Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mwigulu Lameck
Nchemba amesema hakuna shamba lenye thamani ya maisha ya binadamu na kuwataka
wakulima na wafugaji kutatua migogoro yao kwa kufuata sheria na kuacha
kujichukulia sheria mkononi.
Mwigulu ameyasema hayo Bungeni leo wakati akijibu
swali la nyongeza kutoka kwa Mbunge wa Mikumi kupitia (CHADEMA) Joseph Haule
aliyetaka kujua hatua za serikali katika kudhibiti mauaji ya wakulima na
wafugaji yanayotokea mara kwa mara katika jimbo lake na maeneo mengine nchini.
Katika swali lake Mbunge Haule ametaja baadhi ya
mifano ya mauaji katika jimbo lake hususani eneo la Tindiga ambapo mauaji
yamekuwa yakifanyika mara kwa mara huku serikali ikitoa matamko ambayo
hayajazaa matunda.
Waziri Mwigulu Nchemba amesema katika kijiji ambacho
mauaji yatafanyika jeshi la polisi litakamata vijana wote wenye nguvu na
kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria ili wahusika waweze kubainika.
“Naliagiza Jeshi la Polisi kuwakamata vijana wote
wenye nguvu katika kijiji ambacho mauaji yatafanyika ili wahusika wapatikane na
kama magereza zikijaa vibaka walioiba vitu vidogovidogo waachiwe ili hao ambao
wamesababisha mauaji wawekwe humo hatuwezi kufananisha maisha ya binadamu na
mifugo au shamba” Amesema Waziri Mwingulu.
Awali katika swali hilo Naibu Waziri wa Kilimo
Mifugo na Uvuvi Dkt. William Ole Nasha amewataka wafugaji na wakulima kuepuka
kutumia hasira ambazo zinapelekea kugharimu maisha ya watu kwani serikali
haitasita kuwachukulia hatua kali za kisheria.
0 comments:
Post a Comment