SIKU mbili baada ya gazeti hili kuchapisha habari kuhusu ugonjwa wa
homa ya ini (Hepatitis B), kuwa hatari kutokana na kutokuwa na tiba,
Serikali imeeleza sababu zilizochangia ugonjwa huo kugeuka kuwa tishio.
Katika toleo la juzi, gazeti hili lilieleza kuwa ugonjwa wa homa ya
ini ni hatari kwa vile, unaua idadi kubwa ya watu kimya kimya, ambapo
kati ya watu 100, watu wanane wanaweza kuwa na maambukizi sugu ya
ugonjwa huo.
Ilielezwa pia kuwa maambukizi ya ugonjwa huo ni makubwa mara 10 zaidi
ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi na kwamba asilimia kubwa ya
wagonjwa, huugundua wakati ugonjwa uko kwenye hatua za mwisho na hivyo
kusababisha mgonjwa kupoteza maisha.
Hayo yalibainishwa na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Mfumo wa Chakula
na Ini, ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Magonjwa ya Tumbo na Ini,
Idara ya Tiba katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk John
Rwegasha katika mahojiano maalumu na gazeti hili juzi.
Hata hivyo jana akizungumzia ugonjwa huo na hatua zinazochukuliwa na
serikali, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,
Ummy Mwalimu alisema ugonjwa huo umekuwa tishio kwa vile haujapewa
kipaumbele cha kutosha.
Mwalimu alisema maambukizi ya ugonjwa huo kwa hapa nchini
yanaongezeka na kwamba pamoja na kuongezeka huko nchi haikuwa na takwimu
sahihi zinazoonesha ukubwa wa tatizo.
Alisema baada ya kuona ukubwa wake, hivi sasa wizara imeanza mchakato
wa kufanya marejeo ya Sera ya Afya ya Mwaka 2007 ili kuingiza ugonjwa
huo kwenye magonjwa ya vipaumbele.
“Ni kweli ugonjwa huu ni hatari na kasi ya maambukizi hivi sasa
inaongezeka, ingawa hatuna takwimu sahihi tulizozifanya wenyewe kwa kuwa
hatukuupa kipaumbele ugonjwa huu kwa siku za nyuma, ila sasa tumeona
ukubwa wa tatizo na tumeanza kuchukua hatua,” alisema Ummy.
Waziri huyo alibainisha kuwa serikali ilitilia mkazo zaidi kwenye
chanjo kwa watoa huduma walio kwenye sekta ya afya tena kwa wale
wanaohusika zaidi au moja kwa moja na wagonjwa na kuongeza kuwa kutokana
na ukubwa wa tatizo kuna haja sasa ya kuangalia upya sera ya afya.
Alisema baada ya kufanya mapito ya sera hiyo wataangalia jinsi ya
kujikita zaidi kwenye kinga ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo, ambao
idadi kubwa ya wananchi hawana uelewa wa ugonjwa huo na athari zake,
hadi pale mgonjwa anapougua.
Juzi akizungumzia dalili za homa ya ini, kwa aina zote mbili yaani B
na C, Dk Rwegasha alisema mtu mwenye ugonjwa huo ni vigumu kumtambua
hadi pale vipimo vya damu vitakapofanywa na kwamba kwa hapa nchini,
hakuna mazoea ya kupima ugonjwa huo, hadi pale dalili zinapokuwa
zimeanza kuonekana kwenye mwili wa mtu.
Dalili za ugonjwa huo kwa mujibu wa Dk Rwegasha ni pamoja na homa,
tumbo kuuma upande wa juu kulia, kichwa mafua, macho kuwa na njano na
wakati mwingine hata mkojo kuwa njano na pia wakati mwingine mtu
aliyeathirika na ugonjwa huo hana dalili.
Alisema ugonjwa huo ni hatari na wakati mwingine zaidi ya Ukimwi kwa
sababu ni ugonjwa unaoua watu wengi kimya kimya, na mtu anapogundua kuwa
ameathirika na tatizo hilo, huwa ni kwenye hatua za mwisho na hivyo
mgonjwa hupoteza maisha.
Home
Afya
Slider
Waziri afichua mapya kuhusu ugonjwa wa ini*kati ya watu 100 wanane wana maambukizo.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment