Image
Image

Magufuli:Ndani ya mwezi huu, wafanyakazi wa UHURU walipwe mishahara yao milioni 609.

RAIS John Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), amefanya ziara ya kushitukiza katika ofisi za gazeti la Uhuru, mali ya chama hicho tawala na kuagiza ndani ya mwezi huu, wafanyakazi walipwe mishahara yao wanayodai inayofikia Sh milioni 609. Aidha, ameagiza kupatiwa orodha ya taasisi za serikali zinazodaiwa na Magazeti ya Uhuru na Mzalendo, na pia ameagiza deni linalodaiwa na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) kutokana na kutowasilishwa kwa makato ya wafanyakazi lilipwe.
Katika mazungumzo yake na wafanyakazi kwenye ofisi hizo zilizopo Mtaa wa Lumumba jijini Dar es Salaam, wafanyakazi wamelalamikia kutolipwa mishahara yao kwa miezi saba, kutotolewa kwa michango ya wafanyakazi kwa NSSF, kuuzwa kwa mtambo wa kuchapisha magazeti katika hali ya kutatanisha, kutotambuliwa katika ajira kwa baadhi ya wafanyakazi, kutolipwa kwa madeni wanayozidai taasisi za Serikali na wanaostaafu kutolipwa mafao yao.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, wafanyakazi hao pia wamemueleza Dk Magufuli kuwa Bodi na Menejimenti ya Kampuni ya vyombo vya habari vya chama inayoendesha gazeti la Uhuru na Redio Uhuru, zimeshindwa kuendesha vyombo hivyo na wamemuomba aingilie kati ili kuvinusuru, ambavyo kwa sasa vina hali mbaya kutokana na kukabiliwa na madeni makubwa, na biashara yake imeshuka kwa kiasi kikubwa.
Akijibu malalamiko hayo, Rais Magufuli aliyetembelea ofisi za Uhuru akitokea ofisini kwake katika jengo la Makao Makuu ya CCM Ofisi Ndogo Lumumba, amemuagiza Katibu Mkuu wa CCM,
Abdulrahman Kinana kuhakikisha mishahara yote wanayodai wafanyakazi inayofikia Sh milioni 609, inalipwa ndani ya mwezi huu wa tisa, ameagiza kupatiwa orodha ya taasisi za serikali zinazodaiwa na magazeti ya Uhuru na Mzalendo, na ameagiza deni linalodaiwa na NSSF kutokana na kutowasilishwa kwa makato ya wafanyakazi lilipwe.
Kuhusu malalamiko dhidi ya Bodi na Menejimenti ya kampuni hiyo, ajira za wafanyakazi, mafao kwa wastaafu, kuuzwa kwa mtambo wa kuchapisha magazeti na mazingira magumu ya kazi, Dk Magufuli ameahidi kuyafanyia kazi.
Aidha, Dk Magufuli aliwapongeza wafanyakazi wa gazeti la Uhuru kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya licha ya kukabiliwa na changamoto kubwa na amewahakikishia kuwa anatambua umuhimu wao na kwamba atahakikishia anaboresha hali ya chombo hicho muhimu.
Wakati huo huo, Rais Magufuli amemjulia hali Spika mstaafu wa Bunge, Samuel Sitta ambaye anaendelea kupata matibabu jijini Dar es Salaam na hali yake inaendelea vizuri.
Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment