BEI za jumla na za rejareja za mafuta katika mikoa yote nchini,
isipokuwa mkoa wa Tanga, imeshuka ukilinganisha na bei za mwezi
uliopita, taarifa ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati
(Ewura) imeeleza.
Taarifa ya Ewura iliyosainiwa na Mkurugenzi Mkuu, Felix Ngamlagosi
inaeleza kuwa bei za rejareja kwa petroli imepungua kwa Sh 65 sawa na
asilimia 3.50, dizeli Sh 63 sawa na asilimia 3.43 na mafuta ya taa bei
imepungua kwa Sh 86 sawa na asilimia 4.88.
Taarifa hiyo ya Ewura ilisema kwamba bei za jumla, zimepungua pia na
mwezi huu petroli itauzwa kwa Sh 65.31 kwa lita sawa na asilimia 3.63,
dizeli Sh 63.39 sawa na asilimia 3.72, na mafuta ya taa Sh 85.93 sawa na
asilimia 5.20.
“Kushuka kwa bei za mafuta ya petroli katika soko la dunia na
kupungua kwa gharama za usafarishaji wa bidhaa za mafuta hayo kuja
nchini, ndizo sababu kuu zilizochangia kushuka kwa bei za mafuta katika
soko la ndani hapa nchini,” alisema Ngamlagosi.
Bei mpya za rejareja ambazo zitaanza kuuzwa leo katika Mkoa wa Dar es
Salaam kwa petroli itakuwa ni Sh 1,840, dizeli Sh 1,747 na mafuta ya
taa Sh 1,673.
Bei za jumla katika Mkoa wa Dar es Salaam petroli itauzwa Sh 1,731.51, dizeli Sh 1,639.29 na mafuta ya taa Sh 1,565.43 kwa lita.
Katika mji wa Arusha, petroli itauzwa kwa Sh 1,923, dizeli Sh 1,831
na mafuta ya taa Sh 1,757 wakati katika mji wa Mwanza petroli itauzwa
kwa Sh 1,989, dizeli Sh 1,897 na mafuta ya taa Sh 1,823.
Mkoani Kigoma katika Manispaa ya Kigoma Ujiji, petroli itauzwa kwa Sh
2,070, dizeli Sh 1,978 na mafuta ya taa Sh 1,904 wakati mkoani Kagera
katika manispaa ya Bukoba petroli itauzwa kwa 2,054, dizeli Sh 1,962 na
mafuta ya taa Sh1,888.
Kuhusu bei kwa Mkoa wa Tanga, taarifa hiyo ilieleza kuwa bei za jumla
na za rejareja kwa mafuta ya petroli na dizeli katika mkoa huo
zimeongezeka kidogo, ikilinganishwa na toleo la bei za mafuta hayo
lililopita ukilinganisha na mwezi uliopita.
Kwa mwezi huu, bei za rejareja kwa petroli imeongezeka kwa Sh 50 kwa
lita sawa na asilimia 2.64 na dizeli Sh 19 sawa na asilimia 1.03. Bei
katika manispaa ya Tanga, petroli itauzwa kwa Sh 1,932, dizeli Sh 1,822
na mafuta ya taa Sh 1,753. Bei za jumla mkoani humo kwa petroli itauzwa
kwa Sh 1,823.63 kwa lita, dizeli Sh 1,714.15 na mafuta ya taa Sh
1,644.59.
Ngamlagosi alisema kwa kulinganisha mwezi uliopita na bei za mwezi
huu, bei za jumla zimeongezeka kwa petroli Sh 49.61 kwa lita sawa na
asilimia 2.80 na dizeli Sh 18.57 sawa na asilimia 1.1.
“Ongezeko hili la bei limechangiwa kwa kiasi kikubwa na kupokea
mafuta mapya ya petroli na dizeli ndani ya mwezi wa Agosti 2016, ambayo
yalitarajiwa kupokewa mwezi wa Julai 2016 na pia kutokupokea mafuta
mapya ya petroli, dizeli na mafuta ya taa kutoka meli ya MT.NEVASKA LADY
ndani ya mwezi wa Agosti,” alisema Ngamlagosi.
Mkurugenzi mkuu huyo wa Ewura alisema kampuni za mafuta, zipo huru
kuuza bidhaa za petroli kwa bei ya ushindani, mradi tu bei hizo ziwe
chini ya bei kikomo, kama ilivyokokotolewa na fomula iliyopitishwa na
Ewura na ambayo ilichapishwa katika gazeti la Serikali la mwezi Februari
mwaka huu.
Ngalamgosi alisema wanunuzi wahakikishe wanapatiwa stakabadhi ya
malipo, inayoonesha jina la kituo, tarehe, aina ya mafuta yaliyonunuliwa
na bei kwa lita.
Alisema stakabadhi hiyo ya malipo, itatumika kama kidhibiti cha
mnunuzi wa mafuta, endapo kutajitokeza malalamiko ya ama kuuziwa mafuta
kwa bei ya juu kuliko bei kikomo au kuuziwa mafuta yenye kiwango cha
ubora kisichofaa.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment