WENYE nyumba wamerudi! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya mabingwa
watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga jana kuanza vizuri kampeni zao kwa
ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya African Lyon katika mechi
iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Yanga imeanza kutetea taji lake baada ya kutupwa nje ya michuano ya
kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa kufungwa na TP Mazembe ya
Congo DR mabao 3-1 katika mechi ya mwisho ya makundi.
Ikicheza soka safi, Yanga iliichukua dakika 19 kuandika bao la
kuongoza lililofungwa na Deus Kaseke baada ya kuunganisha pasi safi ya
Simon Msuva.
African Lyon ambayo mechi ya kwanza ilitoka sare ya bao 1-1 na Azam,
jana ilizidiwa karibu kila idara na kuonekana kuchoka hasa katika
kipindi cha pili. Msuva aliiandikia Yanga bao la pili katika dakika ya
59 akiunganisha pasi ya Haruna Niyonzima kabla ya kumpiga chenga kipa wa
Lyon na kuujaza mpira wavuni.
Pamoja na kuelemewa huko, Lyon walijaribu kufanya mashambulizi ambapo
katika dakika ya 76 Tito Okello alishindwa kumalizia mpira wa krosi
akiwa amebaki peke yake na kipa.
Yanga iliendeleza mashambulizi na dakika ya 90, Amisi Tambwe alikosa
bao baada ya mpira wa kichwa aliopiga kugonga mwamba na mpira kurudi
uwanjani.
Zikiwa zimebaki sekunde chache mpira kumalizika, Juma Mahadhi
aliyeingia uwanjani kuchukua nafasi ya Msuva aliandika bao la tatu kwa
Yanga baada ya kazi nzuri ya Niyonzima.
Yanga itacheza mechi ya pili keshokutwa ambapo itamenyana na JKT Ruvu kwenye uwanja huohuo wa Taifa.
Kutoka kwenye uwanja wa CCM Kirumba Mwanza, Alexander Sanga anaripoti
kuwa wenyeji Toto Africans wameshindwa kuutumia vizuri uwanja wa
nyumbani baada ya kukubali kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Mbeya City.
Wageni Mbeya waliandika bao hilo katika dakika ya tano lililofungwa
na Haruna Shamte kwa mpira wa adhabu iliyokwenda moja kwa moja golini.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment