HALMASHAURI ya Wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa, imewaondoa wauguzi 13
kwenye orodha ya malipo baada ya kubainika kuwa wana vyeti feki.
Aidha, Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo, limemfukuza kazi na
kumtoa kwenye orodha ya malipo mhudumu wa zahanati iliyopo kijijini
Mkombo, Winfrida Ngulo baada ya kukiri kuwa vyeti alivyokuwa navyo ni
feki.
Pia madiwani wameagiza muuguzi Daraja la Pili aliyekuwa akifanya kazi
kwenye zahanati hiyo ya Mkombo, Fatuma Efanga anayetuhumiwa kutoroka na
zaidi ya Sh 700,000 zikiwa ni michango ya Mfuko wa Bima ya Afya ya
Jamii (CHF) zilizochangwa na kaya maskini ili wahudumiwe kwenye zahanati
hiyo.
Muuguzi huyo inadaiwa alikimbia na fedha hizo baada ya kubainika kuwa na vyeti feki.
Baraza hilo lililazimika kukaa kama kamati ili kumjadili na kumtolea
maamuzi mhudumu huyo Ngulo ambaye inadaiwa alipofikishwa mbele ya
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) alikiri kuwa na
vyeti feki .
Awali akichangia kwenye kikao cha baraza hilo, Diwani Mwachusa
Sinjela alitahadharisha kuwa watumishi hewa na wenye vyeti feki wakipata
taarifa kuwa wamebainika wamekuwa wakitoroka na kusababisha hasara.
“Mfano ninao kuna mtumishi wa afya (Fatuma) kwenye kata yangu
nimepata taarifa kuwa ametoroka kituoni na fedha za michango ya CHF
kiasi cha Sh 700,000 na hajulikani alikojificha,” alidai Sinjela.
Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Dk Arcado Mwamba alisema
orodha yote ya kaya maskini waliochanga fedha hizo CHF ipo na
inafahamika. Kwa mujibu wa Dk Mwamba, zahanati hiyo ya Mkombo ilikuwa na
watumishi wawili tu, Efanga na Ngulo ambao walikuwa wakitoa huduma.
“Kwa mantiki hiyo, zahanati hiyo kwa sasa haina mhudumu yeyote wa
afya ila tuko mbioni kuwapeleka huko wahudumu wengine wa afya,” alieleza
Dk Mwamba.
Akizungumza na gazeti hili nje ya baraza hilo, Ofisa Utumishi na
Utawala wa halmashauri hiyo, John Maholani alisema wauguzi wa afya 13
wameondolewa kwenye orodha ya malipo baada ya kubainika kuwa wana vyeti
feki.
Home
News
Slider
Wauguzi 13 waondolewa kwenye orodha ya malipo baada ya kubainika kuwa wana vyeti feki.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment