Mahakama
Kuu imekana kuitambua kampuni ya Fosters Auctioneers and General
Traders iliyohusika kuondoa vitu vya kampuni za Freeman Mbowe kwenye
jengo la Shirika la Taifa la Nyumba (NHC).
Hayo yalibainishwa jana na
kiongozi wa jopo la mawakili wanaomtetea Mbowe ambaye pia ni mwenyekiti
wa Chadema, Peter Kibatala wakati wa usikilizwaji wa maombi
yaliyofunguliwa na mlalamikaji huyo kupitia kampuni ya Mbowe Hotels Ltd
dhidi ya NHC na kampuni hiyo ya udalali.
Wakati wa usikilizwaji wa
maombi hayo jana, pamoja na mambo mengine Mbowe aliiomba Mahakama
iliamuru NHC na kampuni hiyo wamrejeshe katika jengo hilo pamoja na
vifaa na mali zake zinazoshikiliwa na kampuni hiyo.
Wakili Kibatala aliieleza Mahakama kuwa mteja wake aliondolewa katika jengo hilo kinyume na sheria.
Alidai
dalali aliyetumiwa na NHC kuziondoa kampuni za Mbowe katika jengo hilo
hajasajiliwa na Mahakama kwa kuwa walimwandikia Msajili wa Mahakama
barua kujua kama anatambulika, lakini alijibu kuwa haimtambui.
Kutokana
na majibu ya msajilihuyo kupitia barua yake ambayo wameiwasilisha
mahakamani kama kielelezo, Kibatala alidai sheria na mchakato mzima
uliotumika vilikuwa ni batili.
Mawakili wa NHC, Ipilinga Panya na
Aloyce Sekule walidai shirika hilo kabla ya kumtimua Mbowe lilimwandikia
notisi ya siku 30 iliyokwisha kisha akaongezewa siku 30 zingine kama
sheria inavyotaka ambazo ziliisha na kumpa tena siku 14, lakini hakulipa
deni.
Wakili wa kampuni ya Foster Auctioneers and General Traders,
Aliko Mwamanenge alidai madai ya kuwa mteja wake ni dalali wa Baraza la
Usuluhishi na kwamba anayesajiliwa kama dalali ni mtu binafsi na siyo
kampuni, hayana ukweli kwani upande wa mlalamikaji ulipoandika barua
kuulizia uhalali wake ulipaswa kuuliza jina la mmiliki kampuni hiyo.
Hata
hivyo, wakili wa mlalamikaji Kibatala alidai notisi zinazodaiwa
kuandikwa na NHC zilipelekwa mahali pasipohusika kwa kampuni ya Free
Media badala ya Mbowe Hotels ambayo ina mkataba na NHC. Baada ya
kusikiliza hoja za pande zote, Jaji Sivangilwa Mwangesi anayesikiliza
kesi hiyo aliiahirisha hadi Oktoba 18, mwaka huu atakapotoa uamuzi wa
maombi hayo ya mlalamikaji.
Septemba Mosi, wafanyakazi wa kampuni ya
udalali ya Foster Auctioneers and General Traders walifika kwenye ofisi
za kampuni ya Free Media na kuondoka vifaa mbalimbali vya kazi, zikiwamo
kompyuta na viti kwa madai kwamba mmiliki wake, Mbowe anadaiwa na NHC
fedha nyingi za kodi ya pango.
Chanzo: Mwananchi
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment