RAIS
wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCPHR), Jaji
Augustino Ramadhani, amestaafu utumishi katika mahakama hiyo, huku
akijivunia mafanikio ya kutafsiri maelezo muhimu ya mahakama hiyo kwa
lugha adhimu ya Kiswahili.
Jaji Ramadhani aliapishwa kuwa Jaji wa
Mahakama ya Afrika mwaka 2010 baada ya kustaafu nafasi yake ya Jaji Mkuu
wa Tanzania na mwaka 2014 alichaguliwa kuwa rais wa taasisi hiyo na
kufanikiwa kuitumikia kwa miaka sita.
Akizungumza katika viwanja vya
mahakama hiyo mjini hapa jana baada ya kumwapisha Jaji Marie-Therese
Mukamulisa kutoka Rwanda na Jaji Ntyam Ondo Mengue kutoka Cameron, Jaji
Ramadhani alisema anajivunia mafanikio aliyoyapata na kuomba maelezo
hayo muhimu ya lugha ya Kiswahili kuanza kutumika.
Alisema kuingia
kwa lugha adhimu ya Kiswahili ni mafanikio makubwa kutokana na ukweli
kuwa wakati alipokuwa akiingia kushika wadhifa wa rais wa mahakama hiyo
alikuta maelezo hayo yakiwa yamewekwa kwa lugha mbili tu – ya Kifaransa
na Kiingereza.
“Mafanikio haya ni makubwa kwani tumeweza kutafsiri
maelezo muhimu ya Mahakama ya Afrika kwa Kiswahili. Haya ni mafanikio
makubwa kwetu, hasa Tanzania tukiwa ndio wenye lugha yenyewe ya
Kiswahili.
“Kilichobakia sasa ni kianze kutumiwa tu kwani tayari Rais
Mstaafu Jakaya Kikwete alishazindua maelezo hayo mwishoni mwa mwaka
jana,” alisema Jaji Ramadhani aliyewahi kuchukua fomu ya kugombea urais
kupitia CCM mwaka 2015.
Jaji Ramadhani alisema mbali na kufanikiwa
kukiingiza Kiswahili, pia lugha Kiarabu inayoongoza katika Bara la
Afrika kwa kuzungumzwa na watu nayo iliingizwa katika maelezo hayo
muhimu ya mahakama.
Akielezea kuhusu nafasi ya Tanzania tena kushika
wadhifa huo wa Rais wa Mahakama ya Afrika, Jaji Ramadhani ambaye ni
Mchungaji wa Kanisa la Anglikana Zanzibar, alisema fursa hiyo itakuwa
wazi ifikapo mwaka 2018 endapo kutakuwa na Jaji atakayehitaji
kugombea.
Alisema Bara la Afrika katika utoaji wa majaji wa
mahakama hiyo lilijigawaa katika kanda tano ambazo ni Kanda ya Afrika
Kaskazini, Kusini, Mashariki, Magharibi na Kanda ya Kati ambapo kila
ukanda hutoa majaji wawili.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment