RAIS John Magufuli ameiagiza Bodi ya Pamba Tanzania (TCB) kuhamia
katika mikoa ya Kanda ya Ziwa na kuondoka Dar es Salaam, kwa sababu huko
ndiko ambako wakulima wengi wa zao hilo wanapatikana.
Aidha, ameionya bodi hiyo kwamba hataki kusikia kwamba imetoa tena
mbegu zisizoota kwa wakulima, na endapo hilo litatokea, atawatumbua
viongozi wake.
Rais Magufuli aliyasema hayo mjini Geita wakati akizungumza na
wananchi, akiendelea na ziara zake katika mikoa ya Singida, Tabora,
Shinyanga na Geita, ambayo aliianza mwishoni mwa wiki iliyopita.
Alisema inashangaza kuona kuwa Bodi ya Pamba iko Dar es Salaam wakati
wakulima wengi wa zao la pamba wanapatikana katika mikoa ya Kanda ya
Ziwa ya Geita, Mwanza, Shinyanga, Mara, Simiyu na Kagera, hivyo kuwataka
wahamie katika mikoa hiyo na kuwa karibu na wakulima hao.
Akiwa wilayani Kahama mkoani Shinyanga, alimtaka aliyekuwa Mbunge wa
Kahama, James Lembeli kurejea katika Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuwa
huko aliko (katika Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) amepotea
njia na kuna mafisadi.
“Wana-Kahama tambueni kuwa Lembeli ni rafiki yangu wa siku nyingi na
kuwepo kwake hapa ninategemea mabadiliko makubwa kutoka kwake na
ninakushauri urudi Tanzania, kwani ulikokwenda ulikuwa umepotea njia,”
alisema Rais Magufuli.
Aidha, alimtaka Lembeli kurudi CCM kwani huko alikoamua kwenda, ndiko
kwa sasa walipo hao mafisadi ambao alikuwa akiwazungumzia kila siku.
“Ninakuomba Lembeli urudi kundini, mimi ninakujua unavyowapenda
wananchi wako wa Kahama na ukirudi sitakukata mkia kwani huko
ulikokwenda umepotea njia na mimi ndio mwenyekiti ninayekuwa ninapigania
wanachama wasaliti ambao asubuhi wapo CCM jioni wapo Upinzani,” alisema
Rais Magufuli.
Kwa upande wake, Lembeli alisema aliamua kujitoa CCM na kujiunga na
Chadema kwa madai chama hicho kumekithiri kwa rushwa, ufisadi pamoja na
unafiki.
“Iwapo Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Taifa ambaye ni Rais John
Pombe Magufuli atakisafisha chama hicho, basi na mimi ninaweza kurudi
katika chama hicho kwa lengo la kuwahudumia wananchi,” alisema Lembeli
aliyeshindwa uchaguzi mwaka jana na mgombea wa CCM, Jumanne Kishimba.
Alisema anashukuru Rais Magufuli kwa kuja Kahama na kuongeza kuwa
yeye hana kinyongo na wataendelea kusalimiana, kwani kubadilisha msikiti
sio mwisho wa Uislamu.
Aidha, alisema kama Rais Magufuli akikisafisha chama hicho, hana budi
kurudi kundini kwani kwa sasa bado anasubiri kiongozi huyo kukisafisha
chama hicho, kwa kuwa kimejaa watu ambao hawana sifa ya kukiongoza.
Kwa upande wake, Rais Magufuli alisema yote aliyoyaahidi atayafanyia
kazi na kuongeza kuwa hatalewa madaraka ya Urais na kuwataka Watanzania
kumtanguliza Mungu katika kazi wanazozifanya za kila siku.
Akizungumza kwa niaba ya vyama vya upinzani, Mwenyekiti wa
NCCR-Mageuzi wilayani Kahama, Rajabu Yahaya alimpongeza Rais Magufuli
kwa kuchaguliwa kwake kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwani
kazi anazozifanya, ndio walizokuwa wakizipigania wapinzani katika
majukwaa na kumtaka kuendelea kutumbua majipu.
Akizungumzia masuala mengine, Rais Magufuli aliwaagiza wakurugenzi wa
halmashauri za wilaya nchini kuacha kuwatoza ushuru wafanyabiashara
ndogo kwani wao wao ndio waliosababisha CCM kupata ushindi katika
Uchaguzi Mkuu uliopita.
Alisema aliomba kiti hicho kwa ajili ya kutatua matatizo ya wananchi;
na kuongeza kuwa ushuru au kodi ilipwe kwa watu wanaomiliki maduka na
wafanyabiashara wakubwa waliopo katika maeneo husika.
Aidha, alisema katika uongozi wake hajaagiza wananchi wa kawaida
walipe kodi, bali alitaka wananchi waishi maisha ya amani hasa
wafanyabiashara ndogo ambao ndio walio wengi katika jamii iliyopo
nchini.
Akiwa Isaka, Rais Magufuli alisema hatalipa fidia kwa nyumba
takribani 300 kwa sasa, badala yake kazi kubwa atakayoifanya ni
kuhakikisha anamaliza tatizo la maji katika mji huo, ambalo linawasumbua
wananchi kwa muda mrefu. Imeandikwa na Raymond Mihayo na Kareny Masasi.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment