MAKAMU wa Rais wa zamani wa Uganda, Profesa Gilbert Bukenya,
amemfananisha Rais Yoweri Museveni na Rais wa zamani wa Tanzania,
Mwalimu Julius Nyerere huku akitoa mwito kwa Bunge kubadili katiba ili
atawale maisha.
Akiwa katika hoteli yake ya Katomi huko Wakiso Ijumaa iliyopita, Mbunge
huyo wa zamani wa Busiro, aliliambia gazeti la Observer kuwa Museveni ni
mwasisi wa taifa na hivyo anapaswa kutendewa maalumu.
Kwa marais watakaofuata, hata hivyo, Bukenya alisema, wanapaswa watii ukomo wa umri wa miaka 75 uliowekwa katika katiba.
“Lakini kwa Rais Museveni, tumwache aendelee. Ana mawazo mazuri,
lakini si kwa viongozi wengine, ambao lazima watii ukomo wa umri huo,”
Bukenya alisema.
“Museveni ni Mahathir Mohamad wa Uganda; hivyo, anapaswa kuachwa
aendelee ni kifaa maalumu, atuongoze hadi wakati wake utakapofika.”
Mahathir Mohamad, ambaye alitawala kwa miaka 22, alikuwa waziri mkuu
aliyeongoza kwa muda mrefu zaidi nchini Malaysia na anasifiwa kwa kuleta
mabadiliko yaliyoitoa nchi hiyo kutoka dunia ya tatu kwenda ya kwanza.
Mbali ya Mahathir Mohamad na Nyerere, pia alimlinganisha Museveni na
kiongozi wa zamani wa Singapore, Lee Kuan Yew, kwa kuongoza muda mrefu
na kuzipeleka nchi mahali panapostahili.
Bukenya, ambaye alipoteza umakamu wa rais mwaka 2011 na kiti chake
cha ubunge wa Busiro mwaka 2016, alisema Museveni amefanya mengi na
hivyo anapaswa kupewa kipengele maalumu katika katiba.”
Kwa mujibu wa Bukenya ambaye pia aliwahi kufarakana na Museveni kiasi
cha kutaka kupambana naye katika uchaguzi wa urais mwaka huu kabla ya
wawili hao kupatana, alisema kati ya viongozi wa zamani ni Museveni
pekee aliyeleta maendeleo makubwa kwa taifa hilo.
Museveni ambaye amekuwa akiwania urais pasipo ukomo wa mihula baada
ya ile miwili kuondolewa, amebakiza miaka mitatu kufikisha umri wa miaka
75, ambao ni ukomo kwa mtu kuwania urais.
Tayari chama chake tawala cha National Resistance Movement (NRM)
kimeanza harakati za kutaka kurekebisha kifungu cha katiba ili kumruhusu
Museveni aendelee kugombea urais wakati atakapomaliza muhula wake wa
tano mwaka 2021.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment