Image
Image

Posho serikalini zilipwe kwa kufuata taratibu


MOJA ya hatua zinazochukuliwa na serikali hivi sasa, ni pamoja na kufuta posho ambazo hazina umuhimu.
Serikali pia inazipunguza posho zingine ambazo zinalipwa bila kufuata taratibu. Lengo la hatua hiyo ni moja ya mkakati wa kubana matumizi.
Huko nyuma inaonekana kwamba kulikuwapo na udhaifu wa kutosimamia ulipaji wa posho kwa viongozi wa kisiasa na watumishi wa umma, ili kuhakikisha kwamba ulipaji wake unafuata taratibu na kanuni za malipo ya serikali.
Mkakati wa kudhibiti ulipaji wa posho serikalini umegusa idara na taasisi zote za umma, huku baadhi ya walioathiriwa wakilalamika.
Ulipaji wa posho ni moja ya mambo ambayo yaliisababisha serikali itumie fedha nyingi za umma bila sababu kwa kuwa hazikuwa na tija.
Kibaya zaidi ni kwamba posho ziligeuzwa kuwa sehemu ya ulaji wa watumishi na baadhi ya viongozi. Ndiyo maana safari na vikao visivyo na tija yalikuwa maisha ya kila siku.
Halmashauri ya Jiji la Arusha ni moja ya maeneo yaliyotikishwa na uamuzi wa kudhibiti posho, baada ya Mkurugenzi wake, Athumani Kihamia, kufuta kabisa baadhi ya posho walizokuwa wanalipwa madiwani na watendaji pamoja na kupunguza nyingine.
Kihamia anasema kuwa madiwani walipitisha uamuzi wa kulipana posho hizo bila kufuata kanuni na taratibu za Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) huku wao wakijitetea kuwa viwango hivyo vilipitishwa muda mrefu na wao walivikuta.
Wiki iliyopita, Kihamia alipunguza posho ya nauli kwa madiwani kutoka Sh. 80,000 kwa kila kikao hadi Sh. 10,000 kwa kila mmoja.
Pia, alifuta posho ya mafuta ya Sh. 100,000 na posho ya vocha ya simu ya Sh. 150,000 kwa mwezi kwa kila diwani.
Kabla ya uamuzi wa wiki iliyopita, Mkurugenzi huyo alishafuta posho ya Sh. milioni moja aliyokuwa akilipwa meya na mkurugenzi kila siku ya kitaifa, kwa ajili ya kuwakirimu wageni.
Kwa mujibu wa Kihamia, zaidi ya Sh. milioni 40.8 zimeshalipwa kwa madiwani hao na fedha hizo zinapaswa kurejeshwa katika halmashauri.
Kihamia anastahili pongezi kwa hatua hiyo na anapaswa kuwa mfano wa kuigwa na wakurugenzi wote wa halmashauri pamoja na wakuu wote wa idara, taasisi, wakala na mashirika ya serikali.
Tunasema hivyo kwa kuwa kote huko posho zinalipwa kiholela na kinyume cha taratibu na kanuni, badala ya fedha hizo kutumika kwa ajili ya shughuli za maendeleo.
Kuna wakati ulizuka mjadala mkali nchini ambao watu walikuwa wakihoji sababu za wabunge kulipwa posho nyingi na viwango vikubwa. Hata hivyo, kuna hatua zilichukuliwa za kuzuia wabunge wasilipwe chochote pale wanapotembelea miradi ya sekta zinazofuatiliwa na kamati zao.
Pamoja na mkakati wa serikali wa kudhibiti ulipaji wa posho ili uzingatie taratibu na kanuni, kuna haja ya kuangalia upya utaratibu wa kuwalipa madiwani stahiki zao.
Itakumbukwa kuwa madiwani ambao ni wawakilishi wa wananchi hawalipwi mshahara, hivyo kuishi kwa kutegemea posho. Hali hiyo inawafanya washinikize kulipwa viwango vikubwa vya posho.
Kutokana na kufanya kazi katika mazingira magumu ya kuhudumia watu wengi katika maeneo makubwa ya kata, kuna haja kwa serikali kuanzisha utaratibu wa kuwalipa mishahara madiwani ili kuwaondolea vishawishi na kutekeleza majukumu yao kwa tija na ufanisi.

Share on Google Plus

Kuhusu TAMBARARE HALISI

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment