangelipwa mishahara wangeisababishia serikali hasara
ya zaidi ya Sh bilioni 16.
“Uhakiki huu ni endelevu na tumegundua
changamoto kubwa katika usimamizi wa mishahara ni uadilifu kwa watu
waliokasimiwa madaraka. Maofisa Utumishi, Maofisa Utawala na Wahasibu
wamepewa madaraka lakini wengi wao siyo waaminifu, hivyo kwa sasa
tumeweka uwajibikaji kwa waajiri,” alisema.
Aidha alisema wanaufanyia
mfumo wao maboresho zaidi ili uweze kuchakata taarifa nyingi zaidi
ambapo pia sekta ya mishahara imeshushwa katika ngazi za chini zaidi
hasa katika sekta za elimu na afya ambazo zimekutwa na watumishi hewa
wengi zaidi ili waweze kuwa na taarifa za mtumishi mmoja mmoja.
Alisema
upo muongozo ambao fedha za serikali zinaporejeshwa zinapitia hazina na
kusisitiza kwamba wataendelea kuhakikisha wanasimamia fedha zote ambazo
zilichukuliwa serikalini kinyume na utaratibu na isivyo halali
zinarudishwa kwa mfumo sahihi.
Pia alisema wameongeza kasi ili
kuhakikisha kunakuwa na nidhamu ya kazi na uwajibikaji kwa watumishi wa
umma, hivyo wanaanda mkataba wa utendaji kazi kwa watumishi wa umma na
ikiwezekana utaanza kutumika mwaka ujao wa fedha.
Alisema serikali
imefanya maboresho makubwa katika mishahara na motisha kwa ajili ya
maslahi ya watumishi wa umma, sambamba na kuhimiza taasisi mbalimbali
kuweka vitendea kazi ili kuwawezesha wafanyakazi kutekeleza majukumu yao
ipasavyo.
Akizungumzia ajira hizo mpya Kairuki aliwatoa hofu
watanzania waliokuwa wanatarajia ajira serikalini na kusisitiza kwamba
walichokuwa wanasubiri ni takwimu halisi kwa taasisi ili kujua ni
watumishi wangapi wameondolewa.
“Baada ya kukamilisha mchakato huo,
hatua nyingine zitaendelea… Hii ni neema kwa waliomaliza vyuo, cha
msingi wavute subira maana tutatoa ajira 71,496 kwa mwaka huu wa fedha
na hatukuzifuta ajira.
"Nawashauri vijana wasijiingize kwenye makundi yasiyofaa wasubiri ajira zinakuja,” alisema.
Katika
hatua nyingine, Kairuki alisema, wamepokea malalamiko zaidi ya 200
kutokana na ukiukwaji wa sheria ya maadili ya viongozi wa Utumishi wa
Umma ambayo inamnyima mtumishi kutotumia madaraka yake vibaya.
“Katika
malalamiko hayo 142 yanahusu sheria ya maadili. Sekretarieti ya Maadili
imefanya uchunguzi wa awali na malalamiko 12 yataanza kufikishwa Baraza
la Maadili na hatua mbalimbali zinaweza kuchukuliwa ikiwemo kushushwa
vyeo au kuachishwa kazi,” alisema.
Pia aliwaagiza maofisa utumishi
kuwahudumia watumishi na kuwapa haki zao ikiwemo kuwapandisha madaraja
kwa wakati pale wanapostahili. Aidha Kairuki alikemea tabia ya baadhi ya
watu kughushi taarifa za utumishi wa umma na kusisitiza kwamba jambo
hilo ni kosa kubwa kwa yeyote anayefanya hivyo.
“Mtu yeyote ambaye
anatoa nyaraka za serikali na siyo mlengwa au anayetoa nyaraka ambayo
imewekewa zuio kwa mujibu wa sheria ni kosa la jinai na hatua kali za
kisheria zitachukuliwa dhidi yake. Tunawasisitiza watumishi wa umma
kuhakikisha wanazingatia sheria hizo na mwongozo wa utoaji nyaraka na
kumbukumbu za taarifa za serikali,” alisema.
Home
News
Slider
SERIKALI imeanza kuwashughulikia watumishi walionufaika na fedha za watumishi hewa.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment