WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewasimamisha kazi Maofisa Misitu wanne na
kusimamisha shughuli za uvunaji wa mazao ya misitu wilayani Rufiji kwa
muda usiojulikana baada ya kutoridhishwa na usimamizi wake.
Maofisa
waliosimamishwa kazi ni pamoja na Mkuu wa Idara ya Ardhi, Maliasili na
Mazingira Dk. Paul Ligonja, Ofisa Misitu wilaya Gaudens Tarimo, Ofisa
Misitu Yonas Nyambuya na Ofisa wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) wa
wilaya Seleman Bulenga.
Waziri Mkuu amefanya uamuzi huo leo
(Jumatatu, Septemba 26, 2016) wakati akizungumza na watumishi wa wilaya
ya Rufiji kwenye ukumbi wa halmashauri kabla ya kuzungumza na wananchi
katika mkutano wa hadhara kwenye viwanya jumba la maendeleo wilayani
Rufiji.
Aidha, Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu wa Wilaya hiyo, Juma
Njwayo kukusanya magogo yoye yaliyoko msituni na kuyapiga mnada na
kuitaka wizara ya Maliasili na Utalii kwenda wilayani Rufiji kufanya
uchunguzi wa leseni za uvunaji walizozitoa kwa wilaya hiyo.
Waziri
Mkuu amebainisha kwamba wilaya ya Rufiji ni moja kati ya wilaya
inayoongoza kwa uvunaji wa mazao ya misitu bila ya kufuata taratibu
licha ya kuwa na maofisa misitu.
“Hakuna mafanikio katika sekta ya
misitu kwenye wilaya hii ya Rufiji. Nasimamisha shughuli zote za uvunaji
wa mazao ya misitu pamoja na watendaji wake kwa sababu hatuwezi kuacha
watu wanakata magogo bila ya kufuata taratibu,”
“Haiwezekani Rufiji
iwe shamba la bibi, nimesimamisha uvunaji wa magogo hata kwa wenye
leseni hadi tuzichunguze zimetoka wapi. Hatuwezi kuruhusu maofisa
wanashiriki vitendo vya hujuma kwa kuvuna misitu Rufiji na kugonga
mihuli ya Kilwa kisha fedha wanatia mifukoni,” amesema.
Wakati huo
huo Waziri Mkuu amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya hiyo
Rashid Salum kufuatilia maagizo aliyoyatoa kuhusu kizuizi cha Ikwiriri
kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe alipokutana na
watumishi wa wizara hiyo.
Julai 18 mwaka huu Waziri Mkuu alikutana
na watumishi wa wizara hiyo jijini Dar es Salaam na kusisitiza kwamba
hakuna sababu ya Serikali kuendelea kuwa na watumishi wasiokuwa na
uaminifu, uadilifu na uwajibikaji.
Waziri Mkuu aliitaka wizara hiyo
kupunguza idadi ya vizuizi vya ukaguzi wa mazao ya misitu kwenye
barababara mbalimbali baada ya kukosa tija, alitoa mfano wa barabara ya
kwenda mikoa ya kusini kuanzia Dar es Salaam yenye vizuizi
visivyopungua sita na kila kizuizi kinatumika kwa ajili ya kukagua mazao
ya misitu na maliasili inayotoka kuvunwa.
Awali mbunge wa Rufiji
Mohammed Mchengelwa alilalamikia vitendo vya dharau vinavyofanywa na
watumishi wa sekta mbalimbali katika wilaya hiyo jambo linalosababisha
wananchi kukosa imani na Serikali yao.
Home
News
Slider
Majaliwa awasimamisha kazi Maofisa Misitu wanne wilayani Rufiji kwa muda usiojulikana.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment