LEO ni kilele cha maadhimisho ya miaka 52 ya Jeshi la Ulinzi la
Wananchi wa Tanzania (JWTZ). Kilele hicho kinafikia baada ya
shamrashamra za takribani wiki moja ya wapiganaji wa jeshi hilo
kushiriki kwa hali na mali shughuli za kijamii katika kona mbalimbali za
nchi.
Katika kipindi chote cha shamrashamra, askari wa jeshi hilo lenye
heshima kubwa barani Afrika, walishiriki uchangiaji wa damu katika
hospitali za jeshi hilo, lakini pia wameshiriki kufanya usafi na
upandaji miti katika kambi za jeshi na baadhi ya taasisi nchini.
Aidha, msemaji wa jeshi hilo, Kanali Ngemela Lubinga amesema katika
kilele cha Siku ya Majeshi leo, wananchi wametakiwa kuondoa hofu
watakapoona wanajeshi wakiwa katika shughuli mbalimbali mitaani,
baharini na angani.
Pia amewataka kwenda kupata huduma za tiba, kuchangia damu na hata
kushiriki kwa kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na jeshi hilo
lenye utamaduni wa kuisherehekea siku hiyo kila mwaka.
Katika maadhimisho hayo, JWTZ inayoadhimisha miaka 52 ya kuzaliwa
kwake Septemba 1964, ikichukua nafasi ya jeshi la Tanganyika Rifles
lililorithiwa na ukoloni wa Kiingereza, wananchi pia wanapata nafasi ya
kuangalia ubora wa jeshi letu lenye dhamana kubwa ya mipaka ya nchi hii.
Licha ya kuwa na majukumu ya ulinzi wa mipaka ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, kufanya mafunzo na mazoezi ili kujiweka tayari kivita
wakati wote na pia kufundisha umma shughuli za ulinzi wa Taifa, jeshi
hilo limekuwa mstari wa mbele kushirikiana bega kwa bega na wananchi.
Mara kadhaa majeshi ya ulinzi yamekuwa yakishirikiana na mamlaka za
kiraia katika kutoa misaada ya kibinadamu na uokoaji, kutoa huduma
mbalimbali za kijamii, kukuza elimu ya kujitegemea na uzalishaji mali
kupitia Jeshi la Kujenga Taifa na pia kushiriki ulinzi wa amani
kimataifa.
Hakika, katika miaka yote 52 ya uwepo wa jeshi hilo lenye Kamandi za
Nchi Kavu, Kamanda ya Jeshi la Majini na Kamandi ya Jeshi la Anga,
askari wake wamekuwa watiifu, wakitimiza vyema majukumu yao kwa
kushirikiana vyema na jamii ya Watanzania.
Kwa ujumla, wanastahili pongezi kwani wametuonesha mfano wa kuigwa
katika uwajibikaji, kuheshimu wengine kwa maana ya kudumisha urafiki
baina ya JWTZ, wananchi na taasisi mbalimbali.
Ndani ya jeshi, wapiganaji wake wamepata mafanikio makubwa, baadhi
yakiwa kusaidia nchi za kiafrika ambazo zilikuwa bado hazijapata Uhuru.
Lakini pia kupitia operesheni mbalimbali, limekuwa mfano wa kuigwa
katika kushiriki utoaji huduma wakati wa maafa ya Kitaifa, kushirikishwa
katika ujenzi wa Taifa (Jeshi la Kujenga Taifa) na Jeshi la Kujenga
Uchumi (Zanzibar) na pia ulinzi na wa amani.
Aidha, ilipata mafanikio makubwa kwa kuibuka na ushindi katika Vita
ya Kagera iliyopiganwa kwa takribani miezi kumi kuanzia Oktoba 25, 1978
hadi Julai 25, 1979.
Ni vita iliyokomesha ujeuri wa aliyekuwa Rais dikteta wa Uganda, Iddi
Amin aliyeingia madarakani kwa mabavu akimpindua Rais Milton Obote
mwaka 1971 na kuwatesa wote walimpinga, akifanya ubabe wake kwa
takribani miaka minane.
Baadaye alikusudia kuhamishia ubabe wake nje ya mipaka ya Uganda, kwa
kuvamia sehemu ya Tanzania mkoani Kagera, hatua iliyomlazimu Rais,
Mwalimu Julius Nyerere wa Tanzania kuamuru majeshi kutumika kumwondoa
kwa nguvu ndani ya mipaka ya Tanzania na kutoa adhabu kidogo.
Adhabu hiyo iliwafikisha wanajeshi hao ndani ya Uganda na mji wa
Kampala kutwaliwa Aprili 11, 1979 na Amin kulazimika kukimbilia Libya,
halafu Irak na mwishowe Saudia alikopewa kimbilio kwa masharti ya
kutoshughulikia siasa tena.
Tangu wakati huo, Makamanda na Wapiganaji wa JWTZ wamezidi kuwa na
uelewa wa wajibu wao kwa taifa, lakini pia wakiwa na mshikamano kitaifa
kuanzia ngazi zote. Hakika katika hilo jeshi limefanikiwa sana.
Tukiiga mfano wa wapiganaji wa JWTZ katika uwajibikaji, kwa maana ya
kila mmoja kutimiza wajibu wake, hakika Tanzania tunayoitaka itazidi
kupata mafanikio.
Na kila mmoja atimize wajibu wake kwa staili ya ushirikiano, juhudi
na maarifa mithili ya wapiganaji shupavu wa majeshi yetu yanayoadhimisha
miaka 52 ya kuzaliwa.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment