Image
Image

Wawili wakutwa wamekufa kwenye nyumba ya wageni ya Kings Rest House Dar es Salaam.


Watu wawili wamekutwa wamefariki katika nyumba ya wageni ya Kings Rest House iliyopo Mtaa wa Bumila, Gongo la Mboto jijini Dar  huku miili yao ikiwa imeungua moto. 
Mmiliki wa gesti hiyo, Damian Mng’ong’o alisema alifuatwa kanisani jana saa 1.30 asubuhi na kuambiwa kuna chumba kimoja katika gesti yake kinafuka moshi na aliondoka kanisani kuelekea ilipo nyumba hiyo. 
Alisema alipofika aliona moshi bado unafuka huku nje kukiwa na umati mkubwa wa watu wakishangaa.
“Tulifanya uamuzi wa kufungua mlango lakini hatukuona mtu yeyote chumbani, ndipo mmoja wa wafanyakazi alipofungua mlango wa choo ndani ya chumba tukakuta maiti mbili zikiwa zimechomwa. "
Alisema mhudumu wa gesti alitueleza kuwa jana (juzi) saa tano asubuhi alikuja mwanamume mmoja akachukua chumba na baadaye jioni alikuja kijana mwingine wakawa wameingia wote katika chumba hicho. 
“Baada ya muda nilipiga simu polisi kuripoti tukio hilo nao waliwasili ndani ya muda mfupi wakafanya uchunguzi wao na kuhoji baadhi ya watu, baadaye wakawaleta madaktari kupima, kisha wakaondoka na maiti hizo mbili kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya hatua nyingine.” 
Mfanyakazi wa jikoni katika gesti hiyo ambaye hakupenda jina lake litajwe alisema watu hao waliofariki ni wafanyabiashara wanaouza ng’ombe katika mnada wa Pugu na mara nyingi wakija Dar es Salaam hufikia hapo. 
“Wengi wanaofanya biashara ya ng’ombe wakija hufikia hapa, mpaka sasa sijajua kilichotokea kwa hawa waliokufa, lakini tukio hili limewashtua wenzao kwani baadhi walipoona tukio hili wameingiwa na hofu na kuondoka,” alisema. 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Salum Hamduni alisema wanaendelea kuchunguza na taarifa za awali hazijathibitisha kama waliuawa hapo gesti au sehemu nyingine na kupelekwa hapo. 
“Kuna viashiria kuwa huenda waliuawa wakaletwa pale kwani wana alama ya kamba katika shingo kama vile kuna mtu aliwanyonga na katika matumbo yao kuna majeraha kama wamechomwa kitu chenye ncha kali,” alisema na kuongeza: 
“Mpaka sasa uchunguzi unaendelea na Jeshi la Polisi linafanya kazi yake na tunasubiri taarifa kutoka kwa wataalamu wa masuala ya uchunguzi na alama za vidole ambayo itaeleza kwa nini wao waungue lakini nguo zao zisiungue. Pia kitanda na vitu vingine visiungue na kwa nini watu waende kuzima moto, wakati watu wameshafariki,” alisema Hamduni. 
Hamduni alisema mmoja wa waliofariki alijiandikisha kama Lameck Ludovick, mfanyabiashara na mkazi wa Dar es Salaam.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment