ILIKUWA Februari 2, mwaka 1974, katika mbio za mita 1,500 upande wa
wanaume kwenye fainali za mashindano ya Jumuiya ya Madola nchini
Christchurch, New Zealand ambapo Filbert Bayi alitumia dakika 3 na
sekunde 32.16.
Akiongoza kuanzia mwanzo wa mbio hizo hadi mwisho, Mtanzania pekee
aliyeweka rekodi duniani, Filbert Bayi, alimaliza mbio hizo ambazo
zinaelezwa kuwa ni miongoni mwa mashindano makubwa duniani.
Mwanariadha huyu nyota nchini, aliyezaliwa katika mkoa ulioko maeneo
ya Bonde la Ufa (Rift Valley), Arusha maarufu kwa kutoa wanariadha
wazuri hapa nchini, anasema hali ya hewa na mfumo wa maisha ya watu wa
mkoa huo unachangia kutoa maarifa kwa wakimbiaji wa mbio ndefu.
“Wazazi wangu walikuwa wakulima, wafugaji wa ng’ombe, nilipokuwa
mtoto, nilikuwa naangalia mbuzi na ng’ombe, nikiwa kwenye vichaka
nachunga mifugo, nawinda, nakimbia na mbwa, nakimbia na wanyama,
nafikiri hiyo ndiyo iliyonifanya niwe na stamina katika ukimbiaji.
“Kila asubuhi nilikuwa nakimbia kwenda shule na natakiwa kurudi kwa
chakula cha mchana, kisha natakiwa kurudi tena kwa masomo ya jioni,
hivyo unaweza kuhisi nilikuwa nakimbia kilomita nane kwa siku,”
anasema Bayi.
Kauli hii ya Bayi inaakisi matokeo ya riadha ya mwanariadha, Alphonce
Felix Simbu, kutoka Mkoa wa Singida aliyeshiriki mashindano ya Olimpiki
mwaka huu na kuibuka mshindi wa tano.
Simbu mwenye umri wa miaka 24, ameweka historia kwa taifa kwa kushika
nafasi ya tano, akitumia muda saa 2:11:15 katika mbio ndefu ‘marathon’
akiwaacha wanariadha 155 walioshiriki mbio hizo, lakini hakuweza kupata
medali yoyote.
Kabla ya kuelekea nchini Rio de Jeneiro, Brazil, kushiriki michezo
hiyo, Simbu amekuwa akijituma sana katika mazoezi na mke wake, Rehema
Daudi, anasema: “Kila siku huwa anafanya mazoezi asubuhi na kwenye
maeneo haya ya jirani na nyumbani na hasa maeneo ya milimani na amekuwa
akifanya hivyo kila siku,” alisema Rehema.
Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Antony Mtaka, anasema
kabla ya kuelekea kwenye michezo ya Olimpiki, Simbu aliweka kambi miezi
sita katika Chuo cha Wakala wa Misitu (FITI), kilichopo Siha mkoani
Kilimanjaro chini ya kocha wake, Fransic John, baada ya kufikia viwango
vinavyotakiwa na Shirikisho la Dunia la mchezo huo (IAAF).
Mfumo huo wa maisha ambao Bayi anasema unachangia kuwawezesha
wanariadha kufanya vizuri hivi sasa unatoweka na hivyo wanariadha
wanatakiwa kufanya mazoezi kwa mtindo wa kisasa.
Akizungumza na MTANZANIA SPOTIKIKI kuhusu wanamichezo walioshiriki
michezo ya Olimpiki iliyomalizika, Bayi anasema tunahitaji uwekezaji wa
kutosha iwapo tunataka kufanikiwa katika michezo kwani wanamichezo
wetu hawakuwa na maandalizi ya kutosha.
Licha ya mwanariadha, Simbu kufanya vizuri kwa kushika nafasi ya
tano, Mkenya, Eliud Kipchoge, alishinda mbio hizo na kutwaa medali ya
dhahabu.
Bayi ambaye ni Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki nchini (TOC),
anasema tunatakiwa kuwekeza kwa wanamichezo kwa kuweka programu za muda
mrefu kwa kuandaa wachezaji.
Anasema hatuwezi kufanya vizuri kama wenzetu wa nchi zilizoendelea
kama Marekani, Ufaransa, Ujerumani kama hatutapata makocha wenye uwezo
na viwango vya kimataifa.
Aidha, Bayi anasema wachezaji wanatakiwa kuandaliwa kwa muda mrefu kabla ya kwenda kushiriki katika mashindano ya kimataifa.
Licha ya mwanariadha huyu kijana kutoka Singida Kijiji cha Mampandu,
kufanya vizuri kwa kushika nafasi ya tano, Bayi amedai tunahitaji
uwekezaji mkubwa katika riadha kwa kuandaa vijana wakiwa na umri mdogo
na kwa muda mrefu.
Kama anavyosema Juma Ikangaa ambaye alitamba katika Olimpiki ya mwaka
1984 huko Marekani ambapo alishika nafasi ya sita akikimbia saa 2:11:10
na ile ya mwaka 1988 huko Soul, Korea akikimbia saa 2:13:06 na kushika
nafasi ya sita.
Wanariadha wenye historia ya kufanya vizuri katika mashindano makubwa
hapa nchini ni kama Bayi, Seleman Nyambui na Ikangaa ambao rekodi zao
zimekuwa nadra sana kufikiwa na wanariadha wetu hapa nchini.
Kiwango alichofikia mwanariadha huyu kijana ni kukimbia muda wa saa
2:19:00 alipokuwa akipeperusha bendera ya Tanzania katika michezo ya
Lake Biwa, iliyofanyika Desemba mwaka jana huko nchini Japan.
Hata hivyo, mwanzoni mwa mwaka huu, Simbu alivunja rekodi yake
mwenyewe pale aliposhika nafasi ya 3 katika mashindano hayo kwa kutumia
saa 2:09:19 hivyo kufuzu moja kwa moja katika michezo ya Rio mwaka huu.
Dalili za Simbu kufanya vizuri zilianza kuonekana tangu akiwa hapa
nyumbani, baada ya kujitosa katika mbio za Bagamoyo Marathon siku chache
kabla hajaelekea Rio, ambapo alishika nafasi ya kwanza.
Katika mbio hizo za Bagamoyo kwa upande wa wanaume kilomita 21, Simbu
kutoka Arusha aliibuka mshindi akitumia saa 1:03:56, ambapo kwa
asilimia kubwa mbio hizo ziliongozwa na wanariadha wengi kutoka Arusha.
Katika mbio hizo za Bagamoyo, Simbu alikuwa na Mtanzania Saidi Makula
aliyeshika nafasi ya nne, ambaye yeye katika Rio 2016 alishika nafasi
ya 43 hiyo ikiwa ni baada ya kufikia viwango kwa kukimbia marathon kwa
saa 2:13:25 mjini Casablanca, Morocco Oktoba mwaka jana.
Na ndoto yake ilitimia Aprili 3 mwaka huu aliposhiriki marathon ya Daengu, Korea baada ya kukimbia kwa saa 2:12:01.
Simbu anasema haikuwa rahisi kwake kushika nafasi hiyo kama watu
wanavyofikiria kwani alikuwa akikimbia huku akiwa na wanariadha
mashuhuri na wakongwe katika riadha, hivyo kuziona mbio hizo ngumu sana
kwake lakini hakukata tamaa.
“Sitakuja kusahau pale nilipofika km 20 nikiwa sambamba na Kipchoge,
aisee jamaa huyu anakimbia mbio za mwendokasi na kama ningejaribu
kushindana naye basi ningechemka na kubaki mwishoni, lakini niliona ni
bora niende na kasi ile ile niliyokuwa nayo na hatimaye nilifanikiwa
kushika nafasi hii,” anasema
Mwanariadha huyu anaongeza kuwa amejifunza mambo mengi ambayo amesema
kwa kiasi kikubwa yatamsaidia katika Olimpiki ijayo hapo mwaka 2020
huko Tokyo, Japan hivyo kutoa wito kwa Serikali kuhakikisha inaanza sasa
kampeni ya kutafuta medali.
“Hii ni mara yangu ya kwanza kushiriki lakini nimeweza kupambana kufa
kupona naamini kuwa kama Serikali itatuandaa mapema na kambi yetu ikiwa
ya kisasa tena ikiwezekana nje ya nchi nina uhakika medali itakuja
Tanzania,” alisisitiza mwanariadha huyu na kuongeza:
“Vita ya kusaka medali ianze sasa hivi na si kusubiri wakati
mashindano yanakaribia, nimegundua kuwa wanamichezo wengi waliokuwa Rio
waliandaliwa vizuri sana na nchi zao na ndio maana wamepata medali na
kama walizikosa basi walishika nafasi za juu,” anaongeza Simbu.
Wanariadha wengine ambao nao walishiriki katika michezo ya mwaka huu
ni pamoja na mwanamke pekee, Sara Ramadhani ambaye alishika nafasi ya
126 yeye akidai kuwa viongozi wake walimtelekeza akiwa kwenye mbio hizo
na kujikuta akiwa mwisho huku akikosa maji.
Saidi Makula ambaye na yeye alipambana na kushika nafasi ya 43,
anasema mbio hizo ni ngumu hivyo zinahitaji maandalizi ya kutosha na si
kama alivyojiandaa yeye.
Wakati Fabiano Joseph aliyeshika nafasi ya 112, anadai kabla ya
kwenda nchini humo miezi miwili kabla alipata matatizo ya mguu hivyo
aliposhiriki mbio hizo alitonesha mguu wake.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment