Maelfu
ya waombolezaji na viongozi wa kimataifa walikusanyika Israel kumzika
Rais wa zamani wa nchi hiyo Shimon Peres ambaye alitajwa kama kiongozi
aliyechangia katika juhudi za amani Mashariki ya Kati.
Ni mazishi
yaliohudhuruwa na viongozi mbali mbali wa kimataifa huku rais Barrack
Obama wa Marekani na aliyekuwa rais wa nchi hiyo Bill Clinton pamoja na
rais wa Palestina Mahmoud Abbas wakiongoza orodha kubwa ya viongozi hao
wa kimataifa waliokongamana katika eneo la makaburi ya kitaifa nchini
Israel la mlima Herzl kwa mazishi hayo.
Waziri mkuu wa Israel
Benjamin Netanyahu amesema kuwa ujumbe huo wa viongozi mbali mbali wa
kimataifa ni ishara ya wazi ya upendo aliokuwa nao Shimon Peres,
matumaini na kiu cha amani na mapenzi kwa nchi yake Israel. Alikuwa mtu
aliyependwa na Israel na aliyependwa pia na ulimwengu aliongeza kusema
Benjamin Netanyahu. "Leo ninakulilia. Nilikupenda, sote tulikupenda.
Kwaheri Shimon, mtu mzuri, kiongozi mashuhuri. Tutakuweka ndani ya moyo
wa taifa letu na ninachukua nafasi hii kusema kuwa utakumbukwa katika
mioyo ya mataifa yote," alisema Netanyahu.
Rais Barack Obama
aliyekuwa na uhusiano wa karibu na marehemu Peres, alisema kuwa hakuna
kiongozi aliyetekeleza mengi zaidi ya Peres katika kuimarisha uhusiano
kati ya Marekani na Israel. Kadhalika Obama ametilia mkazo suala la
amani akisema kuwepo katika maziko hayo, rais wa mamlaka ya Wapalestina
kunaonesha haja ya kuliangalia suala la amani Mashariki ya Kati. "Ni
hesima kubwa kwangu kuwa Jerusalem kumuaga rafiki yangu Shimon Peres,
aliyetuonyesha kuwa haki na matumaini ndiyo kiini cha maadili ya
Kiyahudi."
Kiongozi aliyeshika vyeo vingi
Bill Clinton alimtaja
Peres kuwa mtu aliyekuwa na ndoto kubwa. Aliongeza kuwa Peres alianza
kwa kuwa mwanafunzi mwerevu zaidi nchini Israel, mwalimu bora zaidi na
hatimaye kumalizia kwa kuwa mwenye maono makubwa kwa taifa la Israel na
kwamba aliishi maisha yake ya miaka 93 kufikiria jinsi kila mmoja
alivyoweza kutumia uwezo wake kikamilifu na kwamba watu wanapaswa
kujiepusha na hofu na kuishi kila siku kikamilifu huku kukiwa na
matumaini ya kesho.
Watoto wa Peres pia walimtaja baba yao kama mtu
aliyekuwa na upendo kwa familia yake. Bintiye Tzvia Walden alisema kuwa
babake alipenda kujifunza mambo mbali mbali na kupata elimu mpya kila
mara .
Mwanawe wa kiume alichekesha waombolezaji aliposema kuwa
wakati babake alipowahi kuulizwa angetaka aandikiwe ujumbe gani juu ya
kaburi lake, babake alimjibu kuwa yeye ni mchanga sana kufariki.
Peres
aliwahi kuwa Rais, Waziri Mkuu na waziri wa mashauri ya nchi za kigeni
wakati wa uhai wake katika safari yake ya kisiasa.
Alifariki mapema wiki akiwa na umri na umri wa miaka 93 kutokana na ugonjwa wa kiarusi.
Home
Kimataifa
Slider
Maelfu ya waombolezaji na viongozi wa kimataifa wamzika Rais wa zamani wa nchi hiyo Shimon Peres.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment