JAJI Mkuu, Mohamed Chande Othman amesema kanuni za uendeshwaji wa
Mahakama Maalumu ya Ufisadi na Uhujumu Uchumi, zimeshakamilika na
wanasubiri kuanza kusikiliza kesi.
Jaji Othman alisema hayo jana Dar es Salaam wakati akitoa taarifa
kuhusu uzinduzi wa Mpango Mkakati wa Miaka Mitano na Mradi wa Maboresho
ya Huduma za Mahakama unaotarajiwa kufanyika kesho Kibaha mkoani Pwani.
Alisema, kanuni hizo tayari zimeshachapishwa na zimeanza kutumika
rasmi baada ya kutolewa tangazo katika gazeti la Serikali la Septemba 9,
mwaka huu.
Alifafanua kuwa kanuni hizo zinaeleza jinsi ya kufungua kesi na
kulinda mashahidi, kwa sababu kesi hizo zitakuwa kubwa hivyo majina ya
mashahidi yatakuwa yanahifadhiwa isipokuwa mshitakiwa anatakiwa kuyajua.
Aidha, alisema kanuni hizo zinaelekeza kuwa kesi ikifunguliwa ndani
ya siku moja, inapelekwa kwa jaji ambaye anaisikiliza na ndani ya siku
30 mahakama itafanya usikilizwaji wa awali.
“Tayari majaji 14 wameshateuliwa na kupata mafunzo kwaajili ya
kufanyakazi kwenye mahakama hiyo, pia katika kila Mahakama Kuu ya Kanda
kutakuwa na jaji ambaye atakuwa anashughulikia kesi zitakazokuwa
zinafunguliwa huko,” alisema.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment