WAFUASI wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa
Ibrahim Lipumba, wametangaza kwenda kwa Msajili wa Vyama vya Siasa
kuwasilisha malalamiko yao ya kupinga utaratibu uliofanywa na wajumbe wa
Mkutano Mkuu cha chama hicho.
Wakati wanachama hao wanaomuunga mkono Prof. Lipumba wakidai hayo,
CUF imetoa msimamo wake na kusema kuwa imeshamalizana na kiongozi huyo
na kilichobaki sasa ni kujiandaa kujaza nafasi za uongozi zilizo wazi.
Taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na
Mawasiliano ya Umma, Salim Bimani, ilieleza kuwa wajumbe wengi wa
Mkutano Mkuu Maalumu uliofanyika juzi walipiga kura ya kuridhia
kujiuzulu kwa Prof. Lipumba na kwamba mchakato wa kujaza nafasi hizo
utafanyika.
“Ni muhimu kukumbuka kwamba ajenda ya kwanza ya msingi katika Mkutano
Mkuu imekamilika kwa wajumbe wengi kukubali kujiuzulu kwa mheshimiwa
Prof. Lipumba.
“Mchakato wa kukamilisha zoezi la kujaza nafasi wazi za uongozi wa
chama taifa upo palepale na baada ya kukamilisha taratibu za ndani ya
chama, tutatoa taarifa kwa Watanzania wote.
“Chama kinapenda kuwataarifu na kuwahakikishia wanachama, wapenzi wa
chama chetu na marafiki zetu wote kuwa hii ni taasisi kubwa ya kisiasa
nchini iliyo na viongozi makini na mahiri,” alisema Bimani.
Mkurugenzi huyo wa uenezi, alisema kuwa mchakato wa kumwondoa rasmi
Prof. Lipumba katika nafasi yake ulifanyika kwa mujibu wa katiba ya
chama hicho.
Alisema kura zilipigwa baada ya kutimia kwa akidi ya wajumbe halali
waliopaswa kuhudhuria mkutano huo, na kwamba kwa mujibu wa Katiba ya CUF
ya mwaka 1992 ibara ya 79(3) toleo la mwaka 2014, walipaswa kumchagua
mwenyekiti atakayesimamia zoezi hilo.
“Baada ya kuona akidi imetimia, wajumbe walimchagua Julius Mtatiro
kusimamia suala la upigaji wa kura, ambapo waliotaka Prof. Lipumba
aondoke walikuwa 476 na waliopinga walikuwa wajumbe 14, huku wengine
wakikataa kupiga kura,” alisema Bimani.
Aliongeza kuwa kutokana na hali hiyo, Prof. Lipumba si mwenyekiti
tena wa chama hicho, na kwamba wanachama wanapaswa kuwa watulivu katika
kipindi hiki, na kuzipuuza taarifa zote zenye lengo la kupotosha usahihi
wa suala hilo.
WATETEZI WA LIPUMBA
Kutokana na uamuzi huo, wafuasi wanaomuunga mkono Prof. Lipumba,
wamepinga uamuzi huo na kutangaza kwenda kwa Msajili wa Vyama vya Siasa,
Jaji Francis Mutungi, kueleza kilichotokea ikiwamo kuvunjwa kwa
utaratibu.
Akizungumza na MTANZANIA nje ya Ofisi Kuu ya CUF, Buguruni Dar es
Salaam jana, Mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Serengeti, Joseph Magoiga,
alisema kura zilizopigwa si halali kwa sababu hazikuwa za siri kwa
mujibu wa Katiba ya CUF.
Alisema kitendo hicho ndicho kilichosababisha vurugu, huku wajumbe
wengine wakisusia utaratibu huo na kutoka nje ya ukumbi wa mkutano.
“Mtatiro aliwaambia wajumbe wanaomtaka Profesa Lipumba kunyoosha
vidole juu ili aweze kuwahesabu, lakini sisi tulisimama wote na kusema
hatutaki kwa sababu katiba ya chama inataka kupiga kura za siri na si ya
kunyoosha vidole juu,” alisema Magoiga na kuongeza:
“Pamoja na wajumbe kugoma kupiga kura, lakini Maalim Seif (Sharif
Hamad, Katibu Mkuu CUF) alimwambia Mtatiro aendelee kuhesabu wajumbe
walionyoosha mkono na akatangaza matokeo katika hali ya vurugu. Kutokana
na hali hiyo jana (juzi) tuliorodhesha majina zaidi ya 300 ya wajumbe
wa Tanzania bara, tutakwenda kwa Msajili wa Vyama vya Siasa ili tuweze
kumweleza kilichotokea ndani ya mkutano huo.
“Suala hili tutalifanya pamoja na kumwandikia barua ya kupinga uamuzi
uliotolewa na Maalim Seif pamoja na watu wake,” alisema Magoiga.
MTATIRO AELEZA
Kwa upande wake, aliyekuwa Mwenyekiti wa muda wa Mkutano Mkuu huo,
Mtatiro, jana alitoa taarifa huku akieleza mambo 15 yaliyotokea.
Alisema akidi ilitimia kwa pande zote – bara na Zanzibar, na
alichaguliwa kwa kura zaidi ya 500 kuwa mwenyekiti wa muda. Aliyemfuatia
alikuwa ni Ridhiwani wa Morogoro aliyepata kura 170.
“Baadhi ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CUF wapatao 10 kutoka Tanzania
Bara walitoa hoja zao kwa kutaka kikao kimwite Prof. Lipumba ili aje
ajieleze kuhusu kujiuzulu kwake jambo ambalo lilipingwa na wajumbe
wengine,” alisema.
Alisema alipowataka wajumbe wanaotaka Lipumba aletwe kueleza kifungu cha katiba au kanuni kinachotaka hivyo walishindwa kueleza.
Kwa upande wa wajumbe waliokataa Prof. Lipumba kufika mkutanoni,
alisema walinukuu ibara ya 117(2) ambayo inataka taarifa ya kujiuzulu
kwake ndiyo ipelekwe kwenye mkutano mkuu na si yeye mwenyewe.
Alisema aliujulisha mkutano kuwa Prof. Lipumba si mjumbe wa kikao,
kwa hiyo hawezi kuitwa na kwamba mkutano ujadili barua zake na ufanye
uamuzi wa kumrudisha au kutomrudisha.
“Baadhi ya wajumbe wa mkutano mkuu kutoka Tanzania Bara walikataa
mkutano usifanye maamuzi yoyote, huku wengine wakitaka maamuzi
yafanyike.
“Kwa hiyo Tanzania Bara iligawanyika nusu kwa nusu kwenye jambo hilo.
Hofu ya wajumbe wa Bara waliokataa maamuzi yasifanywe ilikuwa ni kuwa
yakifanyika yataathiri mipango yao,” alisema Mtatiro.
Alisema wakati wakijadiliana suala hilo, Prof. Lipumba alijitokeza
akiwa na kundi la mabaunsa wapatao 30 wakisindikizwa na ofisa wa polisi
aliyekuwa na ‘radio call’.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)


0 comments:
Post a Comment