MWENYEKITI wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa
Arusha, Lengai ole Sabaya (29) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu
Mkazi Arusha kwa makosa miwili, ikiwemo kujifanya mtumishi wa umma
katika Idara ya Usalama wa Taifa (TISS).
Sabaya alifikishwa mahakamani hapo jana akitokea Polisi kisha kuwekwa mahabusu kwa muda na kusomewa mashtaka hayo miwili.
Akimsomea mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo,
Gwantwa Mwankuga, Wakili wa Serikali Lilian Mmassy alidai kuwa kosa la
kwanza linalomkabili Sabaya ni la kujifanya mtumishi wa umma ambapo Mei
18, mwaka huu katika Hoteli ya Skyway iliyopo Makao Mapya jijini Arusha
alijifanya kuwa mwajiriwa wa TISS.
Kosa la pili ilidaiwa kuwa katika siku isiyofahamika wala tarehe
mwaka huu, alighushi nyaraka za kitambulisho cha Usalama wa Taifa chenye
picha yake na kutumia namba Saturday. Code. Eagle 3 Idara ya Usalama wa
Taifa chenye namba MT. 86117.
Hata hivyo, Sabaya alikana makosa hayo, na Wakili wa Serikali, Mmassy
alidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na dhamana ya mshtakiwa ipo
wazi. Wakili wa mshitakiwa, Yoyo Asubuhi alimwomba Hakimu Mwankuga
kumpa dhamana mteja wake kwa kuwa ni haki yake ya msingi.
Hakimu Mwankuga alisema kwa kuwa dhamana ipo wazi anampa masharti
Sabaya ambayo ni kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika ikiwemo kusaini
hati ya dhamana ya Sh milioni tatu kwa wadhamini wawili kila mmoja.
Wadhamini hao walikidhi masharti ya dhamana ya Sabaya na hatimaye
kuachiwa kwa sharti la kufika mahakamani kila tarehe ya kesi yake na
endapo atapata udhuru atoe taarifa mahakamani kupitia kwa wadhamini hao.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Oktoba 5, mwaka huu.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment