SERIKALI imemfikisha mahakamani mfanyabiashara Leonard Kamili maarufu
Materu (31) kwa tuhuma za kutishia kuipindua Ikulu kwa maneno.
Mshtakiwa huyo anayedaiwa kutoa maneno hayo kwa nia ya kumtisha Rais
Dk. John Magufuli alifikishwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Margareth Bankika.
Mshtakiwa huyo ni mkazi wa Moshi Baa kwa Diwani, jijini Dar es
Salaam, alifikishwa mahakamani hapo na kusomewa mashtaka na Wakili wa
Serikali, Diana Lukondo.
Wakili Lukondo, alidai kuwa mshtakiwa huyo alichapisha taarifa za uongo kupitia mtandao wa kijamii wa WhatsApp.
Akisoma mashtaka hayo Lukondo alidai mshtakiwa huyo alitenda kosa
hilo, Julai 17, mwaka huu sehemu isiyofahamika jijini Dar es Salaam.
Wakili huyo alidai mshtakiwa huyo siku hiyo huku akijua alichapisha
taarifa na kuiweka katika mtandao huo ikiwa na maneno ya uongo
yasemayo: “Magu ajiandae tunaenda kupindua mpaka Ikulu” alisema.
Inadaiwa ujumbe huo ulikuwa na nia ya kumtishia Rais Dk. John Magufuli.
Mshtakiwa akiwakilishwa na Wakili Neema Lamwai, alikana kutenda kosa
hilo, ambapo Wakili wa Serikali Diana alidai upelelezi haujakamilika na
kuomba kesi iahirishwe hadi tarehe nyingine kwa kutajwa.
Hakimu Margareth alitoa masharti ya dhamana kwa mshtakiwa ambayo
yalimtaka awe na wadhamini wawili watakaosaini dhamana ya Sh milioni
tano kila mmoja.
Mshtakiwa huyo alitimiza masharti ya dhamana, hivyo ameachiwa kwa
dhamana hadi Septemba 20, mwaka huu, kesi itakapokuja kwa kutajwa.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment