MKURUGENZI wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi mkoani Morogoro,
Marcelin Ndimbwa amemsimamisha kazi mara moja Ofisa Kilimo na
Umwagiliaji wa wilaya hiyo, Martin Mhode kwa tuhuma ya kukaidi maagizo
ya wakuu wake wa kazi.
Pamoja na kudaiwa kukaidi maagizo ya Mkurugenzi na Mkuu wa Wilaya ya
Malinyi, Ofisa Kilimo huyo amedaiwa kushindwa kusaidia kufanikisha agizo
la Rais John Magufuli la kuwataka watendaji wa serikali kuwasimamia
wananchi kufanya kazi.
Akizungumza na gazeti hili mjini Malinyi wakati wa Maadhimisho ya
Sikukuu ya Wakulima ya Nanenane, Ndimbwa alisema Ofisa Kilimo huyo
alikaidi agizo la kumtaka kuhakikisha matrekta ya halmashauri hiyo,
yanapelekwa mashambani muda wote ili kulima mashamba ya wakulima.
“Mimi na Mkuu wa Wilaya tuliagiza matrekta ya halmashauri kuwepo
mashambani na kulima muda wote ili kufanikisha malengo ya halmashauri
katika kuhamasisha wakulima waliounda vikundi kushiriki katika kilimo
cha umwagiliaji ndani ya mradi wa umwagiliaji wa halmashauri. “Lakini
kinyume cha maagizo hayo, alikaidi na kuagiza matrekta yatoke shambani
na yaegeshwe katika ofisi za Halmashauri kwa kisingizio kwamba amechukua
hatua hiyo kutokana na wananchi kugoma kusafisha mashamba,” alisema.
Mkurugenzi huyo alisema kitendo hicho ni upuuzwaji wa mamlaka za
serikali na pia kinakwamisha maagizo ya Rais ya kutaka viongozi kuwa
chachu ya kuwafanya wananchi, kupenda kufanya kazi kwa bidii ili
kujiharakishia maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.
“Kama mnavyokumbuka hivi karibuni wakati akiwahutubia wakurugenzi,
Rais alitutaka kuwasimamia watendaji katika ngazi za halmashauri
kuhakikisha mipango ya maendeleo inafanikiwa na si inarudi nyuma. “Ni
jambo la ajabu, Ofisa Kilimo anakwamisha jitihada za kukuza kilimo, kwa
visingizio visivyo na msingi. Kazi yake ni kuwahamasisha wananchi
kushiriki kikamilifu katika kilimo ili kujiharakishia maendeleo na si
kukwamisha mipango tuliyojiwekea,” alisema.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi huyo amewataka Ofisa Kilimo na
Umwagiliaji Msaidizi, Samwel Kuziganita na Ofisa Mifugo, Absalum Gepson
kutoa maelezo ya kwa nini wasichukuliwe hatua za kinidhamu, ikiwa ni
pamoja na kusimamishwa kazi, kwa kufanya kazi kwa mazoea na chini ya
kiwango ndani ya halmashauri hiyo.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment