RAIS John Magufuli ametoa siku saba kwa taasisi zote za serikali
zinazodaiwa malimbikizo ya kodi na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC),
kuhakikisha zinalipa madeni yao, vinginevyo mali zao zitatolewa nje.
Dk Magufuli amemtaka Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Nehemia Mchechu
kutomuogopa mtu yeyote awe Rais, Waziri, CCM, Chadema au kiongozi
yeyote wa serikali endapo hajalipa pango lake la nyumba, atolewe nje
mali zake.
Pamoja na hayo, mkuu wa nchi amewaahidi wakazi 644 wa eneo la
Magomeni Kota, Kinondoni, Dar es Salaam kuwa ndani ya miezi miwili
ujenzi wa nyumba za kisasa utaanza katika eneo hilo, na ndani ya mwaka
mmoja ukishakamilika, wakazi hao watakuwa wa kwanza kupatiwa nyumba
hizo.
Akizungumza na wazee waliokuwa wakazi wa eneo la Magomeni Kota jijini
Dar es Salaam jana, Rais Magufuli alisema tayari ameshatoa maagizo kwa
taasisi zozote za serikali ikiwemo wizara zinazodaiwa na NHC,
kuhakikisha zinakamilisha kulipa madeni yao ndani ya siku saba.
“Wasipolipa nakuagiza bwana Mchechu watolee nje mali zao kama
ulivyomtolea nje yule jamaa. Usiogope mtoe mtu yeyote asiyelipa pango
hata kama ni serikali, waziri, Ukawa, Rais au CCM. Lazima watu hawa
wakulipe ili upate fedha za kuliendesha shirika hili,” alisisitiza Rais
Magufuli.
Aliwataka wapangaji wote wa shirika hilo kuhakikisha wanalipa fedha
za pango la nyumba na endapo wapo ambao hawajalipa wajiandae kuondoka
kwenye nyumba hizo.
“Nashangaa eti hawa wa serikalini wanashindwa kulipa pango la nyumba
kwa NHC, lakini fedha za safari za nje wanazo kila kukicha, wanaomba
vibali vya kusafiri na kulipana posho,” alisema na kuongeza kuwa endapo
shirika hilo litazitolea nje baadhi ya taasisi na wizara za serikali kwa
kushindwa kulipa kodi, itakuwa ni vyema kwa kuwa sasa taasisi hizo
zitaenda moja kwa moja Dodoma kwa ajili ya kuwahudumia wananchi
kikamilifu.
Hivi karibuni, Mchechu alitoa mwezi mmoja kwa kampuni 29 za taasisi
mbalimbali za serikali zilizokwepa kulipa madeni yake kwa shirika hilo
la nyumba la Taifa.
Miongoni mwa taasisi hizo zinazoongoza kudaiwa na NHC madeni ambayo
yamefikia zaidi ya Sh bilioni tisa ni pamoja na Ofisi ya Rais inadaiwa
zaidi ya Sh milioni 10 na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
inadaiwa zaidi ya Sh bilioni mbili.
Taasisi nyingine ni Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
inayodaiwa zaidi ya Sh bilioni moja; Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto inadaiwa zaidi ya Sh bilioni moja; Wizara ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inadaiwa Sh milioni 613
na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inadaiwa Sh milioni 360.
Mchechu alisema pamoja na deni hilo, wapo taasisi na watu binafsi
akiwamo Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),
Freeman Mbowe ambaye hivi karibuni mali zake zilitolewa nje kwa
kushindwa kulipa deni lake.
Mbowe anayeendesha Club Bilicanas iliyoko maeneo ya Posta, Dar es Salaam anadaiwa zaidi ya Sh bilioni 1.1.
Awali akizungumzia mgogoro wa ardhi katika eneo la Magomeni Kota, Dk
Magufuli aliwatoa machozi wakazi wa eneo hilo baada ya kuwaahidi
kuwatimizia makubaliano yao waliyoingia na halmashauri ya manispaa ya
Kinondoni miaka mitano iliyopita.
Alisema ahadi ya ujenzi wa nyumba za kisasa katika eneo hilo, itaanza
kutekelezwa ndani ya miezi miwili na ujenzi wa nyumba hizo utakamilika
ndani ya mwaka mmoja ambapo wakazi hao 644 watapatiwa nyumba za kuishi
watakazoishi kwa muda wa miaka mitano bure.
“Kwanza nawaomba radhi kwa usumbufu mkubwa mliopitia, haingii akilini
muondolewe kwenye nyumba zenu kwa ahadi ya kujengewa nyumba mpya na
kulipwa pango, bila kutimiziwa. Mlinichagua mimi Magufuli kuwa Rais
wenu, sasa nasema kuanzia sasa mateso kwenu tena basi,” alisema.
Alisema wakazi hao waliotaabika kufuatilia haki yao mahakamani kwa
muda wa miaka mitano tangu mwaka 2012 walipotolewa kwenye nyumba hizo,
watapatiwa nyumba hizo za kisasa kulingana na taarifa zao na orodha ya
majina yao ambayo Rais huyo anayo.
Alisema eneo hilo la ekari 33 sasa litajengwa nyumba hizo za kisasa
yakiwemo maghorofa, ofisi na maeneo ya biashara kadri atakavyoshauriana
na NHC na Wakala wa Majengo (TBA).
Kauli hiyo ya Magufuli iliamsha shangwe na vilio vya furaha miongoni
mwa wakazi hao waliokusanyika katika mkutano huo, ili kujua hatma yao
huku wengine, wakimuombea kwa sauti Rais huyo wakitaka Mungu amlinde
azidi kutetea wanyonge.
“Naenda kupanga mikakati, nitatoa fedha za serikali mwezi huu ili
mkandarasi atakayepatikana aanze kujenga nyumba hizi. Wakati wakiendelea
kujenga nyumba hizi, maeneo mengine pia nayo yataendelea kujengwa ili
kuendeleza zaidi eneo hili,” alisisitiza.
Alisema lengo la Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha Jiji la Dar
es Salaam linakuwa jiji la kisasa la kibiashara ambalo wakazi wake wote
wanakuwa na makazi bora bila kujali kipato chao.
Aidha, Rais Magufuli alisema aliamua kumteua Mkurugenzi wa Manispaa
ya Kinondoni, Aron Kagurumjuli kuongoza manispaa hiyo ili apambane na
vitendo vichafu vya uonevu wa ardhi na kudhibiti wale matajiri wanaotaka
kuchukua maeneo ya wazi kwa faida zao binafsi.
“Hali ilikuwa mbaya, ndio maana watu walitaka kujimilikisha hadi
fukwe, walibakisha kidogo tu wajiuzie ikulu. Nimechagua viongozi wa mkoa
wa Dar es Salaam kwa makusudi kabisa, ninataka mabadiliko ya kweli
katika jiji hili,” alifafanua.
Naye Msemaji wa Wakazi wa Magomeni Kota, Mchungaji John Raymond
alisema wakazi hao walikubaliana na Manispaa ya Kinondoni, wapishe
ujenzi wa nyumba za kisasa katika eneo hilo tangu mwaka 2012 na baada ya
ujenzi huo kukamilika watapangishwa na kuuziwa nyumba hizo.
Aidha, alisema pia walikubaliana katika kipindi chote ambacho ujenzi
huo unaendelea, manispaa hiyo iliahidi kuwalipa wakazi hao pango la
nyumba, ahadi ambayo hadi sasa haijatimizwa na hivyo kusababisha wakazi
hao kuidai manispaa hiyo kiasi cha Sh milioni 4.3 kila mmoja.
Alisema kwa niaba ya wakazi hao wanamuomba Dk Magufuli serikali
iwajengee nyumba wakazi hao za bei nafuu, kwani kitendo cha kuondolewa
kwao kwenye nyumba za kota bila malipo yoyote kimesababisha vifo vya
wazee 15 baada ya kupatwa na shinikizo la damu.
Naye Mwenyekiti wa Wazee wa Magomeni Kota, Mwajuma Sama, aliangua
kilio mbele ya Rais wakati akitoa shukurani kutokana na uamuzi wa
kiongozi huyo wa kuwapatia nyumba za kisasa wakazi hao na kuwapa muda wa
miaka mitano kukaa bure kwenye nyumba hizo.
“Mungu akulinde baba, tumetolewa kwenye nyumba hizi nikiwa na miaka
64, leo nina miaka 70 napata matumaini. Nakuombea Mungu akusimamie baba
uishi miaka mingi,” alisema mwanamama huyo, huku akilia kwa sauti hali
iliyozua vilio pia kwa akinamama wenzake waliokuwepo kwenye mkutano huo.
Kwa upande wake, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
William Lukuvi, alikiri kuwa mgogoro huo ni muda mrefu kwani nyumba hizo
zilikuwa chini ya Serikali za Mitaa na bvaadaye NHC lakini kutokana na
kushindwa kuziendeleza kama ilivyokubaliwa ardhi hiyo ilirejeshwa
serikali kuu.
“Na nyumba zote alizoniagiza Rais Magufuli zenye migogoro ya aina hii
nimeshaandaa tangazo la serikali (GN) zote zitarejeshwa kwanza kwa
serikali kuu,” alisema.
Alisema tangu awe waziri wa ardhi, ameshuhudia migogoro mingi ya
ardhi na mingi ikitokana na ufisadi wa maofisa ardhi hali iliyosababisha
apime viwanja 600 maalumu kwa ajili ya kuwalipa fidia wananchi wote
waliodhulumiwa ardhi na maofisa hao.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, aliwashukia wale wote
wanaomkashifu Dk Magufuli kwa kumuita dikteta kutokana na maamuzi
anayoyatoa na kusisitiza maamuzi yote ya Rais huyo yamelenga kuondoa
kero za wanyonge.
Alisema tangu Rais huyo atangaze kuijenga barabara ya Mwenge-Morocco,
kuagiza ndege mpya za Serikali na ujenzi wa mahakama ya mafisadi,
kumekuwa na madai mengi ya kumvunja moyo, hali ambayo wananchi wanapaswa
kutoiunga mkono.
“Mheshimiwa Rais unaposikia mawimbi na dhoruba zinapiga mchana usiku
ujue Mungu hajalala, itafikia wakati wasaidizi wako nikiwemo mimi
tutakukimbia utabaki mwenyewe, usikate tamaa jua Mungu hajalala. Rais
anapochukua uamuzi wa kurejesha eneo kwa wanyonge kuna watu tu
hawatafurahia hatua hii,” alisema.
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment