Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amemuagiza
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA),
kupunguza idadi ya vikao vya baraza visivyo na ulazima ili kuondokana na
matumizi mabaya ya fedha na badala yake fedha hizo zielekezwe kwenye
uendelezaji wa miundombinu ya bandari za maziwa.
Ametoa agizo hilo
mara baada ya kukagua shughuli za utendaji wa bandari ya Kasanga
iliyopo mkoani Rukwa inayohudumia mkoa wa Kigoma, nchi ya Burundi na
Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo (DRC) ambapo amebaini mapungufu ya
kiutendaji ikiwemo malipo yasiyotumia njia za kielektroniki na
miundombinu isiyo rafiki katika kukidhi ushindani wa kibiashara katika
bandari hiyo.
Waziri Mbarawa ameitaka TPA kuweka mfumo wa uendeshaji
vikao kwa njia ya kieletroniki (video conference) kwa lengo la kudhibiti
matumizi ya fedha nyingi zilizokuwa zikitumika katika uendeshaji wa
vikao hivyo.
“Nataka TPA muanze kutumia video Conference katika vikao
vyenu ili fedha zilizokuwa zikitumika zifanyie kazi nyingine za
maendeleo ya Taifa”, amesema Waziri Prof. Mbarawa.
Ameongeza kuwa
TPA imekuwa na wajibu mkubwa wa kuchangia pato la Taifa kupitia huduma
za upakiaji na upakuaji wa mizigo hivyo wanapaswa kuanza kutumia mfumo
wa kielekroniki katika ukusanyaji wa mapato katika bandari zote nchini
ili kudhibiti upotevu wa mapato.
“Tukianzisha mfumo wa kielekroniki
katika bandari hii tutakuwa na uwezo wa kufuatilia mapato yanayopatikana
katika utoaji wa huduma na kujua kama malengo yamefikiwa”, amesema
Prof. Mbarawa.
Katika Hatua nyingine Profesa Mbarawa amekagua
barabara ya Sumbawanga-Matai-Kasanga Port yenye urefu wa KM 112
inayojengwa kwa kiwango cha Lami na kumtaka Mkandarasi wa barabara hiyo
China Railway 15 Bureau Group Corporation kukamilisha ujenzi huo ifikapo
Julai mwakani.
Amesema kukamilika kwa barabara hiyo kutaunganisha
mji wa Sumbawanga na Bandari ya Kasanga na hivyo kurahisisha shughuli
za usafirishaji wa abiria na mizigo kutoka bandarini hapo na hivyo kuwa
kichocheo cha ukuaji wa uchumi katika Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.
“Kukamilika
kwa barabara hii kutawawezesha wananchi kusafirisha bidhaa zao, kutoka
sehemu moja hadi nyingine na hivyo kukuza uchumi wao na kuongeza pato la
Taifa”, amesisitiza Prof. Mbarawa.
Aidha Waziri Mbarawa amemuhimiza
Mkandarasi huyo kujenga barabara hiyo kwa viwango vilivyopo katika
mkataba na kuzingatia thamani ya fedha katika ujenzi huo ili kuwezesha
barabara hiyo kudumu kwa muda mrefu.
Naye Meneja wa Wakala wa
Barabara Nchini, Mkoa wa Rukwa Eng. Masuka Mkina amesema kuwa ujenzi wa
barabara hiyo umekamilika kwa asilimia 62 ambapo kukamilika kwa ujenzi
huo utatagharimu kiasi cha zaidi ya shilingi Bilioni 133.
“Mpaka
sasa Mkandarasi ameweza kukamilisha kujenga makalvati makubwa 11 kati ya
13, na makalvati ya kawaida 169 kati ya 241”, amesema Eng Mkina.
Waziri
Prof. Mbarawa yupo katika ziara ya kukagua miradi ya miundombinu na
kuangalia utendaji kazi wa taasisi zilizopo katika Mkoa wa Rukwa.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment