KOCHA mkuu wa timu ya Yanga, Hans van der Pluijm, ametoa siri ya
ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya African Lyon, akidai kwamba ulitokana na
kuwasoma kwa makini wapinzani wao katika mchezo wao wa kwanza
waliocheza dhidi ya Azam FC.
Juzi Yanga walianza vema mchezo wao wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania
Bara, wakifanikiwa kuondoka na ushindi huo mnono katika Uwanja wa Taifa
Dar es Salaam.
Akizungumza Dar es Salaam juzi baada ya kumalizika kwa mchezo, Pluijm
alisema amefurahi kuanza ligi vizuri kwa kupata ushindi mnono.
“Mchezo ulikuwa mgumu kwa pande zote mbili kwani wapinzani wetu
walifanya mashambulizi kuhakikisha wanapata ushindi, lakini umakini wa
wachezaji wangu ulisaidia kutopata nafasi hizo,” alisema.
Alisema bao la kwanza lilizidisha morali kwa wachezaji wake, ambapo
baada ya kufanya mabadiliko kipindi cha pili, walizidisha mashambulizi
yaliyopelekea kufunga mabao mengine.
Kocha huyo raia wa Uholanzi, aliongeza kuwa kikosi chake kinazidi
kuimarika licha ya kukabiliwa na baadhi ya majeruhi kama Juma Abdul,
Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Ally Mustafa ‘Barthez’ na Obrey Chirwa.
Pluijm aliendelea kusema atahakikisha anayafanyia kazi mapungufu
yaliyojitokeza kwenye mchezo huo ili yasijitokeze kwa mara nyingine.
Wakati huo huo, kocha mkuu wa timu ya African Lyon, Bernardo Tavares,
amekiri timu yake kutocheza kwa kiwango kizuri kwenye mchezo huo kama
ilivyokuwa mchezo uliopita dhidi ya Azam FC.
Tavares alisema kipindi cha kwanza wachezaji wake walikuwa wanacheza
kwa kulinda sana lango lao bila kushambulia, hivyo kuwapa mwanya
wapinzani wao kupata bao la mapema.
“Mchezo uliopita kikosi changu kilicheza kwa kiwango kizuri sana na
kufanikiwa kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Azam FC ila leo (jana),
walitengeneza nafasi za kufunga lakini hawakupata bahati ya kufunga,”
alisema.
Alisema licha ya kutopata ushindi, anawapongeza wachezaji wake kwa
kuendelea kucheza bila kukata tamaa hadi mwisho wa mchezo, akiahidi
kwenda kuyafanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza kwenye mchezo huo ili
yasijitokeze kwa mara nyingine
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment