SIMBA jana ilisherehekea vizuri miaka 80 tangu ilipoanzishwa baada ya
kuichabanga AFC Leopards ya Kenya mabao 4-0 katika mchezo wa tamasha la
`Simba Day’ kwenye Uwanja wa Taifa.
Kocha Mkuu wa timu hiyo, Joseph Omog juzi aliwataka wanachama,
wapenzi na mashabiki wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi Uwanja wa Taifa
kushuhudia kikosi kitakachotwaa taji la Tanzania Bara msimu wa mwaka
2016/2017.
Simba ilipata bao la kuongoza katika dakika ya 38 lililowekwa kimiani
na Ibrahim Ajibu baada ya kupiga shuti kali la moja kwa moja akipokea
pasi ya Mussa Ndusha.
Mchezaji hodari Laudit Mavugo alidhihirisha makali yake pale
aliposaidia kupatikana kwa bao la pili lililofungwa tena na Ajib baada
ya kumtengenezea mpira safi alioujaza wavuni katika dakika ya 57.
Shiza Kichuya aliyejiunga akitokea Mtibwa, aliiandikia Simba bao la
tatu katika dakika ya 66 akimalizia kazi nzuri ya Ajibu na Mavugo, ambao
waligongeana vizuri kabla mpira haujamkuta mfungaji aliyeujaza wavuni.
Wekundu hao wa Msimbazi waliandika bao la nne lililofungwa na Mavugo
baada ya kufanya kazi nzuri uwanjani.
Simba awali walikosa mabao mengi na hii ilitokana na kutoelewana kwa
Frederic Blagnon na Kichuya. Wenyeji Simba walifanya shambulizi la nguvu
katika dakika ya 28 na kupata kona kupitia kwa Mohamed Hussein
‘Tshabalala’.
Hata hivyo, kona hiyo haikuzaa matunda. Awali, Ajibu nusura aigharimu
timu yake baada ya kumchezea rafu Jack Kiyai wa AFC Leopards na
kupatiwa kadi ya njano katika dakika ya 35 na kuamuriwa upigwe mpira wa
adhabu, ambao haukuzaa matunda.
Safu ya kiungo ya Simba imeonekana kuimarika zaidi ikiongozwa na
Jonas Mkude, ambapo hadi kipindi cha kwanza kinamalizika, timu hiyo
ilikuwa mbele kwa bao 1-0.
Katika kuadhimisha miaka 80 tangu kuzaliwa kwa klabu hiyo, Mkuu wa
Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda, Hamisi Kingwangalla, Profesa
Athumani Kapuya, Mohamed Dewji `Mo’, pamoja na viongozi wa Simba,
walikata keki wakati wa mapumziko.
Simba: Vicent Agban, Jonas Mkude, Mohamed Hussein, Janyie Buifunga,
Novaty Lufunga, Method Mwanjale, Mwinyi Kazimoto, Mussa Ndusha, Frederic
Blagnen, Ibrahim Ajib na Shiza Kichuya.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment